WHO: Mambo matano muhimu ya kufahamu kuhusu Ukoma
WHO: Mambo matano muhimu ya kufahamu kuhusu Ukoma
Dunia ikiadhimisha Siku ya Ukoma Duniani Januari 25 Januari Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema ukoma ni ugonjwa unaotibika na unaweza kuzuilika, lakini bado unaathiri mamia ya maelfu ya watu kila mwaka.
Mkakati wa WHO wa kutokomeza ukoma unalenga utambuzi wa mapema, utoaji wa tiba ya mchanganyiko wa dawa (MDT) bila malipo, kinga, kupunguza unyanyapaa, na kuimarisha mifumo ya afya.
Pia limesisitiza kuwa ushirikiano endelevu wa kimataifa na utashi wa kisiasa ni muhimu ili kutoka katika kuutokomeza ukoma kama tatizo la afya ya umma hadi kukomesha kabisa maambukizi na kufikia lengo la kutokuwa nak isa chochote cha ugonjwa huo, bila kuwa na ulemavu, na na bila unyanyapaa.
Cha kufahamu kuhusu Ukoma
1. Ukoma ni ugonjwa sugu wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria
Kwa mujibu wa WHO ugonjwa huu husababishwa na Mycobacterium leprae, ambao huathiri zaidi ngozi na mishipa ya pembeni ya mwili. Usipotibiwa, unaweza kusababisha ulemavu unaoendelea au wa kudumu.
2. Huaambukiza kupitia ukaribu wa muda mrefu na wagonjwa wasiotibiwa
Bakteria huenea kupitia matone kutoka puani na mdomoni wakati wa mawasiliano ya karibu na ya kudumu. Mtu mwenye ukoma huacha kuambukiza mara tu anapoanza matibabu yenye ufanisi.
3. Ukoma unatibika kwa tiba ya mchanganyiko wa dawa (MDT)
WHO inapendekeza na kuwezesha matibabu kwa kutumia mchanganyiko wa dawa za viuavijasumu au antibiotiki (dapsone, rifampicin, clofazimine) na hutoa MDT bila malipo kwa wagonjwa kote duniani. Utambuzi wa mapema na matibabu huzuia ulemavu.
4. Ukoma bado upo licha ya kutokomezwa kama tatizo la afya ya umma
Ugonjwa huu bado unapatikana katika zaidi ya nchi 120, kwa mujibu wa takwimu za WHO huku takribani visa vipya 175,000–200,000 vikisajiliwa kila mwaka na nchi za Brazil, India na Indonesia zikiripoti idadi kubwa zaidi.
5. Kutokomezwa kama tatizo la afya ya umma kumeafikiwa kimataifa, lakini kukomesha maambukizi bado ni kipaumbele
WHO imefafanua kutokomezwa kwa ugonjwa huo ni kama kuwa na kiwango cha chini ya kisa 1 kwa kila watu 10,000. Lengo hili lilifikiwa duniani mwaka 2000, na katika nchi nyingi ilipofika 2010, lakini maambukizi bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo yenye maambukizi mengi.
Nini kinaweza kufanyika kutokomeza Ukoma
Mkakati wa kimataifa wa WHO unachanganya mbinu za kitabibu, ufuatiliaji, kinga, na hatua za kijamii. Vipengele muhimu ni pamoja na:
1. Kugundua kila kisa mapema na kutoa matibabu bila malipo
Kuhakikisha utambuzi na tiba ya mchanganyiko wa dawa (MDT) vinapatikana kwa urahisi katika vituo vyote vya afya, hasa katika maeneo yenye maambukizi. WHO inaunga mkono usambazaji wa MDT bila malipo duniani kote tangu mwaka 2000.
2. Kupanua hatua za kinga
WHO inasisitiza kuwa ufuatiliaji wa watu waliokaribu na wagonjwa na kinga baada ya kuambukizwa (PEP) kwa kutumia dozi moja ya rifampicin kwa waliowasiliana na wagonjwa waliothibitishwa husaidia kupunguza maambukizi.
3. Kupambana na unyanyapaa na ubaguzi
Kushughulikia vikwazo vya kijamii vinavyowazuia watu kutafuta huduma za afya. Mkakati wa sasa wa WHO, kuelekea kutokuwa na ukoma kabisa: mkakati wa kimataifa wa ukoma 2021–2030, unasisitiza kupunguza unyanyapaa kama nguzo kuu.
4. Kuimarisha ufuatiliaji na mifumo ya afya
Mifumo imara ya ufuatiliaji na huduma za afya zilizounganishwa ni muhimu ili kuhakikisha ugunduzi wa mapema wa visa na uendelevu wa muda mrefu, hata pale maambukizi yanapokuwa machache sana.
5. Kudumisha utashi wa kisiasa na ushirikiano
Dhamira endelevu ya kisiasa, ushiriki wa jamii, na ushirikiano wa kimataifa ni muhimu ili kuendeleza mafanikio na kusukuma juhudi za kukatiza kabisa maambukizi.
Nukuu kutoka kwa viongozi wa WHO na washirika kuhusu Ukoma
Kauli hizi zinaakisi dharura na ari ya ushirikiano nyuma ya juhudi za kimataifa:
• Dkt. Jeremy Farrar, Mkurugenzi Msaidizi Mkuu wa WHO:
“Dhamira isiyoyumba ya washirika kama Novartis kwa kipindi cha robo karne imekuwa msingi wa maendeleo yaliyopatikana dhidi ya ukoma. Msaada wao thabiti katika kuhakikisha upatikanaji wa matibabu bila malipo umebadilisha maisha ya mamilioni ya watu na kutuleta karibu zaidi na dunia isiyo na ugonjwa huu wa kale.”
• Yōhei Sasakawa, Balozi Mwema wa WHO wa Kutokomeza Ukoma:
“Moja ya changamoto ngumu zaidi ninazokutana nazo katika safari zangu ni unyanyapaa wa kijamii unaohusishwa na ukoma, ambao mara nyingi ni tatizo kubwa zaidi kuliko ugonjwa wenyewe. Hata baada ya kupona, watu bado hubeba maumivu yasiyoisha ya kutengwa kijamii.”
• Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkuu wa WHO, kuhusu maendeleo ya kitaifa:
“Ukoma umewakumba binadamu kwa maelfu ya miaka, lakini nchi baada ya nchi zinakomesha maambukizi na kuwaweka huru watu binafsi, familia na jamii kutokana na mateso na unyanyapaa wake.”