Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kijana Baraka Ayubu abuni teknolojia ya ‘A.Possible’ kuboresha elimu na afya ya akili Tanzania

Wanafunzi nchini Tanzania wanashiriki katika darasa la elimu ya ICT, wakitumia kompyuta ndogo na wakiongozwa na mwalimu katika mazingira ya maabara ya kompyuta.
UN News
Baraka Ayubu abuni teknolojia ya ‘A.Possible’ kuboresha elimu na afya ya akili Tanzania.

Kijana Baraka Ayubu abuni teknolojia ya ‘A.Possible’ kuboresha elimu na afya ya akili Tanzania

Na Rashid Malekela - Tabora, Tanzania
Utamaduni na Elimu

Wakati ulimwengu Jumamosi wiki  hii ya Januari 24 unaadhimisha siku ya elimu duniani, nguvu ya vijana katika uvumbuzi imetajwa kuwa injini kuu ya mabadiliko ya kijamii na maendeleo endelevu. Katika kuakisi ujumbe wa mwaka huu, “Nguvu ya vijana katika kubuni ili kuboresha elimu kwa pamoja,” kijana Baraka Ayubu, ambaye ni Shujaa na Mchechemuzi wa Vijana wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Tanzania, amekuwa kielelezo cha jinsi teknolojia inavyoweza kuleta mageuzi katika mifumo ya ujifunzaji na ustawi wa wanafunzi.

Mwaka 2023 akiwa kidato cha nne Kupitia programu ya ‘Apps and Girls Coding and Entrepreneurship’, alivumbua programu ya simu iitwayo “A.Possible.” Programu hiyo inalenga kutatua changamoto za uhaba wa rasilimali na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi nchini Tanzania.

Sasa, Baraka mwenye umri wa miaka 18, ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Stashahada ya Uhandisi wa Mechatronics katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), akiendeleza ndoto yake ya  A Possible, kuwa nyenzo mbadala ya kujifunzia.

Mwanamume mchanga mwenye tabasamu akiwa amevaa shati nyeupe la polo anasimama ili kusaidia wanafunzi wawili wa kike wanaotabasamu wanapofanya kazi kwenye kompyuta ndogo darasani.
UN News
Wanafunzi wanaoshiriki katika kujifunza ICT nchini Tanzania wakiongozwa na kijana Baraka Ayubu ambaye alibuni teknolojia ya ‘A.Possible’ kuboresha elimu na afya ya akili nchini humo.

Kutoka Shule ya Kata hadi uvumbuzi wa kidijitali

Akizungumza katika mahojiano maalum na Rashid Malekela wa Idhaa hii kutokea mkoani Mbeya kusini mwa Tanzania, ameeleza kuwa msukumo wa kubuni programu hiyo ulitokana na mazingira magumu aliyopitia wakati wa masomo yake ya sekondari.

“Nimesoma shule ya kata, shule ya sekondari Kwembe, ambapo changamoto ni nyingi. Niliona wanafunzi wenzangu wanafeli sana kutokana na upungufu wa rasilimali na changamoto za kisaikolojia. Baada ya kupata mafunzo ya kutengeneza tovuti kutoka shirika la Apps and Girls, nikaona nitumie ujuzi huo kutatua changamoto hizi kupitia jukwaa la A.Possible,” alisema Baraka.

Programu ya A.Possible inatoa huduma tatu muhimu:

  1. Rasilimali za masomo: Upataji wa vitabu vya kujifunzia kutoka Tai Tanzania na mitihani ya miaka iliyopita.
  2. Ushindani wa kitaaluma: Mashindano ya mtandaoni (quizzes) kuwasaidia wanafunzi kujipima maarifa.
  3. Msaada wa afya ya akili: Kupitia wanasaikolojia wanaowashauri vijana wenye changamoto za nyumbani au shuleni.

Kuhamasisha masomo ya STEM

Akiwa ni mchechemuzi wa UNICEF, Baraka anatumia nafasi yake kuhakikisha wanafunzi, hususan wasichana, wanaondoa hofu dhidi ya masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM). Anaamini kuwa teknolojia ya Mechatronics anayosomea inaweza kuifanya elimu Tanzania iwe ya kisasa zaidi kupitia maabara za kidijitali na roboti.

“Nikiwa mwakilishi wa vijana, ninaona kuboresha elimu kunaanza na kuhamasisha kila mwanafunzi kushiriki kikamilifu. Tunahimiza wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili wasiache sayansi bali wajifunze misingi yake mapema, kwani hii ni msingi wa mafaniko yao ya baadaye,” Baraka alisisitiza.

Wito kwa serikali na wadau

Licha ya mafanikio hayo, Baraka alibainisha kuwa safari yake haikuwa rahisi, akikutana na kukatishwa tamaa na baadhi ya wenzao wasiokuwa na mawazo chanya mwanzoni. Hata hivyo, anasisitiza kuwa ushirikiano kati ya vijana na watu wazima ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mwalimu mmoja nchini Tanzania anasimama mbele ya darasa la wanafunzi wanaotumia kompyuta ndogo kwa ajili ya kikao cha elimu ya ICT.
UN News
Kijana Baraka Ayubu abuni teknolojia ya ‘A.Possible’ kuboresha elimu na afya ya akili Tanzania.

Baraka ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania na wadau wa elimu kuongeza rasilimali na vifaa vya kisasa kama maabara na teknolojia shuleni.

“Kwa wadau wa elimu: Wekeni mikakati ya kuwekeza kwa vijana wenye mawazo mazuri na ubunifu. Toeni mwongozo wa kitaalamu ili kuendeleza mawazo yetu na kusaidia kuboresha elimu kwa wote,” alimalizia Baraka.

Kazi ya Baraka Ayubu inatafsiri upya maana ya elimu na ustawi, ikionesha kuwa vijana si watumiaji tu wa mifumo ya elimu, bali ni washirika hai katika kuifanyia mageuzi mifumo hiyo kulingana na mahitaji ya karne ya 21.