Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa nini mgogoro unazidi kuongezeka Haiti na nini kinafuata

Mwanamke mmoja nchini Haiti anabeba mfuko wa chakula wa WFP na chombo cha maziwa baada ya kupokea msaada wa dharura wa chakula huko Port-au-Prince, Delmas 31, chini ya hali ngumu.
© WFP/Luc Junior Segur Mwanamke mmoja katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince, anakusanya misaada ya chakula inayotolewa na Umoja wa Mataifa.

Kwa nini mgogoro unazidi kuongezeka Haiti na nini kinafuata

Amani na Usalama

Haiti inaingia mwaka 2026 ikikabiliwa na moja ya migogoro tata zaidi katika historia yake ya hivi karibuni. Leo Jumatano, taifa hili la kisiwa cha Karibea liko juu ya ajenda ya kimataifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalofanya mkutano wake wa kwanza wa mwaka kuwapa wajumbe taarifa za hali ilivyo nchini humo.

Magenge ya uhalifu yenye silaha yanadhibiti maeneo makubwa ya nchi, na ghasia zimeenea mbali zaidi ya mji mkuu, Port-au-Prince, jambo linalodhoofisha uwezo wa serikali kutawala na kutoa huduma za msingi.

Uchaguzi wa urais haujafanyika kwa muongo mmoja, na mahitaji ya kibinadamu yamefikia viwango visivyowahi kushuhudiwa, huku mamilioni wakihangaika kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

“Vurugu zimeongezeka na kusambaa kijiografia, na kuzidisha ukosefu wa chakula na kuyumba kwa utulivu, wakati mipango ya uongozi wa mpito inakaribia kumalizika na uchaguzi uliochelewa bado ni wa dharura,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, BINUH.

Mwanamume mwenye silaha amevaa kanzu nyekundu na kinyago cheusi akibeba bunduki ya kushambulia katika eneo la Delmas 3 la Port-au-Prince, Haiti.
Giles Clarke Mwanagenge akipiga picha akiwa na bunduki ya hali ya juu katika kitongoji cha Delmas 3, Port-au-Prince.

Kwa nini Haiti ni muhimu

Mgogoro nchini Haiti una sura nyingi. Udhibiti wa magenge ya uhalifu katika maeneo ya mijini na njia za usafiri, pamoja na kuongezeka kwa shughuli zao vijijini, kunavuruga maisha ya watu na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kote nchini.

Matukio mabaya ya hali ya hhew ikiwemo vimbunga, mafuriko na ukame pamoja na matetemeko makubwa ya ardhi, yamezidisha hali  mbaya ya kibinadamu na kufanya iwe vigumu zaidi kwa nchi kurejea katika hali ya kawaida na kujiendeleza.

Mji wa kusini wa Les Cayes ulifurika kufuatia Kimbunga Melissa mwezi Oktoba 2025.

Zaidi ya mmoja kati ya Wahaiti kumi wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na vurugu, na hivyo nchi iko katika hatari ya kuyumba kwa muda mrefu.

Mwanamume mmoja amesimama kando ya pikipiki yake katika barabara iliyofurika huko Les Cayes, Haiti, baada ya Mvua Melissa.
© UNICEF/Patrice Noel Mji wa kusini wa Les Cayes umejaa mafuriko kutokana na Kimbunga Melissa mnamo Oktoba 2025.

Uhamaji wa watu ikiwemo kupitia uhamiaji unaweza kuongeza shinikizo kwa nchi jirani na kudhoofisha uthabiti wa kiuchumi na kiusalama wa kikanda.

“Vurugu za magenge zinaathiri jamii kote nchini, zikiwa na athari mbaya zaidi kwa wanawake, watoto na vijana, na kudhoofisha muundo wa kijamii wa nchi kwa muda mrefu,” alisema António Guterres.

Usalama: Magenge, vurugu na kikosi cha kudhibiti magenge

Vurugu za kutumia silaha ziliongezeka katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2025 na zinaendelea kuwa nguvu kuu inayounda maisha ya kila siku ya Wahaiti.

Magenge yenye silaha nzito hutumia ukatili wa kingono na utekaji nyara kwa fidia kudhibiti maeneo, huku operesheni za polisi wakati mwingine zikiungwa mkono na Kikosi cha Kuhibiti Magenge kilichoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikipata mafanikio ya muda katika maeneo machache, na kufungua baadhi ya njia muhimu.

Licha ya mafanikio ya kiufundi, mauaji bado yameenea, hasa nje ya mji mkuu, na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya raia yanaendelea.

“Zaidi ya mauaji 8,100 yalirekodiwa kote nchini kati ya Januari na Novemba 2025. Ripoti pia zilionesha kuongezeka kwa biashara haramu ya watoto, huku watoto wakiendelea kutumiwa na magenge katika majukumu mbalimbali, ikiwemo mashambulizi ya kikatili,” alisema António Guterres.

Siasa: Mpito unaokaribia mwisho

Mpito wa kisiasa nchini Haiti unakaribia hatua muhimu. Amri ya uchaguzi na kalenda sasa zinaashiria matumaini kwamba uchaguzi utafanyika, na kusababisha kuapishwa kwa Rais na wabunge waliochaguliwa mapema mwaka 2027.

“Hitaji la haraka ni kwa makundi ya wadau wa kitaifa kupata muafaka juu ya njia za kumaliza kipindi cha mpito na kuharakisha maandalizi ya uchaguzi,” amesema Guterres.

Baadhi ya wachambuzi wanahoji kama uchaguzi unawezekana bila maboresho makubwa ya usalama.

Wafanyikazi wa usalama wa uchaguzi wa Haiti, wakiwa wamevaa shati lenye maandishi 'SECURITE ELECTORALE' nyuma, wamesimama katika kituo cha kupiga kura huko Port-au-Prince wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015.
MINUSTAH/Logan Abassi Watu walipiga kura katika uchaguzi katika mji mkuu wa Haiti Port au Prince, Oktoba 2015. (Maktaba)

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota nchini Haiti huku upungufu wa ufadhili ukipunguza wigo wa misaada ya kuokoa maisha.

  • Ukosefu wa chakula unaathiri watu milioni 5.7, huku karibu milioni mbili wakiwa katika viwango vya dharura.
  • Idadi ya watu waliokimbia makazi yao imeongezeka mara mbili hadi watu milioni 1.4 ndani ya mwaka mmoja.
  • Vituo vingi vya afya vinafanya kazi kwa shida, na kipindupindu kimeendelea kuwa “tatizo kubwa la afya ya umma.”
  • Katika mwaka wa masomo 2024–25, shule 1,600 zilifungwa kutokana na vurugu, na watoto milioni 1.5 hawana upatikanaji wa elimu.

“Hatua za kibinadamu bado zina uhaba mkubwa wa rasilimali, na upatikanaji wa misaada unazidi kuwa mgumu,” amesema António Guterres.

Dieussika, mtoto aliyefukuzwa nchini Haiti, anasimama darasani kwake akiwa amevaa shati la UNICEF, akibeba chokaa, na anaonekana kuwa amezingatia wakati anashiriki darasani.
© UNICEF/Herold Joseph Watoto wengi nchini Haiti wanajitahidi sana kuendelea na masomo yao.

Haki za binadamu: Wanawake na wasichana katika hatari kubwa

Wanawake na wasichana ni miongoni mwa waathirika wakuu wa mgogoro wa Haiti.

Magenge hutumia mara kwa mara ukatili wa kingono, ikiwemo ubakaji wa pamoja, kama chombo cha vitisho na udhibiti.

Utoaji taarifa za matukio unabaki kuwa mdogo kutokana na hofu na unyanyapaa, na upatikanaji wa huduma zinazomlenga mhanga ni mdogo, hali inayoongeza majeraha ya kisaikolojia na kutokuwajibika kwa wahusika.

“Nina wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi endelevu ya ukatili wa kingono na magenge, jambo linalotisha jamii na kudhoofisha kwa utaratibu usalama na heshima ya wanawake na wasichana,” amesema António Guterres.

Njia ya kusonga mbele ni ipi?

Umoja wa Mataifa umeendelea kusisitiza kwamba kurejesha usalama ni muhimu, lakini hakutoshi peke yake.

Bila maendeleo katika utawala bora, haki, uwajibikaji na huduma za kijamii hasa kwa vijana mafankio yoyote ya kiusalama yatakuwa dhaifu.

Muafaka wa kitaifa na uungwaji mkono endelevu wa kimataifa ni muhimu kuvunja mzunguko wa vurugu na kuyumba kwa utulivu.

“Hatua za utekelezaji wa usalama pekee hazitatosha kushughulikia matatizo mapana ya utawala yaliyosababisha mgogoro wa vurugu za magenge,” amesema Guterres.

Umoja wa Mataifa unachukua hatua gani?

Umoja wa Mataifa unaunga mkono Haiti kwa njia kadhaa:

  • Ujumbe wa kisiasa, BINUH, hutoa ufuatiliaji wa haki za binadamu, msaada wa uchaguzi na kusaidia maendeleo ya polisi.
  • Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yanatoa misaada ya kuokoa maisha kwa jamii zilizo hatarini zaidi. Mpango wa Hatua za Kibinadamu wa 2026 unasaka dola milioni 880 za Marekani kusaidia watu milioni 4.2.
  • Maandalizi yanaendelea kwa Ofisi mpya ya Msaada ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti (UNSOH) ili kutoa msaada wa kiufundi na kiutendaji kwa Kikosi cha Kudhibiti Magenge ya Uhalifu.