Muongo wa kuboresha kilimo katika Ukingo wa Magharibi kwa msaada wa FAO na Canada
Muongo wa kuboresha kilimo katika Ukingo wa Magharibi kwa msaada wa FAO na Canada
Kwa muongo mmoja kuanzia mwaka wa 2016 hadi mwaka wa 2025, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa ushirikiano na serikali ya Canada limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya kilimo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Mashariki ya Kati likilenga kuwasaidia wakulima na vyama vya ushirika kushinda changamoto za muda mrefu za uzalishaji, masoko na mnepo wa maisha.
Kilimo kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa maisha ya watu wengi katika eneo hilo, huku kaya zipatazo 115,000 zikitegemea sekta hiyo kama chanzo kikuu cha kipato. Kupitia mradi wa “Kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia uboreshaji wa minyororo ya thamani ya kilimo katika Ukingo wa Magharibi,” FAO na Canada zimewafikia kaya 22,000 za kilimo, asilimia 35 zikiwa zinazoongozwa na wanawake, hatua iliyosaidia kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya chakula na kilimo. Kwa wakulima kama Fayes Fqiat, faida za mradi huo zimekuwa za moja kwa moja na za kubadilisha maisha.
“Tangu Oktoba 2023, nilipoteza kazi yangu, chanzo changu pekee cha kipato, na tulihisi kama tumepoteza kila kitu. Mradi huo ulifungua mlango ambao hatukuutegemea. Tuliweza kuwekeza katika ardhi ambazo zilikuwa zimetelekezwa na shukrani kwa Mungu, tuliona faida kutoka msimu wa kwanza kabisa. FAO na msaada wa Canada walitusaidia kurudi kufanya kazi mashambani mwetu na kupata riziki kwa jitihada za mikono yetu wenyewe, na hilo ni baraka kubwa.”
Katika ngazi ya masoko, uvumbuzi wa vituo vya baada ya mavuno uliboresha mavuno na kupunguza hasara. Mohamad Shreem, mhudumu wa kituo cha baada ya mavuno cha Qalqilya, anakumbuka changamoto za awali:
“Kabla ya mradi, tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kutoa huduma kwa wakulima kwa sababu ushirika ulikuwa katika hali ngumu. Tulikuwa na mipango na malengo, lakini hatukuweza kuyafanikisha kutokana na hali ya jumla na ukosefu wa mipango sahihi na uwezo. Kwa niaba ya wakulima 500 ambao ni wanachama wa ushirika huu, nawashukuru Canada na FAO kwa msaada wao wa jumla ambao unakidhi mahitaji yetu halisi kwa uelewa na heshima.”
Wanawake pia wamenufaika kutokana na kuimarishwa kwa vyama vya ushirika, vilivyoboresha usindikaji, ubora wa bidhaa, na mbinu rafiki kwa mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuongeza lishe na mnepo wa mifugo. Nadia Al Aqra, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wanawake wa Qabalan, anaeleza.
“Mradi huu unahusisha urekebishaji wa makao makuu ya ushirika wa Qabalan kwa ajili ya Maendeleo ya Vijijini, kwa ushirikiano na FAO, ambayo inatoa msaada wa kifedha na kiufundi.”
Baada ya muongo mmoja, ushirikiano wa FAO na Canada umeonesha jinsi uwekezaji wa kilimo unavyoboreshaji maisha, kuimarisha mnepo wa jamii na kuchangia maendeleo endelevu katika Ukingo wa Magharibi.