Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujenzi wa kingo za kuzuia mafuriko unaofanywa na UNMISS kunasaidia kuokoa maisha Sudan Kusini

media:entermedia_image:a71e1d61-41ec-4f8a-b4eb-a8d05cd37ede
© UNMISS/Nektarios Markogiannis
Mvua isiyo ya kawaida katika miaka ya hivi majuzi imesababisha mafuriko makubwa katika Jimbo la Unity. Ili kuwalinda raia, wahandisi wa UNMISS kutoka Pakistan, walioko Bentiu, wanafanya kazi bila kuchoka kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya tabianchi.

Ujenzi wa kingo za kuzuia mafuriko unaofanywa na UNMISS kunasaidia kuokoa maisha Sudan Kusini

Tabianchi na mazingira

Wakazi wa Bentiu, jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, wanaishi katika hofu ya kudumu ya mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa, huku wahandisi kutoka Pakistan wanaohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) wakiendelea kujenga na kuimarisha kingo za kuzuia mafuriko ili kuzuia ufurushwaji watu na kulinda maisha. 

Video iliyoandaliwa na UNMISS inaanza kwa kuonesha maji yaliyofurika karibu na makazi, yakizunguka barabara na maeneo ya wazi, watu wakitembea kando ya maji, wakitazama kwa wasiwasi kiwango cha maji kinachoendelea kuongezeka. Wahandisi wanaonekana wakifanya kazi ya kuongeza urefu wa kingo, wakibeba mchanga, kupanga mifuko ya mchanga na kukagua uimara wa kingo. Bay Choul ambaye ni mkazi wa Bentiu, anaeleza:

“Tumekabiliwa na changamoto kubwa za mafuriko kutokana na mvua nyingi kupita kiasi. Msaada tunaopokea umekuwa wa muhimu sana na umefanikisha kulifanya eneo hili libaki kavu. Bila msaada huu, tungejikuta katika hali ngumu sana kwa sababu hatuna mahali pengine pa kwenda.”

media:entermedia_image:aae390d7-8320-4dd5-8a7f-23611a3feed4
© UNMISS/Nektarios Markogiannis
Mvua isiyo ya kawaida katika miaka ya hivi majuzi imesababisha mafuriko makubwa katika Jimbo la Unity. Ili kuwalinda raia, wahandisi wa UNMISS kutoka Pakistan, walioko Bentiu, wanafanya kazi bila kuchoka kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya tabianchi.

Hali ya hewa isiyo ya kawaida inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi inaongeza mafuriko, ikifunika mashamba na makazi, kuvuruga uzalishaji wa chakula na kuhatarisha maisha hata wakati wa kiangazi. Rhoda James,  anasema:

Kama kingo hizi zisingekuwa zinaimarishwa na kutunzwa, tusingekuwa hapa leo, na watoto wetu wasingekuwa salama.”

Mafuriko pia huathiri miundombinu muhimu kama barabara na uwanja wa ndege wa Bentiu. Kapteni Amber Asif wa Kikosi cha Uhandisi cha UNMISS anaeleza akisema:

“Mji wa Bentiu na kambi ya wakimbizi ina watu takriban 300,000 walioathiriwa na mafuriko, wengi wakitegemea msaada wa chakula unaosafirishwa kwa ndege. Kituo hiki si miundombinu tu; ni njia yao ya kuokoa maisha.”

Walinda amani wa UNMISS wameongeza kingo za kuzuia maji hadi zaidi ya mita nne, lakini kuimarishwa zaidi bado kunahitajika. Meja Namazul Fikar, Naibu Kamanda wa Pakistan katika UNMISS, anasema:

“Ongezeko kubwa la kiwango cha maji limeonekana, na katika miezi miwili iliyopita pekee limeongezeka sentimita 60. Hii inaweka shinikizo kubwa kwenye kingo zilizopo, na matukio ya kuvuja kwa maji na kufura kwa kingo yanaonekana.”

media:entermedia_image:c76c4dfd-169a-489e-a963-6cef079c0f7a
© UNHCR/Tiksa Negeri
Watu waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko wanabeba watoto na mali zao kwenye barabara iliyojaa maji huko Bentui, Sudan Kusini. (Maktaba)

Taarifa hii inaonesha jinsi juhudi za UNMISS kukabiliana na mafuriko zinavyoweza kuokoa maisha, kulinda riziki za wakazi na kuhakikisha usalama wa wakazi wa Bentiu katika hali ya dharura.