Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nishati ya sola yaleta matumaini mapya kwa wananchi Chad

Maono kutoka angani ya shule moja nchini Chad pamoja na watoto wakicheza katika ua, wakiwa na paneli za sola juu ya paa na kwenye jengo lililo karibu.
© World Bank
Watoto wakicheza nje ya shule inayotumia nishati ya jua nchini Chad, kwa msaada wa Benki ya Dunia.

Nishati ya sola yaleta matumaini mapya kwa wananchi Chad

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Chad, utekelezaji wa mradi wa kusambaza nishati ya umeme PAAET umefanikisha vifaa 145,000 vya nishati ya sola kusambazwa kwa gharama nafuu kwa kaya zilizoko majimbo 23 ya taifa hilo na sasa maisha yamekuwa bora.

Video ya Benki ya Dunia inaanza na taswira kutoka angani na kisha moja kwa moja hadi ndani ya nyumba ya Bebou Kaliss, ambamo kifaa kinachotumia nishati ya sola kinatumika kuunganisha nyaya na kuwasha taa za ndani na hata kuchaji simu.

Kaliss akiwa taa ya ndani anasema, “Tangu tupate vikasha vya sola, tunaweza kufanya kazi hadi usiku wa manane. Na tunaweza kukizima au kukiacha kifaa hiki kinawaka hadi asubuhi.”

Mtu mmoja nchini Chad anajaza simu yake ya rununu kwa kutumia kifaa cha nishati ya jua kilichotolewa na Benki ya Dunia.
© World Bank
Mtu mmoja nchini Chad anajaza simu ya mkononi kwa kutumia kifaa cha nishati ya jua kilichofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Kifaa hicho thamani yake ni dola 100 lakini kila kaya inapatiwa kwa dola 20 na lengo la mradi ambao unajumuisha pia kufunga mitambo ya umeme wa sola, ni kufikia wananchi milioni 6 wa Chad, vituo vya afya 850 na shule 70.

Upatikanaji huu wa umeme kwa gharama nafuu umekuwa muarobaini kwa wanafunzi akiwemo Diane Djenosem, mwanafunzi wa darasa la nne mjini Bébalem ambaye awali alipata shida kusoma usiku.

 “Awali tulilazimika kununua betri kila baada ya siku kadhaa. Lakini na hii sola, hilo hakuna tena. Tena na huu mwanga wa taa, wadudu ambao walikuwa wanazingira tochi sasa hawako tena.”

Katika kituo cha afya cha Bitkine, huduma sasa ni saa 24 ilhali kwa Josephine akiwa ameketi mkekani anasema, “hapa kwetu mara nyingi nyakati za usiku nyoka wamekuwa wanatutesa sana. Lakini sasa kwa sababu ya mwanga wa taa usiku, nyoka wanakimbia, na watoto wetu wanaweza kusoma hata usiku bila tatizo lolote.”

Na katika shule ya Loumba Assonghor huko Farachana, mashariki mwa Chad, kuwekwa kwa mfumo wa umeme wa sola kumeboresha mazingira ya kujisomea kwani darasani kuna mwanga wa kutosha wa taa na vile vile kuna mapangaboi.

Mbairane Gedeone mwalimu wa shule ya msingi Bedaman anasema

“Vikasha vya sola vinatuwezesha kuwa na darasa hata usiku. Iwapo wanafunzi wawili au watatu  hawajaelewa naweza kuwaambia warejee usiku ili niwaelimishe zaidi.”

Mradi wa PAAET umegharimu dola milioni 295 na unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme nchini Chad kutoka asilimia 6 mwaka 2018 hadi asilimia 30 mwaka 2027.