Katika Siku ya Kimataifa Dhidi ya Uhalifu Mtandaoni UN yaonya kuhusu ongezeko la uhalifu huo
Katika Siku ya Kimataifa Dhidi ya Uhalifu Mtandaoni UN yaonya kuhusu ongezeko la uhalifu huo
Sheria na Kuzuia Uhalifu
Dunia inapoadhimisha Siku ya Kimataifa Dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni leo tarehe 24 Desemba, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC imeonya kuwa kuongezeka kwa muunganisho wa kidijitali kunakwenda sambamba na ongezeko kubwa la uhalifu wa mtandaoni.
Zaidi ya theluthi mbili ya watu duniani waiweza kufikia mtandao mwaka 2023, na UNODC imesema dunia ya kidijitali imeleta mabadiliko makubwa na manufaa mengi, lakini pia imefungua mlango wa hatari kubwa.
“Muunganisho wa mtandao umebadilisha maisha na kuleta manufaa mengi, lakini ulimwengu wa kidijitali pia una hatari kubwa,” UNODC imesema, ikionya kuwa wahalifu wa mtandaoni wanatumia mifumo ya kidijitali kuiba fedha, data na taarifa nyeti.
Makundi ya uhalifu yanatapeli mabilioni mtandaoni
UNODC imesema tishio la uhalifu mtandaoni linaendelea kuongezeka, likichochewa na makundi ya uhalifu wa kupangwa yanayovuka mipaka ya nchi. Makundi haya yameanzisha kile kinachojulikana kama “makampuni ya utapeli,” yakisimamia kwa ustadi mitandao ya utapeli inayolenga waathiriwa kote duniani.
“Tishio hili linaendelea kuongezeka,” UNODC imesema, ikibainisha kuwa mitandao ya kihalifu inatumia mahusiano ya kimapenzi mtandaoni, ulaghai wa uwekezaji na mbinu nyingine za utapeli kuwalaghai waathiriwa mabilioni ya dola.
Wakati huo huo, ofisi hiyo imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu gharama ya kibinadamu ya uhalifu huo, ikisema kuwa makundi hayo yanawavuta watu kupitia majukwaa ya mtandaoni na kuwasafirisha kwa nguvu ili kufanya kazi katika vituo vya utapeli.
“Uhalifu huu unawaathiri waathiriwa katika nchi zilizoendelea zaidi huku ukiwasafirisha na kuwanyonya waathiriwa kutoka nchi maskini zaidi,” imesema UNODC.
Kinga na ushirikiano waonekana kuwa muhimu
UNODC imesisitiza kuwa kinga ndiyo ngao bora dhidi ya uhalifu wa mtandaoni na unyonyaji wa kidijitali, ikitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kuongeza uelewa wa hatari hizo duniani kote.
“Kinga ndiyo silaha bora dhidi ya vitisho vya mtandaoni,” shirika hilo limesema, likihimiza serikali kuongeza juhudi za kuelimisha umma kuhusu hatari za utapeli wa mtandaoni, uandikishaji na usafirishaji haramu wa binadamu.
Shirika hilo limesisitiza kuwa uhalifu wa mtandaoni ni wa kuvuka mipaka ya nchi na hauwezi kupigwa vita kwa ufanisi ikiwa mataifa yatafanya kazi peke yao.
“Ushirikiano wa kimataifa lazima uimarishwe,” UNODC imesema, ikiongeza kuwa nchi wanachama zinapaswa kufanya kazi pamoja kuzuia na kukabiliana na uhalifu huo, na kuwalinda wananchi.
Juhudi za kimataifa kupambana na uhalifu mtandaoni
UNODC imesema inaongoza juhudi za Umoja wa Mataifa katika kupambana na uhalifu wa mtandaoni kwa kutoa mafunzo na msaada wa kiufundi kwa nchi duniani kote.
Kwa kutumia utaalamu wake maalum katika kupambana na uhalifu wa kupangwa na rushwa, shirika hilo linasaidia maboresho ya kisheria, kuimarisha uwezo wa vyombo vya dola, na kuboresha ushirikiano wa kimataifa.
“UNODC inatoa msaada wa kiufundi kuimarisha kinga, kurekebisha mifumo ya kisheria, kujenga na kuboresha uwezo wa vyombo vya sheria, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,” imesema taarifa hiyo.
Mkataba mpya wa uhalifu mtandaoni waweka historia
UNODC imeangazia kupitishwa kwa Mkataba wa Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni, uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka 2024 baada ya miaka mitano ya mazungumzo.
Mkataba huo unaweka mfumo wa kimataifa wa kuchunguza na kufungulia mashtaka makosa yanayofanywa mtandaoni, ikiwemo mashambulizi ya ransomware au kudai kikombozi, ulaghai wa kifedha na usambazaji wa picha au video za faragha bila ridhaa.
“Ni mara ya kwanza katika historia kwa mkataba wa kimataifa kutambua kisheria usambazaji wa maudhui ya faragha bila ridhaa kama kosa la jinai,” imesema UNODC, ikiuelezea kama ushindi mkubwa kwa waathiriwa wa ukatili mtandaoni.
Mkataba huo ulifunguliwa kwa kutiwa saini mwezi Oktoba 2025 mjini Hanoi Viet Nam, ambapo nchi 72 tayari zimetia saini.
Utaanza kutumika rasmi siku 90 baada ya nchi ya 40 kuweka hati ya kuridhia, hatua inayotarajiwa kuimarisha mapambano ya kimataifa dhidi ya uhalifu mtandaoni.