Baraza la Usalama: Hakuna aliye salama Sudan wakiwemo wahudumu wa kibinadamu
Amani na Usalama
Vita vya Sudan vinapokaribia kutimiza siku 1,000, hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota kwa kasi, huku raia wakiendelea kubeba mzigo mkubwa wa ghasia zinazoendelea na hali ya kukwepa uwajibikaji ikitamalaki , limearifiwa leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama hii leo kwa niaba ya afisa mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Edem Wosornu Mkurugenzi wa operesheni wa Ofisi ya Kuratibu wa Mausla ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa “ukatili wa mgogoro huu unaonekana kutokuwa na mipaka, huku mashambulizi yakienea na kushika kasi katika maeneo mengi.”
Kordofan yawa Kitovu kipya cha ghasia
Majimbo ya Kordofan yameibuka kuwa kitovu kipya cha mapigano ya umwagaji damu, amesema Bi. Wosornu yakishuhudia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, makombora na kuimarishwa kwa kuzingirwa kwa miji.
Katika Jimbo la Kordofan Kusini pekee, zaidi ya raia 100 waliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mapema Desemba, yakiwemo mashambulizi dhidi ya shule ya chekechea na hospitali yaliyosababisha vifo vya angalau watu 89, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
“Kuzingirwa kwa miji ya Kadugli na Dilling kumeimarishwa,” Wosornu amesema, akibainisha kuwa mashambulizi yaliendelea hata baada ya kituo cha vifaa cha Umoja wa Mataifa kushambuliwa, hali iliyolazimu kuhamishwa kwa wafanyakazi.
Ufikishaji wamisaada uko hatarini
Shughuli za misaada zinakabiliwa na hatari na vikwazo vinavyoongezeka, huku mashambulizi yakilenga moja kwa moja wahudumu wa kibinadamu na mali zao. Katika jimbo la Kordofan Kaskazini, lori la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP lilishambuliwa mwezi huu, na dereva wake kujeruhiwa vibaya likiwa shambulio la sita dhidi ya mali za WFP nchini Sudan mwaka huu.
“Hili lilikuwa onesho jingine la hatari kubwa zinazowakabili wafanyakazi wa misaada kote Sudan,” Wosornu ameliambia Baraza la Usalama, akiongeza kuwa usajili wa lazima vitani na vizuizi vya raia kuondoka maeneo ya mapigano vinazidisha mgogoro.
Mauaji na ukatili waendelea Darfur
Mahitaji makubwa ya kibinadamu yanaendelea kote Darfur, ambako ripoti za mauaji ya halaiki, ukatili wa kingono na mashambulizi dhidi ya raia vinaendelea kuripotiwa.
Wosornu amenukuu ripoti ya hivi karibuni ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iliyoeleza “kuuawa kwa makusudi kwa raia na ukatili wa kutisha wa kingono, ikiwemo ubakaji na ubakaji wa makundi” wakati wa mashambulizi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika jimbo la Darfur Kusini na Kaskazini mapema mwezi huu yaliua makumi ya watu zaidi, huku wahudumu wa afya wakizuiliwa Nyala katikati ya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya afya.
Mfumo wa misaada wakumbwa na shinikizo kubwa
Licha ya hali mbaya ya kiusalama na upungufu wa fedha, mashirika ya kibinadamu yamefanikiwa kuwafikia watu milioni 16.8 tangu Januari, Wosornu amesema.
Hata hivyo, ameonya kuwa mfumo huo uko “chini ya shinikizo ambalo halijawahi kushuhudiwa, na kwa kuongezea, unashambuliwa moja kwa moja,” huku uhaba wa chakula ukiongezeka, maeneo mapya yakiingia katika njaa, na miundombinu muhimu ikiwemo vituo vya umeme vikilengwa mara kwa mara.
UN: hatua za haraka za ulinzi, ufikiaji na amani
Amehitimisha taarifa yake Wosornu akilitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua kwa “ujasiri na dhamira ya pamoja zaidi”, akitoa wito wa hatua za haraka kulinda raia, kuhakikisha upatikanaji wa misaada na kuendeleza amani.
“Baraza lazima litume ujumbe thabiti na usio na shaka kwamba mashambulizi dhidi ya raia kuwa hayataweza kuvumiliwa,” amesema, akisisitiza haja ya kusitisha mtiririko wa silaha na kusukuma pande zinazopigana kuelekea “usitishaji wa mapigano wa kitaifa, jumuishi na wa kudumu ambao unahitajika kwa dharura.”