UNHCR: Wimbi la wakimbizi wa DRC kuongeza changamoto za kibinadamu Burundi
UNHCR: Wimbi la wakimbizi wa DRC kuongeza changamoto za kibinadamu Burundi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, leo limeonya kuhusu kuongezeka kwa kasi kwa janga la kibinadamu nchini Burundi, linalochochewa na kuongezeka kwa machafuko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Shirika hilo linasema tangu mapema Desemba, zaidi ya watu 84,000 waliokimbia mapigano huko Kivu Kusini wamevuka mpaka na kuingia Burundi, na hivyo kuongeza idadi ya wakimbizi na wanaotafuta hifadhi kutoka Congo nchini humo hadi zaidi ya watu 200,000.
“Hali imefikia hatua ya hatari,” amesema Mwakilishi wa UNHCR nchini Burundi, Brigitte Mukanga-Eno, akionya kuwa kasi na ukubwa wa uwasili wa wakimbizi vimezidi uwezo wa maeneo ya mapokezi.
Wanawake na watoto waathirika wakuu
Maelfu ya watu wanaendelea kuvuka mpaka kila siku kwa miguu na kwa boti, wengi wao wakifika wakiwa wamechoka, wenye njaa na waliopata mshtuko wa kisaikolojia.
UNHCR inasema wanawake na watoto wameathirika zaidi, huku baadhi ya wanawake wajawazito wakiripoti kuwa hawakuwa wamekula kwa siku kadhaa. “Watu wanafika wakiwa wamebeba majeraha ya kimwili na kisaikolojia yaliyotokana na ghasia za kutisha,” amesema Mukanga-Eno, akisisitiza hitaji la haraka la ulinzi na msaada wa kibinadamu.
Msongamano vituoni waongeza hatari za kiafya
Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi vituo vya mapokezi, vituo vya mpito na maeneo yasiyo rasmi nchini Burundi vinafanya kazi kwa kiwango kinachozidi uwezo baadhi kwa karibu asilimia 200 hali inayoyaacha maelfu ya familia katika mazingira magumu yasiyokubalika.
Upungufu mkubwa wa maji safi na huduma za usafi unaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa yakiwemo kipindupindu na Mpox Limesema shirika hilo.
“Mahitaji ya haraka ya makazi, vyoo, maji, chakula na vifaa vya tiba ni muhimu ili kuzuia janga la afya ya umma,” kwa mujibu wa Mukanga-Eno.
Eneo jipya la makazi latoa afueni kiasi
Ili kupunguza msongamano, Serikali ya Burundi imefungua eneo jipya la makazi huko Bweru, mkoani Ruyigi Buhumuza, ambako karibu wakimbizi 21,000 tayari wamehamishiwa.
Hata hivyo, hali bado ni mbaya inasema UNHCR ambapo familia nyingi bado zinalala nje kwa kukosa mahema, zikiwa wazi kwa mvua zinazoendelea na baridi kali za usiku katika eneo hilo la mwinuko.
“Maelfu bado wako hatarini bila ulinzi wa kutosha,” amesema Mukanga-Eno, akitoa wito wa kuboresha hali katika eneo hilo kwa dharura.
Ghasia zinaendelea ndani ya Kivu Kusini
Upande wa pili wa mpaka nchini DRC, mgogoro unaendelea kuongezeka.
Huko Kivu Kusini ghasia, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mabomu yamewalazimisha zaidi ya watu 500,000 kuyahama makazi yao, wengi wao kwa mara ya pili au ya tatu mwaka huu.
Kwa mujibu wa UNHCR shule zimegeuzwa mabweni yenye msongamano mkubwa, kesi za kwanza za kipindupindu zinaanza kuripotiwa, na mapigano yanaendelea kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.
Mukanga-Eno ameongeza kuwa “Pale ambapo upatikanaji unaruhusu, tunatoa msaada wa kuokoa maisha, lakini mahitaji ni makubwa sana”.
Pengo la fedha latishia msaada wa kuokoa maisha
UNHCR inaomba dola za milioni 47.2 kwa kipindi cha miezi minne ijayo ili kusaidia hadi watu 500,000 waliokimbia makazi yao ndani ya DRC na wakimbizi 166,000 nchini Burundi na nchi jirani.
Licha ya UNHCR na washirika wake kuendelea kusajili wanaowasili, kugawa mahitaji ya msingi na kujenga miundombinu ya awali, shirika hilo linaonya kuwa rasilimali zilizopo hazitoshi.
“Bila ufadhili wa haraka zaidi, utoaji wa misaada utaendelea kuchelewa na maisha zaidi yatawekwa hatarini,” amesema Mukanga-Eno, akisisitiza tena wito wa kumaliza mgogoro na kuwalinda raia.