Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Darfur ni jinamizi linalotia hofu kubwa: Chaloka Beyani

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari, Chaloka Beyani, amesimama mbele ya jengo la kioo lenye mimea ya mitende, akiwa amevaa suti na shati la waridi.
Habari za Umoja wa Mataifa
Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari, Chaloka Beyani.

Hali ya Darfur ni jinamizi linalotia hofu kubwa: Chaloka Beyani

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa unaendelea kuonesha wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la Darfur, Sudan, ukionya kuwa mashambulizi yanayolenga makundi maalum ya watu yanaweza kuashiria hatari kubwa zaidi ya mauaji ya kimbari.

Hayo yamewekwa bayana na Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Chaloka Beyani, ambaye amehitimisha ziara yake ya kwanza jijini Nairobi Kenya katika wadhifa huo kufuatia taarifa za mauaji na ukatili mkubwa unaofanyika katika mji wa El Fasher na maeneo jirani.Beyani akizungumza na UN News amesema

“Ujumbe huu umechochewa na taarifa zinazoendelea kuhusu uhalifu wa kutisha katika mji wa El Fasher na maeneo mengine ya Darfur. Ilikuwa muhimu kufika katika eneo hilo, kukusanya taarifa, kuzithibitisha, na pia kuzungumza na wadau kuhusu njia ya kusonga mbele na mikakati ya kikanda ya kukabiliana na uhalifu huo wa kikatili.”

Kambi kubwa ya wakimbizi huko Tawila, Darfur, Sudan, ambako karibu watu 89,000 wametoroka El Fasher. Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali hutoa misaada ikiwa ni pamoja na chakula, maji, huduma za afya, na msaada wa kisaikolojia.
© UNOCHA/ Mohamed Galal
Maelfu wamekimbia El Fasher na maeneo jirani huku wengi wakiwasili katika eneo la Tawila baada ya kutembea kwa siku kadhaa chini ya tishio la ghasia.

Ameongeza kuwa tathmini ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa ukatili huo ni mpana na unaendelea kwa mfumo mmoja, ukihusisha mauaji ya watu wengi, ubakaji wa halaiki, watu kutoweshwa kwa lazima na mateso. Ameonya kuwa asili ya mashambulizi hayo inaleta tahadhari kubwa chini ya sheria za kimataifa.

“Ni vitendo vilivyoenea, vinavyoendelea kwa uthabiti, na vinahusisha mauaji ya halaiki na unyanyasaji wa kingono kwa kiwango kikubwa. Tathmini yetu inaonesha kuwa uhalifu huu unayalenga makundi maalum ya Waafrika huko Darfur, jambo linalowasha taa nyekundu katika muktadha wa Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.”

Ingawa amesisitiza kuwa ni mahakama yenye mamlaka pekee inayoweza kisheria kubaini kama mauaji ya kimbari yametokea, Beyani amesema hatari yake ni kubwa sana. Pia amewasilisha ujumbe kwa waathirika na manusura, wengi wao wakiwa wamekimbia makazi yao au kuvuka mipaka kutafuta usalama.

“Hawako peke yao katika mateso yao. Hali hii inafuatiliwa kwa karibu, ushahidi unakusanywa, na wahusika hawataachwa waendelee bila kuwajibishwa. Tunahitaji mtazamo unaompa kipaumbela muathirtika, kusimamisha mapigano, kujenga amani, kuhakikisha uwajibikaji, na kutoa fidia kwa waathirika.”

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 11 wamekimbia makazi yao ndani ya Sudan, huku wakimbizi kati ya milioni tatu na nusu hadi milioni nne wakiwa katika nchi jirani, na makumi ya maelfu bado hawajulikani walipo.

Beyani anasisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua za haraka sasa kuzuia ukatili zaidi na kuhakikisha haki inapatikana.