Ubakaji kama silaha ya vita: Safari ya manusura wa Congo katika kupata uponyaji na heshima
Ubakaji kama silaha ya vita: Safari ya manusura wa Congo katika kupata uponyaji na heshima
Ubakaji unaotumika kama silaha ya vita huacha majeraha yasiyofutika ya mwili, akili na ya roho. Katika ushuhuda huu wenye nguvu, manusura mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye sasa anaishi kama mkimbizi nchini Burundi, anasimulia safari yake ya maumivu baada ya kunusurika ukatili wa kingono uliomsababishia majeraha makubwa ya mwili, ikiwemo fistula, pamoja na makovu ya kina ya kihisia.
Akiwa katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi nchini Burundi, Amina, manusura huyu ya ubakaji na mateso anasema kupitia msaada wa mashirika wa kibinadamu alipata huduma ya kuokoa maisha na kurejeshewa tumaini jipya. Simulizi yake ni kielelezo cha ustahimilivu, ujasiri, na hitaji la dharura la kuwalinda wanawake na wasichana katika mazingira ya migogoro. Amina anasimulia siku maisha yake yalipobadilika milele. Anasimulia akisema,
“Watu wasiojulikana walikuja kuchukua nyumba yetu. Walikuwa wamevaa kanzu ndefu. Waliingia ndani na kumkamata mume wangu. Walimpiga risasi mara mbili, akafa. Mdogo wake alitoka nje kuomba msaada, naye pia alipigwa risasi na kuuawa. Waliziacha miili yao nje kisha wakarudi ndani. Walinikamata na kunifunga. Walikuwa wanane. Walipokuwa wanapora nyumba, wanaume wanne walinisukuma chini na kuanza kunibaka hadi nikapoteza fahamu.”
Baada ya mazishi ya mume wake na shemeji yake, alizimia tena kutokana na mshtuko. Baadaye, washambuliaji walirudi na kuwachukua watoto wake watatu. Akiwa katika hatari kubwa, alifanikiwa kukimbilia Burundi akiwa na watoto wake wengine saba. Anasema,
“Nilibakwa na wanaume wanne ambao hata sikujua walitoka wapi. Baada ya hapo, waliingiza kitu katika sehemu zangu za siri na kunisababishia mpasuko. Nilipokuwa nikitembea barabarani na kuhisi haja ya ghafla, nilijisaidia hapo hapo. Nilijawa na aibu kubwa. Sikuweza kukaribia watu tena; nilijitenga kabisa.”
Alipowasili kambi ya Musenyi, alihamishiwa Kituo cha Urumuri Gitega, alipokea matibabu ya fistula, msaada wa kitabibu na kisaikolojia kutoka taasisi ya FONAREV na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), pamoja na kifurushi cha heshima, na sasa anaishi kwa matumaini mapya.
“Kifurushi hiki cha heshima kimenisaidia sana, hasa katika usafi wangu binafsi. Global Development Community Burundi na UNFPA wamenisaidia, na leo niko hai. Zaidi ya hayo, siko tena na harufu mbaya. Sihisi tena aibu kusimama pamoja na wenzangu. Zamani niliepuka kusimama karibu na wanawake wengine kwa sababu ya kuvuja bila hiari. Sasa nina afya njema. Nawahimiza wanawake wengine wasijinyanyapae, watafute matibabu. Wasikae nyumbani, kwa sababu tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa kukaa nyumbani.”
Simulizi ya maisha ya Amina inaonesha ustahimilivu na ujasiri, na kusisitiza umuhimu wa kuwalinda wanawake na wasichana katika migogoro na kuwapatia huduma za kuokoa maisha na kurejesha matumaini.