Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je, mazungumzo yanaweza kuponya dunia iliyogawika? Muungano unaoongozwa na UN unaweka hoja hiyo mezani

Kikundi cha vijana mbalimbali katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Vijana huko Cascais, Ureno, walipunga na kutabasamu kando ya bahari Novemba 25, 2024.
UN News/Eileen Travers
Washiriki wa Jukwaa la Vijana walileta ujumbe wa amani kwa Muungano wa Umoja wa Mataifa wa Ustaarabu, huko Cascais, Ureno.

Je, mazungumzo yanaweza kuponya dunia iliyogawika? Muungano unaoongozwa na UN unaweka hoja hiyo mezani

Masuala ya UM

Dunia inavyokaribia mwishoni mwa mwaka 2025, mgawanyiko wa kijiografia unazidi kuongezeka kati ya Kaskazini na Kusini, Mashariki na Magharibi. Ndiyo maana Jukwaa la Riyadh nchini Saudi Arabia linatumika katika Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa UNAOC) kama mahali pa kukutanisha serikali, asasi za kiraia, vijana viongozi na wanawake wajenzi wa amani ili kuendeleza juhudi za kuvuka tofauti, kupambana na kutovumilia hotuba za chuki, na kuimarisha kuheshimiana katika dunia yenye nguvu nyingi.

Mazungumzo haya yanawezekana kupitia kuwaleta pamoja wadau kutoka maeneo mbalimbali ya dunia ili kujenga uelewano na kukuza umoja wa kibinadamu.

Mnamo tarehe 14–15 Desemba, katika mji mkuu wa Saudi Arabia utakuwa mwenyeji wa Jukwaa la 11 la Kimataifa la Muungano huo, likiwaleta pamoja serikali, asasi za kiraia, viongozi vijana, wanawake wajenzi wa amani, na wadau wa vyombo vya habari.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “UNAOC: Miaka miwili ya mazungumzo kwa ajili ya ubinadamu kuendeleza enzi mpya ya kuheshimiana na kuelewana katika dunia ya nguvu nyingi.”

Kwa nini hili lina umuhimu kwako?

Katika mabara mbalimbali duniani, kutovumiliana na chuki dhidi ya wageni vinaongezeka. Tofauti za kitamaduni na kidini zinageuzwa kuwa silaha za kuhalalisha vurugu na kutenga watu.

Hotuba ya chuki hasa mtandaoni inashamiri, ikiongeza kutoaminia na kudhoofisha mshikamano wa kijamii. Katika mazingira haya, dhamira ya UNAOC  kukuza kuheshimiana na kuelewana baina ya tamaduni na dini mbalimbali  ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote.

UNAOC iliundwaje?

Muungano huu ulizaliwa baada ya misururu ya matukio ya huzuni. Baada ya mashambulizi ya tarehe 9/11 nchini Marekani na milipuko ya baadaye huko Bali, Madrid, London na Istanbul, Hispania na Türkiye lilianzisha wazo la kuunganisha dunia iliyogawanyika.

Ulizinduliwa mwaka 2005 na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ukiwa na lengo la kuzuia migogoro ya utambulisho na kugeuza utofauti kuwa nguvu, si sababu ya vurugu.

Muungano unafanya nini?

Ukiwa na kaulimbiu “Tamaduni Nyingi. Ubinadamu Mmoja,” UNAOC imekuwa jukwaa kuu la UN kwa mazungumzo ya tamaduni. Kazi yake inahusisha vijana, elimu, uelewa wa vyombo vya habari, uhamaji, na kukabiliana na hotuba ya chuki.

Kutoka kuwawezesha wanawake kama wapatanishi wa amani hadi kutumia nguvu ya michezo na sanaa kuwaunganisha watu, Muungano umeanzisha miradi inayovunja dhana potofu, kuzuia msimamo mkali, na kukuza ujumuishi. Mtandao wake wa wahitimu sasa unajumuisha mamia ya wajenzi wa amani duniani kote.

Nini kitaendelea Riyadh?

Jukwaa litajumuisha:

• Mkutano wa ngazi ya juu wa kundi la marafiki wa UNAOC lenye wanachama 161.
• Jukwaa la vijana, likionesha wahitimu walioleta mabadiliko katika jamii zao.
• Vikao vya mada muhimu kama, upotoshaji unaosukumwa na AI, wanawake mstari wa mbele katika amani, uhamaji na utu wa kibinadamu, na kupambana na hotuba ya chuki.
• Tamasha la Video la Vijana la PLURAL+, likisherehekea sauti bunifu zinazopinga chuki dhidi ya wageni na kukuza utofauti.

Matokeo yanayotarajiwa ni yapi?

Jukwaa linatarajiwa kupitisha Tamko la Riyadh, litakaloelekeza sura inayofuata ya UNAOC. Ushirikiano na makubaliano mapya ya mwaka 2026 na kuendelea yatatangazwa, pamoja na mapendekezo yatakayochangia mpango wa utekelezaji wa 2027–2031.
Miaka ishirini baadaye, ujumbe wa UNAOC unabaki wazi: mazungumzo si anasa ni mwokozi wa ubinadamu katika dunia inayozidi kugawanyika.

Jinsi ya kufuatilia Jukwaa:

• Timu ya habari ya UN itakuwa Riyadh kuripoti na kutoa taarifa na mahojiano.
• Matangazo ya moja kwa moja na yaliyorekodiwa yatapatikana kupitia WebTV.
• Pakiti za video za ubora wa matangazo na taarifa zitapatikana kupitia UNifeed.