Upatikanaji wa maji yanayoweza kurejelezwa kwa mtu mmoja wapungua kwa asilimia 7 katika miaka 10 - FAO
Upatikanaji wa maji yanayoweza kurejelezwa kwa mtu mmoja wapungua kwa asilimia 7 katika miaka 10 - FAO
Upatikanaji wa maji safi yanayoweza kurejelezwa kwa mtu mmoja mmoja umepungua kwa kiwango cha asilimia 7 katika muongo mmoja, huku shinikizo likiongezeka katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji, hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya taarifa ya kuonesha picha halisi ya rasilimali maji na matumizi yake duniani, AQUASTAT 2025 iliyotolewa leo tarehe 12 Desemba 2025 na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO).
Ripoti hiyo inatoa taswira ya mwenendo wa kimataifa wa rasilimali za maji, ikijumuisha matumizi, umwagiliaji, ufanisi wa matumizi, na viwango vya ukosefu wa maji kama yalivyoripotiwa katika mzunguko wa AQUASTAT wa 2024. Maji yanayoweza kurejeshwa ni yale yanayojazwa upya na mzunguko wa maji unaojumuisha uvukizaji, urejeshaji wa maji ya mvua.
Maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji yaendelea kukabiliwa na shinikizo
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Afrika Kaskazini na Asia ya Magharibi bado zinakabiliwa na upungufu mkali wa rasilimali za maji. Nchi kama Kuwait na Qatar zinaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye kiwango cha chini zaidi cha maji kinachopatikana kwa mtu duniani.
Wakati huo huo, matumizi ya maji yameongezeka katika maeneo kadhaa, yakiongeza mzigo kwa mito na vyanzo vya maji ardhini. Kilimo kimebaki kuwa sekta kubwa zaidi inayotumia maji duniani, kikichangia wastani wa asilimia 72 ya matumizi katika maeneo mengi.
Mitindo ya kikanda na mabadiliko ya matumizi
Katika maeneo ya Afrika Kaskazini, upatikanaji wa maji kwa mtu mmoja umesalia chini wakati matumizi yameongezeka kwa asilimia 16 katika kipindi cha miaka kumi. Asia ya Magharibi, ambayo ni nyumbani kwa idadi kubwa ya watu wanaoongezeka kwa kasi na mahitaji ya juu ya kilimo, nayo inakabiliwa na shinikizo linalozidi kuongezeka kwa rasilimali zilizopo.
Hata hivyo, maeneo yenye rasilimali nyingi za maji bado yanashuhudia ushindani mkubwa wa matumizi baina ya sekta za kilimo, mijini na viwandani, kutokana na ongezeko la umwagiliaji na kasi ya ukuaji wa miji.
Pengo la umwagiliaji na tofauti katika ufanisi
Ripoti inaonesha tofauti kubwa kati ya maeneo katika kiwango cha umwagiliaji na ufanisi wa matumizi ya maji. Katika sehemu za Amerika ya Kusini na Asia, umwagiliaji una mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao. Lakini katika maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, ardhi inayomwagiliwa bado ni ndogo, jambo linaloashiria changamoto kubwa katika upatikanaji wa miundombinu ya maji ya kilimo.
Ingawa baadhi ya maeneo yameongeza ufanisi wa matumizi ya maji, ukosefu wa maji bado ni mkubwa sana katika nchi ambako matumizi yanazidi kiwango kinachoweza kurejeshwa kila mwaka.
SDG 6.4: Ufuatiliaji wa matumizi endelevu ya maji
Ripoti ya AQUASTAT pia imetoa taarifa zilizothibitishwa kuhusu viashiria vya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6.4), vinavyopima ufanisi wa matumizi ya maji (6.4.1) na kiwango cha ukosefu wa maji (6.4.2). Ingawa ufanisi umeimarika kwa ujumla, kiwango cha juu cha uhaba huo kinabainisha haja ya kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, sambamba na kuongezwa kwa hatua za kukabiliana na ongezeko la maji.