Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Hakuna ushahidi unaonyesha chanjo zinasababisha Usonji

Msaidizi wa chanjo akimpa mtoto wa miezi saba chanjo anayeshikiliwa na mama yake katika makazi ya mbali katika jimbo la Bahari Nyekundu nchini Sudan.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih Mtoto mchanga apewa chanjo ya polio katika eneo la vijijini la jimbo la Bahari Nyekundu nchini Sudan.

WHO: Hakuna ushahidi unaonyesha chanjo zinasababisha Usonji

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limetoa taarifa mpya ikieleza kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya chanjo na ugonjwa wa usonji au kwa lugha ya kiingereza ukifahamika kama autism kwa watoto. Hii imetokana na uchambuzi mkubwa uliofanywa na jopo la wataalam wa kimataifa wanaochunguza usalama wa chanjo.

Kwa miaka kadhaa, kumekuwa na hofu na taarifa potofu katika jamii zikidai kuwa chanjo za watoto huweza kusababisha usonji. Lakini wataalam wanasema hakuna ukweli katika madai hayo.

Utafiti mkubwa uliohusisha mataifa mbalimbali

Wataalam wa WHO walipitia tafiti 31 zilizofanyika kati ya mwaka 2010 na 2025 katika nchi mbalimbali. Matokeo yote yanaonesha kuwa:

  • Chanjo ni salama kwa watoto na wajawazito.
  • Hakuna ushahidi kuwa chanjo husababisha usonji.

Wataalam pia walichunguza chanjo zenye viambato vidogo kama thiomersal na kiasi kidogo cha aluminum ambacho hutumika kuongeza ufanisi wa chanjo. Uchambuzi wa miaka zaidi ya 20 haukuonesha madhara yanayopelekea mtoto kupata usonji.

Kwa mfano, utafiti mmoja mkubwa uliofanyika nchini Denmark, uliowachunguza watoto zaidi ya milioni moja waliozaliwa kuanzia mwaka 1997 hadi 2018, haukuonesha uhusiano kati ya chanjo na usonji.

Mfanyakazi wa afya mwanamke nchini Tanzania akiandaa chanjo kwa ajili ya mtoto wakati wa kampeni ya chanjo UNICEF .
UNICEF TANZANIA

Chanjo zimeokoa maisha milioni 154

WHO inakumbusha kuwa chanjo ni moja ya mafanikio makubwa ya afya duniani. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, chanjo zimeokoa maisha ya watu zaidi ya milioni 154, hasa watoto.

Wito kwa Serikali na Jamii

WHO inazitaka serikali zote duniani kuendelea kutegemea ushahidi wa kisayansi katika kufanya maamuzi kuhusu chanjo. Pia inaomba wazazi waendelee kuwapeleka watoto kupata chanjo ili kuwalinda dhidi ya magonjwa hatari kama surua, polio, nimonia na mengine.