Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya upandaji mpunga yawanufaisha wanajamii katika eneo la Bor, Sudan Kusini

Walinda amani wa Korea Kusini wanawasaidia wakulima wa eneo hilo kwa mashine ya kupanda mpunga katika shamba lililofurika huko Bor, Sudan Kusini.
UNMISS Walinda amani wa Korea Kusini wanaohudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) walisaidia wanasayansi na wakulima wa ndani katika mradi wa kilimo cha mpunga huko Bor.

Mafunzo ya upandaji mpunga yawanufaisha wanajamii katika eneo la Bor, Sudan Kusini

Ukuaji wa Kiuchumi

Msaada wa mafunzo wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Korea Kusini wanaohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS) kupitia wanasayansi na wakulima wa eneo la Bor katika mradi wa kilimo cha mpunga umeleta ustawi kwa jamii ya katikati mwa Sudan.

Miaka michache iliyopita, athari za mabadiliko ya tabianchi ziliwakumba wakulima katika Jimbo la Jonglei, eneo la chini linalokumbwa na mafuriko nchini Sudan Kusini. Madhara yalikuwa makubwa, huku wengi wao wakishuhudia mazao na vyanzo vyao vya riziki vikiharibiwa au kuondolewa kabisa na maji.

“Nilikua na miti ya embe kama 400, mipera, limau na miti ya mitiki, miti ya matunda. Lakini mafuriko yalipokuja mwaka 2020, yaliharibu kila kitu.”

Baada ya kubaini kuwa mabadiliko haya ya hali ya hewa yenye mvua nyingi yangeendelea, na mazao ya kienyeji kama mtama na mahindi yakiendelea kuwa hatarini kuangamia, ilibidi hatua zichukuliwe.

Mwezi Juni 2023, wanasayansi wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha John Garang mjini Bor, wakiwa wamehamasishwa na kuungwa mkono na walinda amani wa Korea Kusini wa UNMISS, walikuja na wazo ambalo kwa baadhi lilionekana kama la ajabu: Kwa nini wasioteshe mpunga, zao linalostawi vizuri kwenye maeneo yenye maji mengi?

Tangu wakati huo, takribani wakulima 150 wa kiume na wa kike kutoka ndani na nje ya Bor wamejifunza hatua zote muhimu za kilimo cha mpunga, na John Chol akiwa miongoni mwa wahitimu wa hivi karibuni.

“Wakulima tuliitwa na Chuo Kikuu cha John Garang kwenda kuona jinsi mradi wa mpunga unavyoendeshwa kwa kushirikiana na UNMISS. Tulipewa mbegu, tukaambiwa tuende tukazipande.”

Tarehe 10 Agosti, miezi michache baada ya kusafisha ekari moja ya shamba jipya, John alifanya hivyo. Miezi mitatu baadaye, anavuna matunda ya kazi yake.

Mlinda amani wa Korea Kusini anaendesha mashine ya kupuria mchele mwekundu karibu na rundo la majani huko Bor, Sudan Kusini, kama sehemu ya mradi wa kilimo unaoungwa mkono na UNMISS.
UNMISS Walinda amani wa Korea Kusini wanaohudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) walisaidia wanasayansi na wakulima wa ndani katika mradi wa kilimo cha mpunga huko Bor.

Magunia 15 (kilo 750) ya mpunga anayotarajia kutoka kwenye eneo lake dogo la majaribio yamewabadilisha majirani waliokuwa na mashaka na sasa wanaamini. John anafafanua hilo.

“Nilipoanza kupanda hapa, walikuja wakasema, ‘Unafanya nini?’ Nikasema napanda mpunga. Wakasema, ‘Mpunga unaweza kuota hapa?’ Nikawaambia unaota. Sasa wanaona mpunga umekomaa. Wanasema watanisaidia palizi. Walikuja, bila kuwapa chochote, wakapalilia. Na wanasema, ‘Mwaka ujao tutajiunga nawe kupanda mpunga’. Hapa ndipo niliwaambia viongozi wetu kuwa kuna wanawake zaidi ya 200 wanaotaka kupanda mpunga mwaka ujao.”

Kutokana na mahitaji makubwa ya mafunzo, maprofesa wa chuo kikuu, walinda amani wa Korea Kusini, na wanafunzi wa awali wanaosaidia kufundisha wanaoanza watakuwa na kazi nyingi kwa miaka ijayo.

Mwanamke wa Sudan Kusini akivuna mpunga shambani, huku wakulima wengine wakifanya kazi nyuma.
UNMISS Walinda amani wa Korea Kusini wanaohudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) walisaidia wanasayansi na wakulima wa ndani katika mradi wa kilimo cha mpunga huko Bor.

Kama si msimu wa kiangazi wa Sudan Kusini, uzalishaji ungekuwa mkubwa zaidi. Miezi michache bila mvua inamaanisha kwamba waanzilishi hawa wa Jonglei wanaweza kupata mavuno matatu badala ya manne kwa mwaka. Hata hivyo, kipato cha ziada kutoka kwenye mazao yao kina faida kubwa.

John anatumia kipato hicho kulipia ada za shule za watoto wake saba, na kwa mwanawe mkubwa anayekaribia kumaliza sekondari, ana mpango maalum.

“Nimemwambia nitakupeleka chuo kikuu usome kilimo. Ukirudi, utanifundisha, ‘Baba, kilimo hakifanywi kwa njia hii’. Nimekuwa nikimwambia lazima asome kilimo, kwa sababu kupitia kilimo ndiko tunapata chakula.”

Peter Ajak Ateny, naye ni Mkulima wa mpunga, mnufaika wa mafunzo ambaye pia sasa ni Mkufunzi wa wanafunzi wapya anaeleza alivyonufaika,

“Mafunzo haya yamekuwa na maana kubwa kwangu, kwa wanafunzi niliowafundisha, na kwa wakulima. Matokeo ni kwamba tumepata ujuzi wa kudumu, tumeingia kwenye uzalishaji wa mpunga, kuboresha uchumi na uhakika wa chakula. Kupitia uzalishaji huu, sasa tunauza mpunga, na pia unaliwa shambani na sokoni.”

Mitaala ya mafunzo haya ya ufundi ni pana na inajumuisha maandalizi ya udongo, mbinu bora za upandaji, udhibiti wa wadudu, umwagiliaji, na usimamizi wa maji. Pengine kipengele chake cha kipekee zaidi ni mafunzo ya kuendesha mashine mbalimbali zinazoweza kuongeza tija kwa kiwango kikubwa. Peter Ajak Ateny anafafanua.

“Mara ya kwanza tulizalisha karibu kilo 500 tulipotumia mbinu za mikono. Baadaye tulipoweka mashine, tukaanza kuvuna tani mbili, na sasa tunavuna tani tano.”

Mipango tayari imeanza kwa kundi jipya la wanafunzi, ambao wanatarajiwa kutumia ujuzi wao mpya msimu ujao wa upandaji unapofika.