Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Vikwazo vya umri pekee havita wafanya watoto kuwa salama mitandaoni

Mitandao ya kijamii inaweza kuwezesha unyanyasaji mtandaoni.
© UNICEF/Raphael Pouget
Mitandao ya kijamii inaweza kuwezesha unyanyasaji mtandaoni.

UNICEF: Vikwazo vya umri pekee havita wafanya watoto kuwa salama mitandaoni

Haki za binadamu

Ulimwenguni kote, serikali zinajadiliana ni umri gani ni ‘mdogo sana’ kutumia mitandao ya kijamii, wakati baadhi zikianzisha vikwazo vinavyohusiana na umri katika majukwaa ya mitandaoni.

Hatua hizi zinatokana na wasiwasi ulio halisi: watoto wanakabiliwa na ukatili mtandaoni, unyanyasaji, unyonyaji, na maudhui hatarishi yanayoathiri afya yao ya akili na ustawi wao.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF linasema hali ya sasa inashindwa kuwalinda watoto na inawawekea mzigo mzito wazazi.

Hatari za Kutegemea vikwazo vya umri pekee

UNICEF imeeleza kukaribisha nia ya serikali kulinda watoto, lakini inaonya kuwa marufuku pekee zinaweza kuleta madhara.

Kwa watoto wengi, mitandao ya kijamii ni njia ya kujifunza, kujieleza na kuunganishwa, hasa kwa wanaotengwa au walio katika mazingira magumu. Licha ya vizuizi, watoto bado wanaweza kuingia mitandaoni kupitia njia mbadala au majukwaa yasiyodhibitiwa, jambo linaloongeza hatari.

UNICEF inasisitiza kuwa sheria za umri lazima ziende sambamba na sera pana zinazolinda haki za watoto, faragha yao, na ushiriki wao. Sheria zinazoanzisha vikwazo vya umri si mbadala kwa makampuni kuboresha muundo wa jukwaa na udhibiti wa maudhui.

Wito kwa serikali, makampuni na jamii

UNICEF inatoa wito kwa serikali, wadhibiti, na makampuni kufanya kazi pamoja na watoto na familia kujenga mazingira ya kidijitali ambayo ni salama, yanayojumuisha na yanayoheshimu haki za watoto.

UNICEF inapendekeza kuwekeza katika mazingira salama ya kidijitali kwa watoto kwa:

  • Kufanya uwekezaji wa makampuni katika usalama wa majukwaa kuwa wa lazima, pamoja na udhibiti wa maudhui.
  • Makampuni kubuni majukwaa kwa kuzingatia usalama wa watoto na kutumia mifumo ya kuthibitisha umri inayoheshimu haki za mtoto.
  • Wadhibiti kuweka hatua madhubuti za kuzuia madhara ya mtandaoni.
  • Jamii na washirika kusikiliza sauti na uzoefu wa watoto, vijana, wazazi na walezi katika mijadala ya kanuni za umri.
  • Kutoa msaada kwa wazazi ili kuboresha uelewa wa kidijitali, kwani kwa sasa wanabeba jukumu lisilowezekana la kulinda watoto kwenye mifumo ambayo wao hawakuibuni.

UNICEF imejitolea kuendelea kushirikiana na serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha kila mtoto anajifunza, kuunganishwa na kustawi kwa usalama katika zama za kidijitali.