Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya UN vya ulinzi wa amani nchini DRC vyakabidhiana majukumu

Kamanda Kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Luteni Kanali David Nkungu (Kulia), akipokea bendera ya Tanzania kutoka kwa Kaimu kamanda kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Meja Rafaeli Ngombale aliyemaliza muda wake kama ishara ya kukabidhiwa majukumu ra…
MONUSCO
Kamanda Kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Luteni Kanali David Nkungu (Kulia), akipokea bendera ya Tanzania kutoka kwa Kaimu kamanda kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Meja Rafaeli Ngombale aliyemaliza muda wake kama ishara ya kukabidhiwa majukumu rasmi ya ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Vikosi vya UN vya ulinzi wa amani nchini DRC vyakabidhiana majukumu

Amani na Usalama

Kikosi cha 4 cha ulinzi wa amani kutoka Tanzania kinachohudumu chini ya mwamvuli wa FIB MONUSCO, kimehitimisha rasmi jukumu lake la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo DRC kwa gwaride maalumu la makabidhiano lililofanywa na Tanzqrf ya 4 pamoja na Tanzqrf ya 5 katika makao makuu ya kikosi hico mjini Beni Mavivi katika jimbo la kivu kaskazini. 

Akiongea mara baada ya gwaride hilo kamanda wa kikosi cha 5 Luteni kanali David Nkungu anasema

“Natumaini nitaenda kutekeleza majukumu kwa weledi na ufasaha kwa kuzingatia mamlaka tuliyopewa na Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa majukumu haya ambayo ni ulinzi wa watu, mali na vifaa vilivyo chini ya Umoja wa Mataifa. Yote haya tunafanya ili kuhakikisha amani nchini DRC hususani hapa Kivu kaskazini inaendelea kuwepo na pia kuhakikisha shughuli za raia zinaendelea kama kawaida.”

Kamanda Kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Luteni Kanali David Nkungu akipeperusha bendera ya Tanzania mara baada ya kupokea majukumu ya ulinzi wa amani kutoka kwa kutoka kwa Kaimu kamanda kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Meja Rafaeli Ngombale aliy…
MONUSCO
Kamanda Kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Luteni Kanali David Nkungu akipeperusha bendera ya Tanzania mara baada ya kupokea majukumu ya ulinzi wa amani kutoka kwa kutoka kwa Kaimu kamanda kikosi cha msaada wa haraka TanzQRF, Meja Rafaeli Ngombale aliyemaliza muda wake wa ulinzi wa amani nchini DRC.

Luteni Kanali Nkungu akawapia na ujumbe kwa wananchi wa DRC

“Natoa wito kwa raia wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo DRC kuendelea kuamini vikosi vyetu kuwa tupo kwa ajili yao. Tunachohitaji ni ushirikiano mkubwa kutoka kwao, wasiwe kikwazo kwetu katika kutekeleza haya majukumu.

Kwa upande wake Meja Rafaeli Ngombale kwaniaba ya kamanda wa TanzQRF kikosi cha 4 Luteni kanali Omary Yahya amabaye amemaliza muda wake ameeleza kuwa baadhi ya mafanikio ambayo kikosi chake yamekipata nikurejesha hali ya amani na utulivu ambapo kwa sasa raia wanaendelea na shughuli zao za kila siku tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Kufanikisha hili jukumu kumetokana na jitihada mbalimbali ikiwemo operesheni mbalimbali zilizokuwa chini yangu zote zikiwa na lengo la kuwalinda rai awa DRC. Tumeweza kuvisogeza mbali vikundi mbalimbali kiasi kwamba wananchi wanaweza sasa kuendelea na shughuli zao za kila siku tofauti na matishio yaliyokuwepo wakati tunafika.

Meja Ngambole amezungumzia pia kuhusu uhusiano.

“Tumefanikiwa kuweka uhusiano mwema kati yetu sisi na raia kupitia viongozi mbalimbali wa kijamii na machifu walioko hapa na wote wameweza kutambua kuwa tupo hapa kwa ajili ya kulinda usalama wao na sisi ni sehemu katika maisha yao kwani tunahakikisha amani nchini DRC inadumu na watu wanaendelea na shughuli zao za maisha za kila siku.”

Safari ya ulinzi wa amani katika jimbo la kivu kaskazini nchini jamhuri ya kidemokrasia ya kongo kwa walinda amani wa kikosi cha 4 cha TanzQRFimekamilika na sasa kijiti hicho kimekabidhiwa rasmi kwa TanzQRF kikosi cha 5 kutoka Tanzania.