Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Mlipuko wa kipindupindu wa mwaka huu nchini DRC ni mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25

Miili inazikwa kwa msaada wa wafanyakazi wa WHO baada ya kuanguka kwa Goma kwa waasi wa M23, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mapema Februari 2025.
© WHO
Miili inazikwa kwa msaada wa wafanyakazi wa WHO baada ya kuanguka kwa Goma kwa waasi wa M23, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mapema Februari 2025.

UNICEF: Mlipuko wa kipindupindu wa mwaka huu nchini DRC ni mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25

Afya

Mlipuko wa kipindupindu mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeleta madhara makubwa, ukiwa na jumla ya wagonjwa 64,427 tangu mwanzo wa mwaka huu 2025, na kusababisha vifo 1,888. Watoto waliougua ni 14,818 na waliofariki dunia ni 340, na hivyo kufanya huu kuwa mlipuko mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25 nchini humo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linaeleza.

Mlipuko huu umevuruga elimu ya watoto, ukiwaweka kwenye hatari ya kuugua na kushuhudia mateso na vifo vya wanafamilia. Katika tukio la kusikitisha zaidi, watoto 16 kati ya 62 wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto yatima huko Kinshasa walifariki ndani ya siku chache baada ya ugonjwa huo kusambaa katika nyumba hiyo ya malezi.

“Watoto wa DRC hawapaswi kuathiriwa kwa kiwango kikubwa kiasi hiki na ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kabisa,” anasema John Agbor, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC.

Agbor anaendelea kwamba, “UNICEF inahimiza serikali kuongeza uwekezaji katika huduma za maji, usafi wa mazingira, usafi wa mwili na huduma za afya, hususan katika maeneo yanayojulikana kuwa na mlipuko wa kipindupindu ili kulinda afya na ustawi wa familia na watoto wa DRC.”

Kituo cha afya kinachoungwa mkono na UNFPA huko Goma, ambapo wanawake waliopoteza makazi wanaweza kupata huduma ya uzazi bila malipo.
© UNFPA/Jonas Yunus

Eneo kubwa limeathirika

Majimbo 17 kati ya 26 ya DRC yameathirika kwa sasa, ikiwemo mji mkuu Kinshasa. Asilimia ya watoto katika mlipuko hutofautiana kulingana na mkoa, lakini wastani kitaifa ni takriban asilimia 23.4.

Upatikanaji mdogo wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira unaendelea kuchochea kuendelea kwa kipindupindu nchini DRC. Kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (DHS) wa 2024–2025, ni asilimia 43 tu ya watu wanaotumia huduma za kiwango cha msingi za maji kiwango cha chini zaidi barani Afrika na ni asilimia 15 pekee walio na huduma za msingi za usafi wa mazingira.

Sababu zaidi

Janga la kipindupindu linachangiwa pia na migogoro inayoendelea, uhamishaji wa watu na ukosefu wa usalama mashariki mwa DRC, ambavyo vinazuia upatikanaji wa huduma za afya; matukio makali ya tabianchi kama mvua kubwa na mafuriko yanayoharibu miundombinu ya maji na usafi; na ukuaji wa haraka wa miji bila mpango, ambao umepelekea msongamano na kuzidiwa kwa mifumo ya maji, usafi na usafi wa mwili (WASH). 

Katika maeneo ambayo awali hayakuwa na maambukizi ya kipindupindu, kama Kinshasa, uelewa mdogo wa ugonjwa na kuchelewa kutafuta matibabu kunachangia vifo vingi zaidi.

Kituo cha afya kinachoungwa mkono na UNFPA huko Goma, ambapo wanawake waliopoteza makazi wanaweza kupata huduma ya uzazi bila malipo.
© UNFPA/Jonas Yunus

Mikakati

Serikali imeandaa mpango wa kitaifa wa kutokomeza kipindupindu, unaojulikana kama Mpango wa Sekta Nyingi wa Kutokomeza Kipindupindu (PMSEC) 2023–2027, wenye bajeti ya dola milioni 192. Hata hivyo, mpango huu unakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha, na tathmini ya muda wa kati iliyokamilishwa Mei 2025 imependekeza kuongezwa kwa uwekezaji na uratibu madhubuti wa sekta mbalimbali.

Kufuatia mlipuko wa 2025, serikali pia imeanzisha mpango wa “Mto Congo bila kipindupindu” ili kushughulikia ukosefu wa hatua za kudhibiti kipindupindu katika bandari, kutokuwa na mpango wa usafi kwa boti, kukosa uelimishaji kwa wahudumu na abiria, pamoja na upatikanaji wa maji safi ya kunywa kando ya mto.

UNICEF inafanya kazi katika sekta mbalimbali kuzuia na kukabiliana na kipindupindu, ikiwemo kusaidia timu za majibu ya haraka zinazotumia mbinu ya Case-Area Targeted Intervention (CATI) mkakati unaosaidia kudhibiti milipuko kwa kuchukua hatua za haraka na za kulenga kaya zinazozunguka mgonjwa aliyethibitishwa.

UNICEF pia inaunga mkono vituo vya matibabu ya kipindupindu, inaongoza kampeni za uhamasishaji jamii kuhakikisha familia zinapata taarifa muhimu za kujikinga, na inafanya kazi kuimarisha miundombinu ya WASH katika shule, vituo vya afya na jamii.

Kupitia kampeni za uhamasishaji zinazoungwa mkono na UNICEF, watu zaidi ya milioni 13.5 nchini kote wamefikiwa kati ya Januari na Oktoba 2025 kwa taarifa kuhusu jinsi ya kuzuia na kukabiliana na kipindupindu.

“Mbali na kuitaka serikali kuwekeza katika huduma za afya, maji safi na miundombinu ya usafi, tunawaomba pia washirika wetu wa kimataifa kuongeza ufadhili, hususan kwa ajili ya majibu yetu ya haraka,” alisema Agbor. “Mfuko wa fedha kwa mwaka 2026 unaonekana kuwa dhaifu sana, na bila fedha za ziada na hatua za pamoja, maisha mengi zaidi yanaweza kupotea.”

UNICEF inahitaji takriban dola milioni 6 mwaka 2026 kuhakikisha kuwa mfumo wa majibu ya haraka dhidi ya kipindupindu unafadhiliwa ipasavyo.