Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM na UNV wazindua mtandao wa ulezi kwa wahamiaji waliorudi barani Afrika

Mfanyikazi wa IOM akimsajili mhamiaji kutoka Ethiopia huko Ma'rib, Yemen, kabla ya kusafiri kwenda Addis Ababa.
© IOM Yemen/Elham Al-Oqabi
Mfanyikazi wa IOM akimsajili mhamiaji kutoka Ethiopia huko Ma'rib, Yemen, kabla ya kusafiri kwenda Addis Ababa.

IOM na UNV wazindua mtandao wa ulezi kwa wahamiaji waliorudi barani Afrika

Masuala ya UM

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) kwa kushirikiana na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Wanaojitolea (UNV) wamezindua mtandao mpya wa ulezi kwa ajili ya kuwasaidia wahamiaji wanaorejea katika nchi zao za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Uzinduzi huu, uliofanyika leo tarehe 5 Desemba katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanaojitolea, unalenga kuimarisha mifumo ya uungwaji mkono katika jamii wanakorejea maelfu ya watu wanaojenga upya maisha yao baada ya safari zenye changamoto.

Kupitia mpango huu, kundi la kwanza la watu 50 wanaojitolea kutoka Umoja wa Mataifa litatumwa kama Walezi wa Jamii kwa wahamiaji waliorudi nyumbani katika nchi za Cameroon, Côte d’Ivoire, Ethiopia, Ghana, Guinea, Mali, Senegal na Gambia. Wengi wao ni wahamiaji wa zamani, hivyo wana uwezo wa kutoa mwongozo unaotokana na uelewa wa moja kwa moja wa changamoto za kurejea nyumbani baada ya safari ngumu.

Mpango huu wa Mtandao wa Ulezi ni zaidi ya mfumo wa msaada; ni uwekezaji madhubuti katika mifumo imara na endelevu ya ujumuishaji upya,” amesema Sylvia Ekra, Mkurugenzi wa Kanda wa IOM kwa Afrika Magharibi na Kati. “Kwa kuwaunganisha wahamiaji waliorudi na walezi wanaoelewa safari yao, tunaimarisha uwezo wa kitaifa, tunajenga mshikamano wa kijamii, na kuhakikisha ujumuishaji unafanyika kwa heshima, uaminifu na mwongozo wa vitendo.”

Tangu mwezi Agosti mwaka 2022, zaidi ya wahamiaji 115,000 waliokwama katika njia hatarishi barani Afrika na Afrika Kaskazini wamerejea kwa hiari katika nchi zao kwa msaada wa IOM. Zaidi ya 100,000 kati yao wamepata aina moja au zaidi ya msaada wa kiuchumi, kijamii au kisaikolojia, hatua iliyowasaidia kuanza upya maisha yao kwa hadhi na uthabiti.

Mpango huu wa Mtandao wa Ulezi umebuniwa kuimarisha mifumo ya kitaifa ya ujumuishaji kwa kutoa usaidizi wa kisaikolojia, kuimarisha mitandao ya kijamii, kupunguza unyanyapaa na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo yenye wahamiaji wengi waliorudi.

Kabla ya kuanza kazi, walezi watapatiwa mafunzo kuhusu usaidizi wa msingi wa kisaikolojia, kanuni za ulinzi, njia za rufaa na mbinu za kuhusisha jamii.

Mpango huu unatekelezwa kwa pamoja na IOM na UNV kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya, ukiwalenga wahamiaji wanaorejea kupitia Programu ya Kurudi kwa Hiari na Ujumuishaji (AVRR). Lengo ni kukuza usaidizi unaoongozwa kijamii na unaotegemea nguvu ya kujitolea ili kuimarisha ujumuishaji kwa muda mrefu na kuchangia jamii jumuishi na thabiti.

Mpango wa Mtandao wa Ulezi unaimarisha mtazamo wetu wa pamoja na IOM kuhusu ujumuishaji endelevu unaotegemea utaalamu wa ndani,” amesema Paul Armand Menye, Meneja wa Kanda wa UNV Afrika Magharibi na Kati. “Ushirikiano huu unaonesha jinsi kujitolea kunavyoweza kuimarisha mifumo ya kijamii na kutoa suluhisho linalojibu hali halisi za jamii,” ameongeza

Mpango huu unasisitiza umuhimu wa mbinu shirikishi inayogusa ustawi wa kiuchumi, afya ya akili, mshikamano wa kijamii na kukubalika kwa wahamiaji katika jamii. Kupitia kuwaweka walezi moja kwa moja katika jamii, IOM na UNV wanatarajia kuunda mifumo inayoweza kupanuliwa, inayoendana na mazingira ya ndani na inayojenga uwezo wa kitaifa kuhakikisha wahamiaji wanapata msaada wanaouhitaji ili kujenga upya maisha yao kwa mafanikio.