Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa watu wanaojitolea ni muhimili wa mabadiliko: UN

Tony Edward Mgimba, ni Mratibu wa wanafunzi wa vyuo wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa-YUNA Tanzania, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam.
UN News
Tony Edward Mgimba, ni Mratibu wa wanafunzi wa vyuo wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa-YUNA Tanzania, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam.

Mchango wa watu wanaojitolea ni muhimili wa mabadiliko: UN

Masuala ya UM

Katika dunia inayohitaji mshikamano ili kufikia maendeleo, mchango wa watu wanaojitolea umeendelea kuwa nguvu muhimu ya kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Kila mwaka tarehe 5 mwezi Desemba, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanaojitolea, mwaka huu ikiwa imebeba maudhui “Kila Mchango Una Umuhimu.” 

Maadhimisho ya mwaka huu pia yanazindua rasmi Mwaka wa Kimataifa wa Wanaojitolea kwa Maendeleo Endelevu 2026. Kutoka Dar es Salaam, Tanzania Sabrina Saidi amezungumza na kijana  ambaye anajitolea katika Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania YUNA Je kasema nini?. Karibu Sabrina...

Umoja wa Mataifa unasema kujitolea ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu, na hapa nchini Tanzania baadhi ya vijana wanaendelea kutumia nguvu na muda wao kuchangia katika ustawi wa jamii.

Tony Edward Mgimba, ni Mratibu wa wanafunzi wa vyuo wa Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa-YUNA Tanzania, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam.

Nimemuuliza nini kinamsukuma kuendelea kujitolea?

"Suala zima la kujitolea kwangu mimi lina umuhimu, kwanza katika kukuza taaluma yangu kwa sababu mimi ni kijana na pia ni mwanafunzi. Ninavyojitolea nakuwa najitahidi kukuza career yangu, kujifunza zaidi ili kupata experience. Lakini pia ukiacha katika kujifunza, ni muhimu kwangu kwa sababu napata exposure na kujuana na watu, kuliko kukaa tu ndani kujifungia kusubiri fursa mbalimbali. Kama Waswahili wanavyosema, mkaa bure sio sawa na mtembea bure.”

Kaulimbiu ya wa mwaka huu, Kila Mchango Una Umuhimu inaakisi pia mtazamo wa vijana wanaotaka kuchangia katika kuleta mabadiliko chanya kama Tony.

Katika kaulimbiu ya mwaka huu, kwangu ina mchango mkubwa sana na inaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu 17. Malengo haya hayawezi kutekelezwa na Umoja wa Mataifa peke yake pasipo sisi kila mmoja wetu. Kwa mfano kwenye suala la utunzaji wa amani na mazingira, vijana lazima tujitolee, kwa sababu mazingira ni ya kwetu sote.”

Tony anahamasisha pia vijana wengine kuchangamkia fursa za kujitolea kama njia ya kupata uzoefu.

Wito wangu kwa vijana wengine, nawashauri wachangamkie masuala ya kujitolea iwe katika msingi sahihi au bora. Kwa sababu tunapojitolea, mbali na kukuza taaluma zetu na kutengeneza fursa, inatusaidia kuelewa vitu zaidi kwa undani, kwa sababu kuna yale tunayojifunza darasani na yale unayokuta nje ya darasa.”

Maudhui ya mwaka huu yanasisitiza kuwa hakuna mchango mdogo. Kila hatua, iwe kupanda mti, kutoa muda kufundisha, kusaidia katika shughuli za jamii, au kushiriki kampeni za amanimhuleta tofauti kubwa katika jamii.