Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaunga mkono matumizi ya dawa za kupunguza uzito, yatangaza utipwatipwa kuwa ni ugonjwa sugu

Picha ya mtazamo wa kutoka juu kwenda chini ya miguu tupu ya mtu amesimama kwenye mizani nyeupe ya dijitali ya bafuni yenye onyesho nyeusi.
© Unsplash/i yunmai Matumizi ya dawa za kudhibiti utipwatipwa yaungwa mkono na Shirika la afya Duniani WHO

WHO yaunga mkono matumizi ya dawa za kupunguza uzito, yatangaza utipwatipwa kuwa ni ugonjwa sugu

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limetoa mwongozo wake wa kwanza kuhusu matumizi ya kundi jipya la dawa za kupunguza uzito, hatua inayowakilisha mabadiliko makubwa katika sera za afya duniani wakati viwango vya unene wa kupitiliza au utipwatupwa vikizidi kuongezeka.

Mwongozo huo unalenga tiba za dawa aina ya GLP-1 ambazo ni dawa kama vile liraglutide, semaglutide na tirzepatide na linatoa mapendekezo ya masharti kuhusu jinsi zinavyoweza kutumika kwa usalama kama sehemu ya matibabu ya muda mrefu.
Picha ya karibu ya fries ya kifaransa iliyokatwa katika chombo cha karatasi, iliyofunikwa na mchuzi wa jibini ya manjano.
Public domain viazi vya kukaanga au chips na jibini. Kwa mujibu wa utafiti wa WHO kuna vifi milioni 17 kila mwaka vinavyosababishwa na maradhi ya moyo

Kuishi na utipwatipwa

Kwa mujibu wa takwimu za WHO zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na unene uliokithiri au utipwatipwa, hali iliyohusishwa na vifo milioni 3.7 mwaka 2024.
Bila kuchukua hatua madhubuti, WHO inaonya kuwa idadi ya watu watakaoathirika inaweza kuongezeka mara mbili kufikia 2030, na hivyo kuongeza mzigo mkubwa kwa mifumo ya afya na kusababisha hasara za kiuchumi duniani zinazokadiriwa kufikia dola trilioni 3 kwa mwaka.
Kama mamlaka kuu ya afya ya umma duniani, taarifa ya WHO inatarajiwa kuathiri sera za kitaifa, bima za afya na mazoea ya kitabibu, hasa wakati mahitaji ya tiba bora za kupunguza uzito yakiongezeka kwa kasi.
Utipwatipwa ni changamoto kubwa ya afya ya kimataifa,” amesema Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. “Mwongozo wetu mpya unatambua kuwa utipwatipwa ni ugonjwa sugu unaoweza kutibiwa kwa huduma jumuishi na ya kudumu. Ingawa dawa pekee haziwezi kutatua janga hili, tiba za GLP-1 zinaweza kuwasaidia mamilioni ya watu kushinda unene kupita kiasi na kupunguza madhara yanayohusiana nao.”
Mvulana aliye na shati la manjano na miwani anaangalia simu yake ya mkononi wakati hamburger na milkshake ziko kwenye tray yake katika mgahawa wa chakula cha haraka.
© UNICEF/Zhanara Karimova Ulaji wa mara kwa mara wa chakula cha mafuta mengi unaweza kuwa na uzoea kwa watoto.

Ugonjwa mtambuka

WHO inasisitiza kuwa unene kupita kiasi si matokeo ya uchaguzi wa mtindo wa maisha pekee, bali ni hali tata na sugu inayohusisha vinasaba, mazingira, biolojia na hali za kijamii.
Mkuu huyo wa WHO ameongeza kuwa utipwatipwa “Ni kichocheo kikuu cha magonjwa ya moyo, kisukari aina ya pili na aina fulani za saratani, na pia huongeza hatari kwa magonjwa ya kuambukiza. Kwa watu wengi, kupunguza uzito na kuudumisha ni jambo gumu bila msaada wa kitabibu.”
Tiba za GLP-1 hufanya kazi kwa kuiga homoni ya asili inayosaidia kudhibiti hamu ya kula, sukari ya kwenye damu na mmeng’enyo wa chakula.
Kwa watu wenye utipwatipwa, dawa hizi zinaweza kusababisha kupungua kwa uzito kwa kiwango kikubwa na kuboresha afya kwa ujumla.
WHO imeongeza dawa hizi kwenye Orodha ya Dawa Muhimu mwaka 2025 kwa usimamizi wa kisukari aina ya pili kwa watu walio katika hatari, na miongozo mipya sasa inapendekeza matumizi yao ya muda mrefu kwa watu wazima wanaoishi na unene, isipokuwa wakati wa ujauzito.
Pendekezo hilo ni la masharti kutokana na ukosefu wa takwimu za kutosha za usalama wa muda mrefu, mashaka kuhusu udumishaji wa uzito baada ya kusitisha dawa, gharama kubwa na wasiwasi kuhusu usawa wa upatikanaji wa dawa hizo miongoni mwa nchi.
Mwanamume mwenye tumbo jingi ameshika sahani na burger kubwa.
© Unsplash/Towfiqu Barbhuiya Unene wa kupindukia ulimwenguni kote umeongezeka karibu mara tatu tangu 1975.

Sio suluhisho pekee

WHO inasisitiza kuwa dawa za kupunguza uzito zinapaswa kutumika sambamba na msaada mwingine.
Matibabu yenye ufanisi zaidi yanachanganya dawa na ulaji bora, kuongeza shughuli za mwili, na ushauri wa muda mrefu kutoka kwa wahudumu wa afya.
Shirika hilo linaeleza kuwa utipwatipwa hauwezi kutatuliwa na mtu mmoja pekee, bali unahitaji hatua pana kutoka kwa serikali na sekta mbalimbali ili kuunda mazingira bora ya chakula na kuhakikisha uingiliaji wa mapema kwa wale walio katika hatari.

Kuhakikisha upatikanaji na usalama

Mahitaji ya dawa za GLP-1 tayari yanazidi kiwango cha uzalishaji. Hata kwa kuongeza uzalishaji, WHO inakadiria kuwa chini ya asilimia 10 ya watu wanaostahili ndio watakuwa na upatikanaji wa dawa hizo kufikia 2030.
Shirika hilo linaonya kuwa bila sera mahsusi, matibabu haya yanaweza kuongeza pengo la usawa wa kiafya duniani.
Mlo unaolenga burger, friji iliyokatwa kwa njia ya 'crinkle-cut', na soda katika kikombe cha plastiki kwenye tray nyekundu.
Unsplash/Christopher William Chakula cha mgahawa wa chakula cha haraka.
Shirika hilo linazitaka serikali kuzingatia mbinu kama ununuzi wa pamoja, bei za haki na leseni za hiari ili kupanua wigo wa upatikanaji wake.
WHO pia inaonya kuhusu kuongezeka kwa usambazaji wa bidhaa bandia au zenye ubora hafifu za GLP-1 kutokana na upungufu wa kimataifa.
Inasisitiza umuhimu wa minyororo iliyodhibitiwa ya usambazaji, maagizo kutoka kwa wataalam waliohitimu na usimamizi madhubuti ili kulinda wagonjwa.
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ombi la Nchi Wanachama na umetumia ushahidi wa kisayansi, mapitio ya wataalam na maoni ya watu wanaoishi na utipwatipwa.
WHO inapanga kusahihisha mapendekezo hayo kadri ushahidi mpya unavyojitokeza na itafanya kazi na wadau mwaka 2026 kuhakikisha kuwa walioko katika mahitaji ya dharura wanapewa kipaumbele.