Zaidi ya taasisi 340 za elimu zimeharibiwa au kuangamizwa nchini Ukraine mwaka huu
Zaidi ya taasisi 340 za elimu zimeharibiwa au kuangamizwa nchini Ukraine mwaka huu
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) leo hii huko Kyiv, Ukraine limeripoti kuwa zaidi ya taasisi 340 za elimu zimeharibiwa au kuangamizwa mwaka huu 2025 nchini humo kutokana na vita vinavyoendelea, ambavyo vinakatiza elimu kwa watoto kwa kuharibu shule na kuwalazimu kukosa haki yao ya elimu salama.
Hili linafanya jumla ya shule zilizoharibiwa au kuangamizwa kufikia 2,800 tangu kuongezeka kwa vita mnamo Februari 2022. Kwa kuwa hizi ni matukio yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa pekee, idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.
“Shule zinapaswa kuwa maeneo salama ambapo watoto wanaweza kujifunza bila hofu, hata wakati wa vita. Wakati wa majanga, elimu huwapatia watoto msaada muhimu na hisia ya maisha ya kawaida, shule ni sehemu za kujifunza ambazo pia zinachangia maendeleo ya jumla ya watoto kupitia mwingiliano wao na wenzao na walimu, pamoja na kutoa fursa ya kupata huduma nyingine za kijamii,” amesema Munir Mammadzade, Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine.
Mwaka huu, watoto milioni 4.6 nchini Ukraine wanakabiliwa na vikwazo vya kielimu wanapojaribu kuendelea na mwaka wa nne wa masomo chini ya vita vya kiwango kikubwa. Mashambulizi yanayoendelea, yanaendelea kuharibu au kuangamiza shule na kuhatarisha maisha ya watoto. Kengele za mashambulizi ya anga hukatiza masomo. Shule nyingi, hasa katika maeneo ya mstari wa mbele, zimefungwa kutokana na mapigano au ukosefu wa makazi ya usalama, na hivyo kuwalazimu karibu watoto milioni 1 kusoma mtandaoni.
Kwa wale wanaosoma kwa mchanganyiko wa mtandaoni na ana kwa ana au mtandaoni kabisa, ukosefu wa kuonana ana kwa ana na walimu wao na wenzao huathiri uwezo wao wa kujifunza na kuongeza mzigo wa kihisia unaosababishwa na vita.
“Licha ya changamoto, watoto nchini Ukraine wameazimia kuendelea kujifunza iwe shuleni au mtandaoni, darasani au kwenye makazi ya dharura. Wana matumaini ya siku zijazo ambapo wanaweza kutimiza ndoto zao,” amesema Mammadzade.
Mwitikio wa UNICEF, kwa ushirikiano na serikali na wadau wa eneo hilo, umewezesha zaidi ya watoto nusu milioni kupata elimu jumuishi ya rasmi au isiyo rasmi, ikiwemo mazingira salama ya kujifunzia na kuwasaidia kurejesha ujifunzaji waliopoteza kupitia Masomo ya kurekebisha mapungufu ya ujifunzaji.
Mwaka huu unatimiza miaka 10 tangu kupitishwa kwa Azimio la Shule Salama, tamko la kimataifa linalolenga kulinda haki ya watoto kupata elimu wakati wa vita, kuiendeleza elimu na kuzuia matumizi ya kijeshi ya shule.
Katika mkutano wa Kimataifa kuhusu Azimio la Shule Salama uliofanyika Nairobi tarehe 25–26 Novemba, UNICEF imeungana na serikali, watoto, watetezi wa vijana na wengine wengi kujadili jinsi ya kulinda vyema elimu ya watoto katika maeneo ya migogoro na kuendeleza upya dhamira hii ya kimataifa.
Kulinda shule na haki za watoto kupata elimu si jambo la hiari wakati wa vita, ni lazima. UNICEF inahimiza wadau wa kimataifa kuendelea kuisaidia sekta ya elimu ya Ukraine kama uwekezaji muhimu na usiopingika kwa watoto na mustakabali wa taifa hilo.