UNIDO: Wajasiriamali vijana waapa kukumbatia fursa na kujenga viwanda vya kesho
UNIDO: Wajasiriamali vijana waapa kukumbatia fursa na kujenga viwanda vya kesho
Vijana wanachangia pakubwa katika uundaji wa viwanda vinavyowanufaisha watu na kulinda sayari. Jukumu lao limetambuliwa leo Jumatano katika siku ya Generation Future ya Mkutano wa Kimataifa wa Viwanda unaofanyika Riyadh Saudia, ambapo kumekuwa na ahadi za kuhakikisha sauti zao zinasikika na mawazo yao kushirikishwa kwa upana zaidi.
Kwa kiwango cha kufeli kwa asilimia 90 kwa biashara changa, vijana wangesamehewa wakiamua kuwa kuanzisha kampuni hasa katika kipindi hiki kigumu kwa uchumi wa dunia ni hatari kubwa.
“Lakini kuna nafasi ya asilimia 10 ya kuboresha maisha ya watu,” anajibu kwa ujasiri mwanafunzi wa usimamizi wa biashara Daniel Wu, akichukua mtazamo wa "glasi imejaa kidogo. Kama hakuna anayechukua ile fursa ya asilimia 10, basi hakuna atakayefanikiwa katika siku zijazo.”
Bwana. Wu amefikisha hadi fainali mradi wake wa kujenga jukwaa la ujuzi wa kidijitali kwa vijana wa vijijini, kuwafundisha kuhusu akili mnemba AI, na ujuzi wa programu, katika Mashindano ya Ubunifu kwa Vijana yanayoendeshwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa UNIDO.
Hii ilimpelekea kualikwa kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Viwanda wa UNIDO mjini Riyadh ambako, leo Jumatano, ameshiriki katika kikao cha Bunge la Vijana ambalo ni jukwaa la kimataifa la mdahalo linaloandaliwa kwa pamoja na UNIDO na Wizara ya Viwanda na Rasilimali za Madini ya Saudi Arabia MIM.
Vijana wengi wenye mawazo ya kibiashara katika mkutano huo wamekuwa na hamasa tele na shauku ya kutumia nafasi za kujenga mitandao ikiwa ni pamoja na kukutana na washauri, watunga sera na wawekezaji watarajiwa.
Ratiba imejumuisha mijadala shirikishi, maonesho ya ubunifu na vipindi vya uongozi wa kitaalamu.
Vijana wametoa suluhu bunifu katika nishati jadidifu, mbinu za uchumi mviringo na utengenezaji wa kidijitali. Mabadilishano haya yamewapa watunga sera na viongozi wa viwanda fursa ya kuzungumza moja kwa moja na vijana kuhusu jinsi mawazo yao yanavyoweza kupanuliwa na kutumiwa katika mazingira mbalimbali.
Tunajua jinsi kizazi chetu kinavyofikiri
Licha ya takwimu zinazoonesha vizingiti vingi pamoja na historia finyu ya kazi ikilinganishwa na wajasiriamali wakongwe Bwana. Wu hasumbuliwi na changamoto hizi. Anasisitiza kuwa vijana wanastahili kuwekeza kutokana na mtazamo wa kipekee wanaoleta.
“Tumekulia kwenye kompyuta, kwenye intaneti, na tunajua jinsi watu wanavyohusiana na aina tofauti za maudhui. Tunaelewa vizuri jinsi kizazi chetu soko kubwa lijalo kinavyofikiria, ndiyo maana tuna uwezo mkubwa kuliko wawekezaji wakubwa,” anasema.
Kwa kutenga siku nzima kwa ajili ya vijana, Mkutano wa Kimataifa wa Viwanda umetuma ujumbe ulio wazi:
mustakabali wa viwanda utaamuliwa sio tu na viongozi waliopo, bali pia na ubunifu, uthabiti na ujasiri wa kizazi kijacho.
Huko Riyadh, mustakabali huo umepata sauti yenye nguvu.
Siku ya kizazi kijacho katika mkutano wa kimataifa wa viwanda
- Generation Future Day ilibuniwa kuwawezesha wavumbuzi, wajasiriamali na wanamabadiliko vijana, kuhakikisha mitazamo yao inaingizwa katika mjadala wa kimataifa wa viwanda.
- Kipengele muhimu kimekuwa Shindano la Ubunifu kwa Vijana, lililolenga kuonesha miradi ya vitendo inayokabili changamoto kubwa duniani. Washiriki wamewasilisha miradi kuanzia zana za AI kwa kilimo endelevu hadi mifumo ya nishati jadidifu ya kijamii. Washindi walioteuliwa watapata msaada kupitia UNIDO na mitandao ya washirika, utakaowawezesha kuanzisha majaribio ya suluhu zao katika maeneo mahususi.
- Siku hiyo pia imeshuhudia kuanzishwa kwa Mtandao wa kizazi kijacho au Generation Future Network, jukwaa la kimataifa linalowaunganisha wavumbuzi vijana na washauri, wawekezaji na watunga sera.
- Mtandao huu unalenga kuendeleza ushirikiano baada ya mkutano, na kuunda njia kwa vijana kushawishi sera na vitendo vya viwanda kwa muda mrefu.
- Kikao cha kufunga kimeoa wito wa kuchukua hatua, kuingiza mitazamo ya vijana katika kila ngazi ya utungaji na utekelezaji wa sera za viwanda. UNIDO imesisitiza tena dhamira yake ya kuwaunga mkono vijana kama washirika katika kujenga viwanda shirikishi, thabiti na endelevu.