Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP30 yatoka na ongezeko la fedha za tabianchi na ahadi kuelekea mpito wa mafuta kisukuku

Harakati za asasi za kiraia
© UNFCCC/Diego Herculano Harakati za asasi za kiraia

COP30 yatoka na ongezeko la fedha za tabianchi na ahadi kuelekea mpito wa mafuta kisukuku

Tabianchi na mazingira

Katika matokeo muhimu ya COP30 huko Belém, Brazil, nchi zimekubaliana juu ya kifurushi kikubwa cha kuongeza fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Paris  lakini bila makubaliano ya wazi ya kuanza kuacha matumizi ya mafuta ya kisukuku.

Kilichoamuliwa:

  • Fedha kwa kiwango kikubwa: Kuchangisha dola trilioni 1.3 kila mwaka ifikapo 2035 kwa hatua za tabianchi, nchi zilizoendelea zikiwa mstari wa mbele.
  • Kuimarisha fedha za kukabiliana na athari: Kuzidisha mara mbili fedha za kukabiliana na athari za tabianchi ifikapo 2025 na kuongeza mara tatu kufikia 2035.
  • Mfuko wa hasara na uharibifu: Uendeshaji na mizunguko ya kuongeza fedha kuthibitishwa.
  • Mikakati mipya: Uzinduzi wa Global Implementation Accelerator na Belém Mission to 1.5°C ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kuongeza kiwango cha nia ya nchi.
  • Kupambana na upotoshaji: Nchi kujitolea kukuza uadilifu wa taarifa na kupambana na upotoshaji kuhusu tabianchi.
Uamuzi wa mwisho unaweka kipaumbele mshikamano na uwekezaji, ukiweka malengo makubwa ya kifedha huku ukiacha nje lugha ya kuelekeza mpito wa nishati jambo lililozua wasiwasi kwa mataifa mengi, ikiwemo baadhi ya nchi za Amerika Kusini, Umoja wa Ulaya na makundi ya kiraia.
Huu ni mkutano wa kwanza wa COP kufanyika katika eneo la Amazon na wa kwanza tangu UN itoe onyo kwamba ongezeko la kihistoria la gesi chafu linaifanya kuwa “karibu haiwezekani” kuzuia dunia isivuke 1.5°C bila kuizidi kwa muda mfupi katika miaka ijayo.

Mtazamo wa kina

Baada ya majuma mawili ya mazungumzo makali, maandishi ya mwisho yanataka angalau dola trilioni 1.3 kwa mwaka kufikia 2035 ziwekwe kwa ajili ya hatua za tabianchi, sambamba na kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari na kuanzisha rasmi mfuko wa hasara na uharibifu ulioafikiwa katika COP28.
Pia yanazindua hatua mbili kubwa Mkakati wa kimataifa wa utekelezaji au Global Implementation Accelerator na mkakati wa Belém kuhakikisha nyuzijoto 1.5°C  kusaidia nchi kutekeleza michango yao iliyopangwa kitaifa (NDCs) na mipango ya kukabiliana na athari.
Kwa mara ya kwanza, uamuzi unakubali haja ya kukabiliana na upotoshaji kuhusu tabianchi, ukiahidi kukuza uadilifu wa taarifa na kupambana na simulizi zinazodhoofisha hatua zinazoongozwa na sayansi.
Wiki iliyopita, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva alifungua mkutano akitangaza kwamba ungejulikana kama “COP ya ukweli,” na uamuzi huu umeonekana kama hatua muhimu ya kulinda uaminifu wa umma katika sera za tabianchi hata kama kukosekana kwa lugha ya mpito kutoka mafuta ya kisukuku kunadhihirisha ugumu wa kisiasa katika mazungumzo ya nishati.

Safari kuelekea maridhiano

Safari ya kufikia makubaliano katika mkutano wa hivi karibuni wa nchi wanachama wa UNFCCC haikuwa rahisi hata kidogo.
Mapema wiki hii, makundi ya wananchi wa jamii za asili yalifanya maandamano na vizuizi wakitaka ulinzi mkubwa zaidi kwa Amazon. Ijumaa jioni, moto uliozuka katika ukumbi mkuu wa mkutano ulisitisha mazungumzo wakati muhimu. Wajadiliano walifanya kazi usiku kucha kujenga daraja juu ya masuala ya fedha na kiwango cha hatua huku urais wa Brazil ukiongoza mchakato kuelekea matokeo ya kisiasa yanayowezekana.

Ushirikiano wa kimataifa bado upo hai

Kutoka Mkutano wa nchi 20 tajiri duniani G20 mjini Johannesburg, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma ujumbe wa wazi kwa COP30: Kwenye lango la Amazon, mataifa yamefikia makubaliano yanayoonesha bado yanaweza kuungana kukabiliana na changamoto ambazo hakuna nchi inayoweza kuzishinda peke yake.
Guterres amesema COP30 imeleta maendeleo, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa Global Implementation Accelerator ili kuziba mapengo ya matarajio na kuthibitisha Makubaliano ya UAE, yakiwemo mpito wa haki, wa utaratibu na wa usawa kutoka kwa mafuta ya kisukuku.
Lakini akatahadharisha kuwa “Siwezi kudai kwamba COP30 imeleta kila kitu kinachohitajika.” Kupita kwa 1.5°C kunatoa onyo kali kwamba upunguzaji mkubwa na wa haraka wa hewa chafuzi na fedha za kiwango kikubwa za tabianchi ni muhimu.
“COP30 imekamilika, lakini kazi bado ipo,” ameongeza, akiwasihi wote waliotembea, kujadiliana na kuhamasisha.