Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP30 yakunja jamvi kwa hatua muhimu ya kuharakisha hatua za tabianchi, lakini mgawanyiko bado upo

Ras wa COP30 André Corrêa do Lago (Katikati) akijadiliana na timu yake wakati wa kufunga mkotano huo
© UNFCCC/Kiara Worth
Ras wa COP30 André Corrêa do Lago (Katikati) akijadiliana na timu yake wakati wa kufunga mkotano huo

COP30 yakunja jamvi kwa hatua muhimu ya kuharakisha hatua za tabianchi, lakini mgawanyiko bado upo

Na Na Felipe de Carvalho, Belém
Tabianchi na mazingira

Huko Belém kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa abadiliko ya Tabianchi COP30, majadiliano yamefanyika hadi usiku wa manane, na kupitia mvutano mkali ili kuthibitisha kwamba ushirikiano wa kimataifa kuhusu tabianchi bado unaendelea. 

 

“Uchumi mpya unaibuka. Uchumi wa zamani unaochafua mazingira unakaribia mwisho wa safari,” amesema Mkuu wa  masuala ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa Simon Stiell wakati wa kufunga mkutano huo wa COP30 leo Jumamosi.

Mwelekeo kwa nishati na misitu

Licha ya kushindwa kupata makubaliano ya kusitisha rasmi matumizi ya mafuta ya kisukuku, Rais wa COP30 André Corrêa do Lago ameahidi kusonga mbele na ramani mbili za njia zinazotegemea sayansi na ushirikishwaji, moja ya kusitisha matumizi ya mafuta ya kisukuku kwa usawa, na nyingine ya kusimamisha ukataji wa misitu kuelekea COP31 nchini Uturuki.

Mshiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa Belém, Brazil wakisubiri mjadiliano kukamilika
© UNFCCC/Kiara Worth
Mshiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa Belém, Brazil wakisubiri mjadiliano kukamilika

Kulinda lengo la nyuzi joto 1.5°C

Stiell amesifu mafanikio makubwa ambayo ni mikakati ya kuharakisha utekelezaji wa Mkataba wa Paris, kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, na ahadi za mabadiliko ya nishati yenye usawa.

“Waraka wa Kikosi Kazi, ambayo ni nyaraka kuu ya mkutano, unaunganisha maeneo manne yenye mvutano mkubwa upunguzaji wa uzalishaji wa hewa ukaa, fedha na biashara katika makubaliano ya pamoja, pamoja na maamuzi mengine 17.

Mjadala wa mafuta ya kisukuka haujakamilika

Zaidi ya nchi 80 zimeunga mkono pendekezo la Brazil la ramani ya njia, lakini maandishi ya mwisho yamerejea tu “Makubaliano ya UAE ya COP28 kuhusu kuondoka hatua kwa hatua kwenye mafuta ya kisukuku.”

Mwanasayansi wa Brazil, Carlos Nobre, ameonya kuwa matumizi ya mafuta ya kisukuku lazima yafike ukomo kabisa kati ya mwaka 2040–2045 ili kuepusha ongezeko la joto hatari kwa kiwango kisichodhibitika.

Mshiriki akieleza maoni yake katika majadiliano ya COP30
© UNFCCC/Kiara Worth
Mshiriki akieleza maoni yake katika majadiliano ya COP30

Mpito usioweza kurejeshwa nyuma

Hati hiyo inasema kuwa dunia sasa iko katika mwelekeo usioweza kubadilishwa wa maendeleo yenye utoaji mdogo wa hewa ukaa, ikitaja faida za kiuchumi na kijamii.

Stiell amebainisha kuwa uwekezaji katika nishati jadidifu sasa unazidi ule wa mafuta ya kisukuku kwa uwiano wa mbili kwa moja ishara ambayo masoko na wanasiasa hawawezi kupuuza.

Uwanja mpya: upotoshaji wa taarifa za tabianchi

Kwa mara ya kwanza, nchi zimekubaliana kukuza “uadilifu wa taarifa,” hatua inayoungwa mkono na tamko la Umoja wa Mataifa lililoidhinishwa na mataifa 18.

Mazungumzo yanaendelea kufanyika siku nzima katika COP30 huko Belém, Brazili.
© UNFCCC/Kiara Worth
Mazungumzo yanaendelea kufanyika siku nzima katika COP30 huko Belém, Brazili.

Fedha na kiwango cha juhudi

Nchi wanachama zinalenga kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na madhara ya tabianchi ifikapo 2035 na kuchangisha dola trilioni 1.3 kila mwaka.

Programu ya kazi ya miaka miwili kuhusu fedha inaanza, huku “Mkakati wa Belém kwa ajili ya nyuzi joto 1.5°C” ukilenga kuziba mapengo ya nia na hatua.

Miongoni mwa mipango hiyo ni:

  • Mfuko wa Tropical Forests Forever: Umekusanya dola bilioni 5.5 na sasa una nchi washiriki 53, angalau asilimia 20 ya fedha zinakwenda moja kwa moja kwa watu wa asili na jamii za wenyeji.
  • Mpango wa Afya wa Belém: Hatua ya kwanza ya kimataifa inayolenga vitisho vya kiafya vinavyosababishwa na tabianchi, uliozinduliwa kwa ufadhili wa dola milioni 300 kutoka kwa taasisi 35 za kifilantropia.
  • Muungano wa UNEZA: Mashirika ya umma ya umeme yameahidi dola bilioni 66 kila mwaka kwa nishati jadidifu na dola bilioni 82 kwa usafirishaji wa umeme na miundombinu ya kuhifadhi nishati.
  • Miji, kanda na kampuni: Muungano wa majengo 25,000 umeripoti kupunguza zaidi ya tani 850,000 za hewa ukaa au CO₂ mwaka 2024.

Haki ya tabianchi yawekwa mbele

Nchi pia zimekubaliana kuanzisha utaratibu wa mpito wa haki, unaolenga kuimarisha ushirikiano, msaada wa kiufundi na ujenzi wa uwezo.

Uthibitisho wake umepokelewa kwa makofi makubwa zaidi katika kikao cha mwisho umeonyesha wazi umuhimu wa harakati za kijamii katika kuhakikisha usawa unakuwa nguzo kuu ya mazungumzo ya tabianchi.