Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO imelaani vikali mashambulizi ya ADF Lubero DRC yalioua raia 89

Kaskazini Mashariki mwa Kivu, DRC: Kikosi cha Morocco cha Munigi POB kikifanya doria.
MONUSCO/Aubin Mukoni
Kaskazini Mashariki mwa Kivu, DRC: Kikosi cha Morocco cha Munigi POB kikifanya doria.

MONUSCO imelaani vikali mashambulizi ya ADF Lubero DRC yalioua raia 89

Amani na Usalama

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ujulikanao kama MONUSCO, leo umelaani vikali mashambulizi makubwa yaliyofanywa na kundi lenye silaha la Allied Democratic Forces ADF kati ya tarehe 13 na 19 Novemba 2025 katika baadhi ya maeneo ya Lubero, jimboni Kivu Kaskazini na kukatili maisha ya raia wengi.

Taarifa zilizokusanywa na MONUSCO na kutolewa leo mjini Kinshasa zinaonesha kwamba mashambulizi hayo yaliyofanywa katika utawala wa Bapere na Baswagha yamesababisha vifo vya raia 89, wakiwemo wanawake 20 na idadi ya watoto bado haijulikani. Katika kijiji cha Byambwe, kilichoko kilomita 60 magharibi mwa Lubero, angalau raia 17 wakiwemo wanawake waliokuwa wakipatiwa huduma katika wodi ya uzazi waliuawa ndani ya kituo cha afya kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki. Wakati wa shambulizi hilo, wodi nne zenye wagonjwa ziliwaka moto.

Maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Mabiango, Tunarudi, Sambalysa, Thucha na Butsili, pia yameathirika na ukiukaji mkubwa wa haki, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, wizi wa vifaa vya tiba, kuchomwa kwa nyumba na uharibifu wa mali za jamii ambazo tayari ziko katika hali mbaya ya kibinadamu.

“MONUSCO inatoa rambirambi zake za dhati kwa familia na jamii zilizoathirika na inaonesha mshikamano wa Umoja wa Mataifa na wote waliokumbwa na matukio haya.”

Kauli ya MONISCO iko bayana “vurugu zinazofanywa dhidi ya raia, ikiwemo katika vituo vya afya, zinaweza kuhesabiwa kuwa uhalifu wa vita na ukiukaji mkubwa wa sheria za kibinadamu,” amesema Bwana Bruno Lemarquis, Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa chini DRC na Kiongozi Mtendaji wa MONUSCO.

MONUSCO inaendelea kujitolea kikamilifu kusimama na jamii na itaendelea kusaidia mamlaka ya Congo katika juhudi zake za kulinda raia, kuzuia ukiukaji wa haki za binadamu na kupambana na utoro wa sheria.

MONUSCO pia inashirikiana kwa karibu na mamlaka za serikali, Jeshi la Wananchi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC, washirika wa kikanda wanaoshiriki operesheni za pamoja, na wadau wa ndani.

MONUSCO inaendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa raia katika maeneo ambako bado ipo. Hii ikijumuisha Operesheni Nyondo iliyofanywa hivi karibuni na Kikosi cha Uingiliaji, ambayo ilisaidia kuzuia mashambulizi zaidi ya ADF katika eneo la Komanda. Kupitia Operesheni Safisha, FARDC na wanajeshi wa Kikosi cha Uingiliaji wanaendelea kuwafuatilia wanachama wa ADF katika maeneo yaliyopo kati ya Beni na Eringeti na Kasindi.

Vilevile, Operesheni MidNight Guard, ambayo inaendelea, inalenga kuhakikisha usalama wa vituo vikuu vya watu kando ya Eringeti katika saa za usiku.

MONUSCO inahimiza mamlaka ya DRC kuanza haraka uchunguzi huru na unaoaminika ili kubaini wahalifu na washirika wao wa mauaji haya na kuwafikisha mbele ya sheria. Bwana Lemarquis amerudia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa makundi yote yenye silaha ya ndani na ya kigeni kusalimisha silaha zao bila masharti yoyote.