COP30: Wakati wa ahadi hewa za tabianchi umepita watu wanataka matokeo asema Guterres
COP30: Wakati wa ahadi hewa za tabianchi umepita watu wanataka matokeo asema Guterres
Wakati mazungumzo ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30 yakiendelea mjini Belém, Brazil, Katibu Mkuu wa UN António Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo ametoa onyo kali kwa viongozi wa dunia, akisisitiza dharura ya kuchukua hatua za dhahiri dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi.
Amesema “Amesema “Jamii zilizo mstari wa mbele zinaangalia zikihesabu nyumba zao zilizozamishwa na mafuriko, mavuno yaliyossambatatika, vyanzo vya maisha vilivyopotea na kuuliza kwa kiasi gani zaidi waendelee kuteseka? Wamesikia visingizio vya kutosha, sasa wanataka matokeo”.
Kuzingatia ulinzi wa watu kwanza
Guterres amesisitiza umuhimu wa haraka wa fedha za kujenga mnepo ili kulinda watu walioko hatarini. “Kwa mamilioni, mnepo si lengo la nadharia. Ni tofauti kati ya kujenga upya na kubebwa na mafuriko, kati ya kupanda tena na kufa njaa, kati ya kubaki kwenye ardhi ya mababu na kuipoteza milele,” amesema. Ameonya kuwa dunia inakabiliwa na hatari ya joto kuzidi lengo la nyuzi joto 1.5°C mapema kufikia miaka ya 2030, jambo ambalo linafanya kuwa muhimu zaidi “kuongeza kiwango cha fedha za kujenga mnepo mara tatu ifikapo 2030.”
Pia ametaka haraka mtaji wa Mfuko wa Hasara na Fidia, ambao amesema “uko tayari lakini bado haujajazwa vya kutosha.”
Wito wa kupunguza uchafuzi wa hewa
Kuhusu kupunguza uchafuzi wa hewa, Guterres ameonekana kuwa mkali, “Miaka kumi baada ya Makubaliano ya Paris, tumesonga lakini si vya kutosha. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mtifa la Mazingira UNEP ya Emissions Gap inaonesha kuwa Mipango ya Kitaifa ya Kupunguza Uchafuzi hata ikitekelezwa kikamilifu inatuelekeza kwenye joto zaidi ya nyuzi joto 2°C. Hii ni hukumu ya kifo kwa wengi.”
Alisisitiza kuwa mipango ya kitaifa lazima iwe msingi, sio kizingiti, na kuhamasisha nchi kuongeza kasi ya mchakato wa nishati mbadala.
Mpito wa haki wa nishati sahihi
Katibu Mkuu amesisitiza haja ya mpito wa haki kutoka matumizi ya mafuta ya kisukuku kwenda kwenye nishati safi. “Lazima tuanze mpito wa haki, uliopangwa na usio na upendeleo kutoka kwenye mafuta ya kisukuku kama ilivyokubaliwa COP28 Dubai. Hii ni lazima kwa ajiliya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na ni kipimo cha utulivu wa uchumi, usalama wa nishati, na utawala unaowajibika,” amesema.
Guterres amesisitiza msaada kwa wafanyakazi na jamii zinazorudia kwenye makaa, mafuta, na gesi kwa mafunzo na fursa mpya, akitaka matokeo ya Belém yaendeleze mpito wa haki unaolingana na dunia ya nyuzi joto 1.5°C.
Fedha za kuendelea hatua
Guterres amesisitiza kuwa hakuna hatua yoyote ya hali ya hewa inayowezekana bila ufadhili thabiti. “Tunahitaji njia ya kuaminika ya kutimiza Lengo la Fedha la Baku. Wakati nchi zilizoendelea zikiongoza kuhamasisha angalau dola bilioni 300 kila mwaka ifikapo 2035 na njia wazi ya kufikia dola trilioni 1.3 kwa mwaka ifikapo 2035,” amesema.
Pia ametaka marekebisho ya mfumo wa kifedha wa kimataifa na ushirikiano mkubwa zaidi wa Benki za Maendeleo ya Kimataifa kufungua fedha za sekta binafsi kwa kiwango kikubwa.
Uongozi na dharura
Akihitimisha hotuba yake, Guterres ametoa changamoto moja kwa moja kwa wajumbe wa mazungumzo “Tafadhali shiriki kwa uaminifu kufikia makubaliano yenye uthubutu. Nyuzijoto 1.5°C lazima iwe mstari wako wa mwisho. Hii ni saa ya uongozi. Jitahidi. Fuata sayansi. Weka watu mbele ya faida. Na tafadhali zingatia mstari wa mwisho.”
Ujumbe wake umeainisha hatari kubwa kwenye COP30, ukisisitiza kwamba hatua za pamoja na za haraka ni muhimu ili kuzuia madhara yasiyoweza kurekebishwa.
Brazil yapendekeza ramani kuelekea mpito wa nishati
Jumatano usiku, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva aliongea kuhusu jinsi mazungumzo ya COP30 yanavyoweza kusaidia kujenga njia endelevu ya kupunguza matumizi ya mafuta ya kisukuku.
“Hicho ndicho kilichosababisha tutenge wazo la ramani ya njia kwa sababu tunahitaji kuonesha jamii kwamba tunachukua jambo hili kwa dhati. Hatutaki kuwalazimisha watu chochote, wala kuweka muda wa mwisho. Kila nchi lazima iamue ni nini inaweza kufanya kwa wakati na uwezo wake. Lakini lazima tupunguze uzalishaji wa gesi chafuzi. Na ikiwa mafuta ya kisukuku yanazalisha uzalishaji mkubwa, lazima tuanze kufikiria jinsi ya kuishi bila hayo na jinsi ya kujenga njia hiyo. Na ninasema hili kwa urahisi mkubwa, kama kiongozi wa nchi inayotoa mafuta, inayochimba mafuta lita milioni 5 kwa siku.”
Rais Lula ameongeza kuwa Brazil pia ni nchi inayotumia zaidi ethanol iliyochanganywa kwenye petroli na kuzalisha kiasi kikubwa cha biodiesel.
Sifa kwa ushiriki wa umma
Rais huyo wa Brazil amesema kuwa ili mpito wa nishati uwe wa kweli, makampuni ya mafuta, makampuni ya madini na matajiri sana lazima wachangie sehemu yao. Pia amesisitiza kwamba benki za kimataifa lazima zisiweke riba za juu sana kwa nchi za Afrika na nchi maskini zaidi za Amerika ya Kusini, na badala yake zigeuze sehemu ya madeni hayo kuwa uwekezaji.
Lula amesifu ushiriki wa umma katika COP30, akibainisha kuwa maandamano yaliyoandaliwa tarehe 15 Novemba yalikuwa “mazuri sana na yenye utaratibu.”
Pia amesherehekea ushiriki ulioweka rekodi wa Watu wa Asili 3,500 kwenye mkutano huo, pamoja na ushiriki kamili wa wanawake.