COP30: Shule moja Amazon yageuka kuwa mwanga wa mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
COP30: Shule moja Amazon yageuka kuwa mwanga wa mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Safari ya mashua kutoka Belém hadi Barcarena ni kupitia mto wenye mwanga unaong’aa na misitu ya smariti, ambapo Amazon inakutana na Atlantiki kwa urembo wa ajabu. Lakini chini ya mandhari hiyo mwanana, mabadiliko ya tabianchi yameanza kubadilisha taratibu kanuni za maisha.
Kando ya mto huo wenye mchanga, shule ndogo yenye paa lililosheheni paneli za sola inasimama kama hadithi tofauti ya mnepo, ubunifu, na matumaini kwa kizazi kijacho.
Shule iliyoundwa kwa ajili ya zama zijazo
Kwa muda wa miaka mitatu, Shule ya Manispaa ya Maria Naura Gouvêa imekuwa ikitumia moja ya mada kuu za Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi COP30, ujumishaji na ubadilishaji.
Kuta zake zinazostahimili mafuriko na mmomonyoko wa udongo, paa lililopambwa kwa paneli za sola mifumo ya nishati ya jua, na intaneti kupitia satellite inaiweka shule hii kuwa kimbilio salama na adimu. Kisima cha mita 150 kinahakikisha upatikanaji wa maji safi mali adimu katika sehemu nyingi za eneo hili.
Wakati wa ziara yetu, Kamal Kishore, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Majanga (UNDRR), ameiita shule hiyo “taarifa ya mwanga,” na kuongeza kuwa “Ningependa kuona angalau shule 100,000 kama hii duniani kote.”
Ukame, mmomonyoko na kupanda kwa kina cha bahari
Meya wa Barcarena, Renato Ogawa, ameelezea kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi hapa ni ndogo lakini zinaharibu,
“Matukio makuu ni ukame wa mito na mikondo. Wiki moja, wanafunzi wanaweza kufika kwa mashua, wiki inayofuata, kutokana na mabadiliko ya mawimbi, hawawezi kufika shule kwa wakati na lazima watembelee kando ya milima na fukwe za maji safi ambazo, kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha kina cha bahari, zimeanza kufurika, zikisababisha mmomonyoko.”
Kuta za kudhibiti sasa zipo kando ya mito, lakini Bw. Ogawa ameonya “Kama hakuna kitakachofanywa, kwa miaka ijayo tutahitaji kuinua na kupanua kuta hizo.”
Kuongezeka kwa kiwango cha bahari pia kunabadilisha mienendo ya samaki, kuhatarisha lishe ya jamii za watu wa asili kwani maji ya mito yanazidi kuwa yenye chumvi.
Changamoto hizi zimeweka Barcarena mstari wa mbele wa ujumlishaji wa mabadiliko ya tabianchi, zikipata utambuzi wa kimataifa.
Uongozi wa kijiografia kwenye jukwaa la kimataifa
Mnamo 2023, Barcarena ilikabidhiwa heshima ya kuwa Kitovu cha Uwezo wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi cha 25 duniani na cha kwanza katika Amazon.
Vituo hivi vilivyotambuliwa na UNDRR ni miji inayojulikana kwa rekodi yao thabiti katika kupunguza hatari za majanga na ubadilishaji wa hali ya hewa, na vinaahidi kuongoza miji mingine kwa kushirikisha suluhu halisi na utaalamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat, Anaclaudia Rossbach, amesisitiza umuhimu wa COP30 kuimarisha sauti kama ile ya Bwana. Ogawa
“Tunahitaji kulinda watu ili kulinda sayari. Na jambo jingine muhimu ni umuhimu wa serikali za mitaa, hatua za mitaa na uongozi wa mitaa.”
Ameongeza kuwa utambuzi pekee haukutoshi “Lazima ufuatane na mifumo thabiti na imara ya utekelezaji.”
Tofauti katika eneo la Amazon
Waziri wa Miji wa Brazil, Jader Filho, amepongeza maendeleo ya Barcarena lakini akabainisha kuwa “Shule hii ni tofauti na haiwakilishi hali ya elimu katika Amazon kubwa. Lakini inaonesha kile kilichowezekana pale ambapo fedha na dhamira ya kisiasa vinaungana.”
Wanafunzi walionesha miradi inayogeuza mafuta ya kupikia kuwa sabuni, kutengeneza rangi za asili kutoka mboga, na kupanda miti kupambana na joto.
Lyndisse Wandra Santos amehitimisha dhamira yao kwa kusema “Kila mti ulio pandwa ni ishara ya upendo na matumaini, kujenga mnepo ni kuendelea kusonga mbele licha ya changamoto.”
Kamal Kishore kwa upande wake amesema amevutiwa na maono yao “Brazil ni hadithi ya mafanikio,” akataja miji zaidi ya 2,000 duniani kote iliyo katika kampeni ya “kuifanya miji kuwa na mnepo” au Making Cities Resilient, nyingi zikishirikiana na Brazil.
Urithi wa COP30 katika eneo la Barcarena
Meya Ogawa amebainisha kuwa COP30 tayari imeharakisha uwekezaji,
“Mwishoni mwa mwaka, tutafikia asilimia 90 ya tiba ya maji taka na maji safi kwa asilimia 95 ya manispaa. Vinginevyo malengo haya yangechukua miaka 10 hadi 15.”
Kile kinachofuata kwenye ajenda yak, kubadilisha mashua za usafiri wa umma kusafiri kwa kutumia nishati safi.
Kiongozi wa UN-Habitat, Bi. Rossbach, ameonya kuwa uwekezaji kama huu unahitajika haraka sehemu nyingine, hasa katika makazi, kwani mamilioni wanaishi katika hali hatarishi chini ya vitisho vinavyoongezeka vya tabianchi.
Kutoka COP ya misitu hadi COP ya miji
Ameelekeza macho yake kwenye mtaa wa Maré, Rio, ambapo joto linaweza kupanda hadinyuzijoto 6°C juu ya wastani wa jiji, kulingana na takwimu zilizokusanywa na wenyeji wenyewe.
Matumaini yake ni kwamba “COP hii ya Misitu kama COP30 inavyoitwa kwa kuwa inafanyika Belém, Brazil, karibu na msitu wa mvua wa Amazon lazima pia iimarishe ajenda ya miji, ikitoa kipaumbele kwa ulinzi wa wale walio hatarini zaidi.”
Kadri COP30 inavyoendelea Belém, hadithi ya Barcarena inatoa somo lenye nguvu la uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaanza ngazi ya jamii. Kutoka madarasa yanayopatikana kwa kutumia nishati ya jua hadi miradi inayosimamiwa na wanafunzi, manispaa hii ya Amazon inaonesha kuwa ujumuishaji sio tu unawezekana tayari unaendelea.
Na katika dunia inayokabiliana na kuongezeka kwa kina cha bahari na mawimbi yanayobadilika, masomo haya ni muhimu zaidi kuliko hapo awali.