Hali ya kibinadamu Yazidi kuwa tete DRC - ICRC
Hali ya kibinadamu Yazidi kuwa tete DRC - ICRC
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali ya kibinadamu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini bado ni tete.
Mkurugenzi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Kanda ya Afrika Patrick Youssef ambaye amerejea hivi karibuni kutoka DRC amewaleza waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi kwamba raia wa DRC wanaendelea kubeba mzigo mzito wa mapigano, hata wakati shughuli chache za kibiashara zikiendelea kurejea Goma.
Ametoa tahadhari kuwa mgogoro huo unakabiliwa na upungufu mkubwa wa ufadhili, ukatili wa kingono unaongezeka, na zaidi ya asilimia 70 ya watu waliojeruhiwa kwa silaha mwaka huu ni raia.
Msaada wa kisaikolojia wahitajika
Amesma takriban watu 22,800 wameomba msaada wa kisaikolojia na hao ni wale tu waliokuja kuomba msaada.
Youssef anazitaka pande zote zenye silaha kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kuruhusu upatikanaji wa huduma muhimu kama maji, usafi na afya.
Alisisitiza kuwa, ingawa mifumo hii ipo kwa maandishi, lazima itumike kwa vitendo. Hospitali katika eneo hilo zinahitaji haraka dawa na vifaa, lakini mara nyingi hazifikiki kutokana na mapigano yanayoendelea.
ICRC iko tayari kuongeza msaada ufikiaji ukiwezekana
ICRC imesisitiza umuhimu wa kurahisishwa kwa ufikishaji wa huduma za maji, usafi, na huduma za afya.
Mara tu fedha na ufikiaji vitakapoimarika, shirika hilo linasema lipo tayari kuchukua jukumu kubwa zaidi mashariki mwa DRC.
Youssef amesisitiza kuwa wavamizi wa silaha lazima waheshimu utu wa kila mtu.
Ingawa jitihada za kumaliza mzozo zinatambulika, ICRC inaendelea kushuhudia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo.