Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP30: WHO na Brazil zasema wakati wa kuchukua hatua ni sasa kutekeleza Mpango wa Afya wa Belém

Wanawake na mtoto wakichota maji kwenye makopo katika kijiji cha vijijini cha Ethiopia.
© WHO/Nitsebiho Asrat Kutokuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunasababisha vifo vya mamilioni ya watu kila mwaka.

COP30: WHO na Brazil zasema wakati wa kuchukua hatua ni sasa kutekeleza Mpango wa Afya wa Belém

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO na Serikali ya Brazil wamezitaka nchi kuchukua hatua za haraka kutekeleza Mpango wa Afya wa Belém, wakati mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi COP30 ukiendelea mjini Belém, Brazil.

Wito huo umetolewa kupitia ripoti maalum ya pamoia iliyochapishwa na WHO, Serikali ya nchi ya Brazil ambayo ni mwenyekiti wa COP30, Wizara ya Afya ya Brazil na Wataalamu wa kimataifa, leo tarehe 14 mwezi Novemba 2025, ikionesha kuwa mabadiliko ya tabianchi tayari yamesababisha dharura ya kiafya duniani.

Ripoti hiyo, iliyopewa kichwa Ripoti Maalum ya COP30 kuhusu Afya na Mabadiliko ya Tabianchi: Kutekeleza Mpango wa Afya wa Belém, imeonesha kuwa ongezeko la joto na mifumo ya afya inayodorora vinaendelea kugharimu maisha ya watu duniani kote.

Ripoti hii imekuja mara baada ya kuzinduliwa kwa Mpango Kazi wa Afya wa Belém, moja ya nguzo kuu za uenyekiti wa Brazil katika COP30, uliotangazwa jana tarehe 13 mwezi huu wa Novemba 2025 katika Siku Maalum ya Afya ya COP30.

“Mabadiliko ya tabianchi ni janga la kiafya siyo kwa miaka ijayo, bali sasa,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. "Ripoti hii inatoa ushahidi wa athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi kwa watu na mifumo ya afya, sambamba na mifano halisi ya hatua ambazo nchi zinaweza kuchukua kulinda afya na kuhimili mishtuko inayotokana na tabianchi."

Mvulana mdogo anakimbia kuelekea kwenye mwamba mkubwa wenye kidimbwi kidogo cha maji katika eneo kavu na tasa katika wilaya ya Ban Phai, mkoa wa Khon Kaen, Thailand.
© UNICEF/Roengrit Kongmuang Mvulana anacheza katika mandhari iliyoathiriwa na ukame kaskazini mashariki mwa Thailand.

Madhara ya joto kali kote duniani

Ripoti imeeleza kuwa zaidi ya watu 540,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na joto kali, huku hospitali 1 kati ya 12 duniani ikikabiliwa na hatari ya kufungwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi tabianchi. Zaidi ya watu bilioni 3.3–3.6 wanaishi katika maeneo yaliyo hatarini sana.

Kwa sasa, ongezeko la joto duniani limevuka kiwango cha nyuzi joto 1.5°C, na hatari ya hospitali kuharibiwa na matukio ya hali mbaya ya hewa imeongezeka kwa asilimia 41 ikilinganishwa na mwaka 1990.

Ripoti inaonya kuwa bila kupunguzwa haraka kwa uzalishaji wa hewa ukaa, idadi ya vituo vya afya vilivyo hatarini inaweza kuongezeka mara mbili ifikapo katikati ya karne. Sekta ya afya yenyewe inachangia asilimia 5 ya hewa ukaa duniani.

Pengo kubwa katika mipango ya nchi

Licha ya ukubwa wa tishio, ni asilimia 54 tu ya mipango ya afya ya kitaifa inayofanyiwa tathmini ya hatari, na chini ya asilimia 30 ya tafiti huzingatia vipengele kama kipato, jinsia, au watu wenye ulemavu.

Ushahidi ni Dhahiri, kulinda mifumo ya afya ni moja ya uwekezaji bora zaidi kwa nchi yoyote, amesema Profesa Nick Watts, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Ushauri wa Kitaalam na Mkurugenzi wa Kituo cha NUS cha Tiba Endelevu.

Kuweka hata kiwango cha asilimia 7 ya kiasi cha fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye afya kunaweza kulinda mabilioni ya watu na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea wakati wa majanga,”ameongeza.

Hatua zinazoendelea kuchukuliwa

Kati ya kipindi cha mwaka 2015 na 2023, idadi ya nchi zilizo na Mifumo ya Taifa ya Tahadhari za Mapema kwa ajili ya Kukabiliana na Majanga (MHEWS) iliongezeka maradufu kufikia 101, zikifunika takribani theluthi mbili ya idadi ya watu duniani. Hata hivyo, niasilimia 46 tu ya Nchi Maskini (LDCs) na asilimia 39 ya Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo (SIDS) zilizo na mifumo madhubuti.

Mama na binti wakipita kwenye maji ya mafuriko kwenye barabara iliyozama majini huko Feni, Bangladesh.
© UNICEF/Sultan Mahmud Mukut Mama akiwa na mwanaye wakitembea katika maji ya mafuriko Feni, Bangladesh.

Ripoti inazitaka serikali:

  • Kujumuisha afya katika Michango Inayokusudiwa Kufikiwa Kitaifa ya Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (NDCs) na Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NAPs);
  • Kutumia akiba ya kifedha kutoka kwenye upunguzaji wa kaboni kufadhili uhimilivu wa sekta ya afya;
  • Kuwekeza kwenye miundombinu imara ya afya, hasa hospitali;
  • Kuwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika kutoa suluhisho linaloendana na mazingira yao.

Wakati huo huo, Brazil imezindua ripoti ya ziada inayoangazia umuhimu wa ushiriki wa kijamii katika utekelezaji wa Mpango wa Afya wa Belém, ikionya kuwa jamii zilizo hatarini ndizo zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Mpango huo unaongozwa na misingi ya usawa wa kiafya na haki ya tabianchi, pamoja na uongozi shirikishi, na umejengwa katika maeneo matatu:

1. Ufuatiliaji wa afya unaozingatia tabianchi;

2. Sera na mikakati yenye ushahidi;

3. Ubunifu, uzalishaji na afya-dijitali.