Fahamu kuhusu ugonjwa wa kisukari na jinsi ya kujikinga
Fahamu kuhusu ugonjwa wa kisukari na jinsi ya kujikinga
Tarehe 14 Novemba kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kisukari na mwaka huu kauli mbiu ni “Kisukari katika hatua mbalimbali za maisha.” Je wafahamu ugonjwa huu unampata mtu gani na unawezaje kujikinga usiugue?
Lengo la siku hii ni kutoa fursa ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa kisukari kama suala muhimu la afya ya umma duniani, kueneza maarifa na ufahamu na pia kuleta mabadiliko ya kudumu kwa wote walioathirika na ugonjwa wa kisukari.
Daktari Sania Martin Kasiandu ni Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani hasa Kisukari na homini katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mloganzila nchini Tanzania ameeleza kuhusu ugonjwa huo“Kisukari ni ugonjwa wa muda mrefu na usioambukizwa ambapo kiwango cha sukari kwenye damu kinakuwa juu kuliko kawaida kwasababu mwili hauzalishi insulini ya kutosha au hautumii insulini ipasavyo.”
Dkt. Kasiandu ameeleza kuna aina mbalimbali za kisukari lakini kuna aina mbili zinazojulikana kama Type1 na Type 2 .
“Type 1 ni ile ambayo mwili umeshindwa kabisa kutengeneza Insulini na hii huanza utotoni au kwa kijana, mgonjwa anategemea insulini maisha yake yote. Aina ya pili (Type 2) Mwili unatengeneza Insulini lakini haitumii vizuri kitu ambacho kinajulikana kitaalamu kama insuline resistant. Hapo zamani ilikuwa inaonekana kwa wazee lakini sasa vijana wengi wanaipata. ”
Dalili za sukari
Haijalishi mgonjwa anaugua aina gani, dalili zote ni sawa “Dalili kuu zinazoweza kuwapata watu wengi zinaweza kuwa ni kukojia mara kwa mara, kusikia kiu kali au njaa kali, kupungua uzito na kuchoka mara kwa mara.”
Lakini nini hasa kinasababisha mtu kuugua ugonjwa wa kisukari? Daktari bingwa anaeleza “Sababu zinatofautia kati na kila aina ya Kisukari. Type 1 inatokana na pale mwili unapoona kongosho ni adui na kinga ya mwili inaanza kupingana na kongosho kwahiyo kongosho inakuwa haina uwezo tena wa kutengeneza insulini na hapo mtu ataweza kupata kisukari cha aina ya kwanza. Pia inaweza kuwa sababu ya vinasaba vya mtu.”
Aina ya pili (Type 2) na jinsi tunavyoishi maisha yetu kula vibaya, kutofanya mazoezi, kunywa pombe sana nakadhalika.”
Jinsi ya kuepuka kupata kisukari aina ya pili
Je, mtu anafanye nini ili kuepuka kupata kisukari aina ya pili?
“Kitu cha kwanza ni kupunguza uzito kupita kiasi, ukipunguza usito kwa asilimia 5 mpaka 7 ya uzito wa mwili hupunguza hatari ya kupata kisukari kwa kiwango kikubwa. Kitu cha pili kula chakula chenye lishe bora- punguza vyakula vya kukaanga, vyenye sukari nyingi kama juisi, soda, chocolate au keki na uongeze mbogamboga na matunda pamoja na nafaka siziso kobolewa.”
Ameongeza kuwa mtu anapaswa kuchagua protini nzuri kama samaki, kuku, maharage na kula nyama nyekundu kama nyama ya ngombe na nguruwe kwa kiwango kidogo kwasababu zina mafuta mengi. Pia inashauriwa kupunguza kula unga mwingi na wanga uliosindikwa kama mkate.
“Kitu kingine ni kufanya mazoezi mara kwa mara, mazoezi yanasaidia mwili kutumia insulini vizuri . Angalau dakika 30 za kutembea kwa kasi mara tano kwa wiki au kuogelea, kupanda ngazi, kuendesha baiskeli hata kutembea dakika 10 baada ya mlo kunasaidia sana kupunguza sukari- hapa namaanisha dakika 10 baada ya kifungua kinywa, dakika 10 baada ya mlo wa mchana na dakika 10 baada ya mlo wa usiku, jumla hapo ni dakika 30 kwa siku na hii itasaidia kupunguza kiwango cha sukari kwenye mwili.”
Kudhibiti msongamano wa mawazo, msongo wa mawazo hupandisha homoni zinazoleta upinzani wa insulini kwenye mwili kwahiyo kinachotakiwa ni kufanya mazoezi, kupumzika vya kutosha kutasaidia kupunguza msongo wa mawazo.
Punguza kunywa pombe kupita kiasi, unywaji wa pombe nyingi huongeza uzito, mafuta ya tumbo na hatari ya kisukari.
Punguza kunywa vinywaji vyenye sukari, kama soda, juisi zilizo sindikwa, vinywaji vya kuongeza nguvu, na vitu vyenye sukari sana kama milkshake, badala yake kunywa maji, chai isiyo na sukari, juisi ya matunda asilia kiasi kidogo.
“Kulala masaa 7 mpaka 9 kila siku ni muhimu sana. Usingizi mdogo husababisha kuongeza uzito na insuline resistance. “
Ugonjwa wa kisukari unaweza kuathiri watu katika hatua zote za maisha, ikiwa ni pamoja na utoto, miaka ya uzazi, umri wa kufanya kazi na utu uzima mkubwa.
Ujumbe wa WHO
Kauli mbiu ya Siku ya Kisukari Duniani ya WHO mwaka huu, "Kisukari katika hatua mbalimbali za maisha," inatambua kuwa kila mtu anayeishi na ugonjwa wa kisukari anapaswa kupata huduma jumuishi, mazingira ya usaidizi na sera zinazokuza afya, utu na kujisimamia. Kampeni hii inasisitiza umuhimu wa mbinu ya maisha kwa kuzuia, kudhibiti na ustawi wa jumla wa kisukari.
Ujumbe muhimu kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO katika maadhimisho ya mwaka huu ni kuwa ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yeyote kuanzia utotoni, ujana hadi uzee hivyo kusaidia ustawi na kujitunza kutawezesha watu wenye ugonjwa wa kisukari katika kila umri.