Chanjo Gaza: WHO, UNICEF na UNRWA waanza uchanjaji zaidi ya watoto 44,000
Chanjo Gaza: WHO, UNICEF na UNRWA waanza uchanjaji zaidi ya watoto 44,000
Mashirika ya Umoja wa Mataifa WHO, UNICEF na UNRWA wameanzisha kampeni ya pamoja ya Uchanjaji watoto waliokosa huduma muhimu za kuokoa maisha kutokana na miaka miwili ya machafuko katika Ukanda wa Gaza umeanza kutekelezwa na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la afya duniani, la kuhudumia watoto UNICEF na la kusaidia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.
Kampeni hii inayowalenga watoto kuanzia siku moja hadi miaka mitatu, imeanza majuzi tarehe 10 mwezi huu wa Novemba na itaendelea hadi tarehe 18 Novemba. Utoaji wa huduma hizi muhimu za afya kwa maelfu ya watoto unategemea kuheshimiwa kwa usitishaji mapigano kuhakikisha familia, wataalamu wa afya na wahudumu wa kibinadamu wanaweza kufika katika vituo vya chanjo kwa uhuru na usalama.
Video inaanzia katika Kituo cha Afya cha Al-Daraj kilichoko Gaza City, Palestina. Wazazi wanaume kwa wanawake wakiwa na watoto wao wamefurika kituoni hapo, wakihudumiwa na wahudumu wa afya kabla ya kupata chanjo.
Refqa Skaik, Afisa wa Kiufundi wa Polio katika WHO, anasema, “kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, UNICEF, Jumuiya Mwezi Mwekundu ya Palestina na sisi WHO, tunatoa utaalamu na msaada wa kiufundi katika utekelezaji wa kampeni hii, hususan kwa kundi la watoto walio chini ya miaka mitatu, wanaokadiriwa kufikia watoto 44,900.”
Mahmoud Saleh, mhudumu wa chanjo, anasema:
“Ndiyo, mahudhurio katika Kituo cha Afya cha Shuhada Al-Daraj ni makubwa sana. Tunawaelekeza watu ambao hawajapokea chanjo hizi kutokana na kuhama au kuchelewa, kufika kwenye vituo hivi haraka iwezekanavyo.”
Afisa mwingine wa chanjo baada ya kumchanja mtoto mmoja anamweleza mama mtoto akisema, “anapata sindano begani kushoto kumkinga dhidi ya kifua kikuu, na sindano nyingine kwenye paja la kushoto kumkinga dhidi ya homa ya ini aina ya B. Sindano hizi hazina madhara, homa wala usumbufu. Chanjo inayofuata itakuwa tarehe 6 Desemba ambapo atapokea chanjo ya kila mwezi. Ni muhimu kufika kwa wakati, kwani chanjo za kila mwezi hutolewa siku za Jumamosi pekee.”
Kutoka Kituo cha Afya cha Al-Daraj, safari inaendelea hadi kliniki ya Mwezi Mwekundu, eneo la Al-Zaytoon, Gaza City. Hapa pia shughuli ni moja tu, kwenye bega, kwenye paja, ni mwendo wa chanjo tu.
Iftikhar Hajji, mama wa mtoto anayechanjwa anasema:
“Chanjo zinawalinda watoto kwa sababu kuna uchafuzi wa mazingira na magonjwa. Chanjo bila shaka huzuia magonjwa, hivyo ni lazima tuzitumie kuwalinda watoto.”
Naam, kama si suala la muda kuwa ukuta ningekupeleka katika Kiliniki ya Al-Salam na hata katika Hospitali ya Nasser katika eneo la Khan Younis. Kote huko nako ni mwendo wa sindano kwenye bega, sindano kwenye paja, ilimradi watoto wote waliokosa chanjo Gaza, sasa wawe salama dhidi ya magonjwa.