COP30: Watu waliofurushwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi watoa wito wa hatua za urekebishaji
COP30: Watu waliofurushwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi watoa wito wa hatua za urekebishaji
Janga la tabianchi linaendelea kubadili ramani ya uhamaji wa watu duniani. Mafuriko, mawimbi ya joto, ukame na dhoruba vinalazimisha mamilioni ya watu kuzikimbia nyumba zao kila mwaka. Wengi wao hubaki ndani ya nchi zao, lakini bado wakikosa makazi salama. Wataalamu wanaonya kwamba katika miaka ijayo, mataifa mazima yanaweza kutoweka kutokana na kupanda kwa viwango vya bahari au ukame mkali unaozuia maisha.
Uhamaji wa tabianchi katika ajenda ya urekebishaji
Katika mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), unaofanyika mjini Belém, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linahimiza wajumbe kutambua uhamaji unaosababishwa na tabianchi kama sehemu muhimu ya ajenda ya urekebishaji.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Ugochi Daniels, ameiambia UN News (Idhaa ya Umoja wa Mataifa) kwamba hatua za urekebishaji lazima zisaidie kupunguza hatari ya watu kulazimika kuhama kutokana na athari za tabianchi, na pia kulinda wale ambao tayari wako njiani kwa kuweka njia salama, za kawaida na zenye heshima.
“Wale wanaochagua kubaki lazima wawe salama, na wanaoamua kuhama wawe na fursa ya kufanya hivyo kwa heshima,” amesema Daniels.
IOM inaendesha miradi ya uhamaji wa tabianchi katika zaidi ya nchi 80, ikizipa jamii za wenyeji nafasi ya kuongoza katika kutafuta suluhu zinazolingana na hali zao halisi. Daniels anatumai kwamba COP30 itakuwa “hatua ya mabadiliko” katika kutambua uhamaji wa watu kama eneo kuu la hatua za tabianchi, hususan katika mipango ya kitaifa ya urekebishaji na ufadhili wa kushughulikia hasara na uharibifu unaotokana na majanga.
“Sekunde kumi zilizobadilisha maisha yangu milele”
Kwa Robert Montinard kutoka Haiti, mjadala huu ni wa kibinafsi. Tetemeko la ardhi la mwaka 2010 lililoitikisa nchi yake lilidumu sekunde kumi pekee lakini liliharibu maisha ya vizazi. Akisaka usalama na maisha mapya, Robert alikimbilia Brazil kama mkimbizi, na sasa anaongoza Chama cha Mawon, kinachosaidia wakimbizi na wahamiaji kuanza upya maisha yao.
Katika COP30, Robert anasisitiza umuhimu wa sauti za wakimbizi kusikika.
“Tunataka kuwa sehemu ya suluhisho. Tunataka wahamiaji na wakimbizi wasikike. Wale wanaoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi wakimbizi, watu wa asili, jamii za weusi, wanawake wana suluhisho. Tunaleta mapendekezo yanayogeuza maumivu ya watu kuwa hatua,” amesema.
Wiki hii, Robert amekabidhi waraka wa mapendekezo kwa Mke wa Rais wa Brazil, Rosângela Janja da Silva, na Waziri wa Mazingira, Marina Silva. Waraka huo unataka kuanzishwa kwa mabaraza ya tabianchi katika ngazi za manispaa, kupambana na ubaguzi wa mazingira, na kuunda vikundi vya jamii kukabiliana na majanga ya asili.
Anasema hali ya Haiti ni mfano wa “ukosefu wa haki wa tabianchi.” Kimbunga kinachopiga Florida, anasema, huleta uharibifu mkubwa nchini kwake pia lakini wakati Marekani hujenga upya haraka, majengo yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi la 2010 nchini Haiti bado yapo katika kifusi.
Janga la tabianchina migogoro ya ardhi nchini Ethiopia
Kutoka Ethiopia, Makebib Tadesse anaona mabadiliko ya tabianchi yakichochea migogoro ya ardhi na rasilimali. Anasema nchi hiyo inakabiliwa na “mzunguko unaoendelea wa vurugu na kuhama,” unaoongezeka kadri uhaba wa chakula na maji unavyoongezeka.
Kaskazini mwa Ethiopia, ambako alizaliwa, Tadesse anasema athari za mabadiliko ya tabianchi sasa zinakaribia au hata kuzidi uharibifu ulioletwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1974 hadi 1991.
“Mabadiliko ya tabianchi yanawasukuma watu kuondoka Ethiopia kwa njia ambazo hatujawahi kuona kabla,” amesema.
Robert na Makebib ni sehemu ya ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) katika COP30, pamoja na kiongozi wa kiasili kutoka Venezuela, Gardenia Warao.
“Ukarimu wa Brazil unapaswa kupongezwa”
Alfonso Herrera, mwigizaji kutoka Mexico na Balozi Mwema wa UNHCR kwa Amerika ya Kusini, anatoa sauti kwa ujumbe huo wa wakimbizi.
“Sauti za wakimbizi zimekuwa zikinyoamazishwa lakini sasa lazima zisikike,” amesema Herrera katika mahojiano na UN News.
Amesafiri katika nchi kadhaa za ukanda huo kutoka Mexico hadi Venezuela, Honduras na El Salvador akishuhudia athari za kibinadamu za uhamaji wa tabianchi na juhudi za Umoja wa Mataifa kuwarejeshea matumaini wahamiaji kupitia elimu na msaada wa kisheria.
Amesema Brazil inastahili pongezi kwa sera zake za uwazi na ukarimu katika kuwapokea wakimbizi, hasa “wakati ambapo mataifa mengine mengi yanachukua msimamo wa kinyume kabisa.”
Wakati COP30 ikiendelea kujadili njia za kukabiliana na sayari inayobadilika, watu waliokoseshwa makazi wanaukumbusha ulimwengu kwamba hatua za tabianchi si tu kuhusu kulinda mazingira bali pia kuhusu kulinda maisha, kuhifadhi utu wa binadamu, na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma wakati bahari inapopanda.