Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo mpya na zana shirikishi kuimarisha usimamizi wa kukabiliana na hatari za joto kali duniani

Watoto nchini Thailand wanastahimili joto kali sana na ukame
© UNICEF/Sukhum Preechapanich
Watoto nchini Thailand wanastahimili joto kali sana na ukame

Mfumo mpya na zana shirikishi kuimarisha usimamizi wa kukabiliana na hatari za joto kali duniani

Tabianchi na mazingira

Wakati dunia ikishuhudia ongezeko kubwa la viwango vya joto, mashirika ya kimataifa yamezindua Mfumo na Zana ya Usimamizi wa kukabiliana Hatari za Joto Kaliduniani leo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP30, huko mjini Belém, nchini Brazil.

Hatua hii inalenga kusaidia nchi wanachama kuboresha uratibu, mipango na uwekezaji katika kukabiliana na joto kali linaloongezeka duniani.

Joto kali: tishio kubwa kwa afya, uchumi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani WMO, limeonya kuwa joto kali limekuwa moja ya vitisho vikubwa vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi, likisababisha zaidi ya mamilioni ya vifo duniani kote kila mwaka na upotevu wa takribani saa bilioni 639 za kazi mwaka 2024 pekee sawa na hasara ya kiasi cha dola trilioni 1 za Kimarekani au asilimia 1 ya pato la dunia.

Aidha, WMO imesema miji imeripoti kupanda kwa joto mara mbili ya wastani wa dunia, hali inayosababisha misukosuko kwenye sekta za nishati, usafiri na kilimo, huku upotevu wa mazao ukiwaweka mamilioni ya watu katika hatari ya njaa.

Zaidi ya hayo, Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, amesema kuwa mwaka 2025 unatarajiwa kuwa miongoni mwa miaka mitatu yenye joto zaidi katika historia.

Tunaona ongezeko la matukio ya joto hatari, na viwango vya zaidi ya nyuzi joto 40°C hadi 50°C si jambo la nadra tena,” amesema.

Joto kali linaathiri mamilioni ya watu kote ulimwenguni.
© Unsplash/Nathan Hurst
Joto kali linaathiri mamilioni ya watu kote ulimwenguni.

Ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya hatua za haraka

Kwa kuzingatia changamoto hizo, mfumo huu umetayarishwa kwa ushirikiano kati ya WMO, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), Mtandao wa Kimataifa wa Afya na Joto (GHHIN) na Chuo Kikuu cha Duke. Uandaliwaji huu unajibu Wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Hatari za Joto Kali.

Pia zana hii inatoa mbinu za vitendo na ushahidi wa kisayansi kusaidia serikali na taasisi kutathmini sababu kuu za hatari ya joto, kubaini mapungufu katika mifumo ya usimamizi, na kupanga hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu ili kulinda maisha na uchumi.

Kukabiliana na joto kali si hiari tena”

Akizungumzia umuhimu wa hatua hii, Mkuu wa UNDRR, Kamal Kishore, amesisitiza kwamba:

Ushirikiano mpana uliotumika kuandaa mfumo huu unaonesha ukweli muhimu — usimamizi wa joto kali unaohusisha sekta na ngazi zote si chaguo tena, bali ni sharti la kuendelea kuishi.”

Vilevile, hafla ya uzinduzi ilifanyika katika tukio la ngazi ya juu lenye kaulimbiu Usimamizi wa Hatari za Joto Kali: Mfumo Mpya na Zana kwa Ajili ya Hatua za Haraka, lililofanyika pembeni ya mkutano wa COP30. Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi wa kimataifa, wawakilishi wa serikali, taasisi za fedha na mashirika kama Rockefeller Foundation, EBRD, na CREWS Initiative.

Afya na tabianchi vyatambuliwa kama nguzo shirikishi

Zana hii pia imeangaziwa wakati wa Siku ya Afya ya mkutano huo wa COP30 leo tarehe 13 mwezi Novemba, ambapo Mpango wa Utekelezaji wa Afya wa Belém umepitishwa.

Mpango huo unatambua uhusiano wa karibu kati ya afya na mabadiliko ya tabianchi na unatoa wito wa kuimarisha utafiti, tathmini za athari, ufuatiliaji wa hatari na mifumo ya tahadhari za mapema.

Hii inadhihirisha kwamba usimamizi wa joto kali unapaswa kuzingatiwa kama suala la afya ya umma, si la mazingira pekee.

Nchi tatu kuanza majaribio ya mfumo huo mwaka 2026

Kwa kuangalia mbele, mwaka 2026 mfumo huu utaanza kutekelezwa kwa majaribio katika nchi za Barbados, Senegal, na Cambodia, kwa ufadhili wa mpango wa CREWS ambao ni Mfumo wa Hatari za Mabadiliko ya Tabianchi na Tahadhari za Mapema

Majaribio haya yatahusisha uratibu wa sekta mbalimbali, maandalizi ya fedha na hatua za tahadhari za mapema ili kuimarisha uhimilivu wa jamii dhidi ya joto kali. Hatua hii inalenga kuonesha jinsi zana hii inaweza kutumika kwa vitendo katika mazingira tofauti ya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Joy Shumake-Guillemot, mwenyekiti mwenza wa Mtandao wa Kimataifa wa Afya na Joto (GHHIN):

Mfumo huu unarahisisha mabadiliko kutoka katika juhudi zilizotawanyika hadi mifumo ya pamoja inayookoa maisha na kujenga uthabiti.”