Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la uraibu wa nikotini hasa miongoni mwa vijana kujadiliwa

WHO inahimiza hatua za haraka kupiga marufuku tumbaku yenye ladha na bidhaa za nikotini
© Unsplash/Zaya Odeesho
WHO inahimiza hatua za haraka kupiga marufuku tumbaku yenye ladha na bidhaa za nikotini

Ongezeko la uraibu wa nikotini hasa miongoni mwa vijana kujadiliwa

Afya

Zaidi ya wajumbe 1,400 kutoka serikali mbalimbali, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia wanatarajiwa kushiriki katika mikutano muhimu itakayojadili ongezeko la uraibu wa nikotini hususani miongoni mwa vijana, pamoja na tishio la biashara haramu ya bidhaa za tumbaku.

Tarehe 17 mpaka 21 Novemba 2025 huko Geneva Uswisi kutafanyika mkutano wa Nchi Wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO FCTC, ukifuatiwa na Mkutano wa Nchi Wanachama wa Itifaki (MOP4) tarehe 24 hadi 26 Novemba.

Mikutano hiyo, inayofanyika chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku (WHO FCTC) na Itifaki ya Kutokomeza Biashara Haramu ya Bidhaa za Tumbaku, inalenga kuimarisha utekelezaji wa mikataba hiyo miwili ya afya ya umma iliyoanzishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Kaimu Mkuu wa Sekretarieti ya WHO FCTC Andrew Black amesema “Mikutano hii ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza dhamira ya kisiasa katika kupambana na janga la tumbaku duniani, linalosababisha vifo zaidi ya milioni saba kila mwaka.”

Sigara za kielektroniki

Siku ya ufunguzi itajumuisha kikao cha mawaziri kuhusu hatua za kulinda watoto dhidi ya athari za sigara za kielektroniki (e-cigarettes) na bidhaa nyingine za nikotini, kikihudhuriwa na viongozi wa afya kutoka Ulaya na Amerika Kusini.

Aidha, mkutano utaadhimisha miaka 20 tangu kuanza kutumika kwa WHO FCTC. Tukio hilo litawakutanisha maafisa wa serikali, Umoja wa Mataifa, wanaharakati wa vijana na mashirika ya kiraia chini ya kaulimbiu “Kujumuisha Vizazi kwa Dunia Isiyo na Tumbaku.”

Wakati huo huo, wajumbe watajadili ripoti ya maendeleo ya utekelezaji wa mkataba wa mwaka 2025, hatua za kupunguza matumizi ya tumbaku, uraibu wa nikotini na athari za moshi wa tumbaku, pamoja na athari za bidhaa za tumbaku kwa mazingira.

Biashara haramu ya tumbaku

Baada ya mkutano huo, nchi 71 wanachama wa Itifaki zitakutana kujadili mbinu za kuzuia biashara haramu ya tumbaku, ambayo inakadiriwa kuchangia asilimia 11 ya soko la tumbaku duniani na kupoteza zaidi ya dola bilioni 47 za mapato ya kodi kila mwaka.

“Biashara haramu ya tumbaku inahatarisha afya ya umma na inachochea uhalifu wa kimataifa. Ni tatizo la dunia linalohitaji suluhisho la dunia,” imesema taarifa ya WHO-FCTC.

Mikataba hii inatoa mfumo wa kisheria wa kudhibiti tumbaku kupitia sheria za maeneo yasiyoruhusiwa kuvuta sigara, onyo la picha kubwa kwenye vifurushi, na kodi za juu kwa bidhaa za tumbaku — hatua ambazo tayari zimeokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani.