Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lamchagua Phoebe Okowa wa Kenya kuwa jaji wa ICJ

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ
© ICJ/Frank van Beek
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ

Baraza la Usalama lamchagua Phoebe Okowa wa Kenya kuwa jaji wa ICJ

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatano limemchagua Phoebe Okowa kutoka Kenya kuwa Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), baada ya duruu nne za upigaji kura.

Upigaji kura huo ulifanyika kwa wakati mmoja na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lakini kwa utaratibu tofauti, kama inavyotakiwa na Katiba ya Mahakama hiyo ya Haki.

Bi. Okowa amechaguliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Abdulqawi Ahmed Yusuf wa Somalia, ambaye hivi karibuni alitangaza kujiuzulu.

Kazi yake imeaanza rasmi leo, jana 12 Novemba 2025, na itadumu hadi tarehe 5 Februari 2027.

Wagombea wenye sifa kuu

Jumla ya wagombea wanne waliteuliwa rasmi na makundi yao ya kitaifa kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo, wakiwemo:

  • Taoheed Olufemi Elias  kutoka Nigeria, aliyeteuliwa na Bahrain, Italia, Latvia, Jordan, Malta, Nigeria na Ufilipino;
  • Charles Chernor Jalloh  kutoka Sierra Leone, aliyeungwa mkono na Afrika Kusini, Burkina Faso, Canada, Ecuador, Liechtenstein, Sierra Leone na Jamhuri ya Czech;
  • Paul Kuruk  kutoka Ghana, aliyeteuliwa na Ghana na
  • Phoebe Okowa kutoka Kenya, aliyeungwa mkono na Afrika Kusini, Colombia, Kenya, Namibia, Uholanzi, Romania, Uswisi na Vanuatu.

Duru nyingi za upigaji kura

Katika duru ya kwanza hakuna mgombea aliyeweza kupata kura za kutosha kufikia wingi wa kura nane unaohitajika katika Baraza la Usalama.

Matokeo yalikuwa: Bi. Okowa alipata kura 6, Bw. Jalloh alipata kura 5, Bw. Elias alipata kura 3 na Bw. Kuruk alipata kura 1.
Baada ya Bw. Kuruk kujiondoa, duru ya pili ilihusisha wagombea watatu pekee ambapo Bw. Jalloh alipata kura 8, Bi. Okowa kura 6 na Bw. Elias kura 1.

Ingawa Baraza la Usalama lilimpa Bw. Jalloh kura nyingi, Baraza Kuu lilimpa Bi. Okowa kura za juu zaidi, jambo lililosababisha kufanyika kwa duru ya tatu. Hatimaye, katika duru ya nne, vyombo vyote viwili vilimchagua Bi. Okowa kwa wingi wa kura ambapo alipata kura 8 katika Baraza la Usalama na kura 106 katika Baraza Kuu, dhidi ya Bw. Jalloh aliyepata kura 7 Baraza la Usalama na 79, kwenye Baraza Kuu

Utaratibu wa uchaguzi

Kwa mujibu wa Katiba ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, mgombea anachukuliwa kuwa amechaguliwa endapo atapata wingi wa kura katika Baraza la Usalama na Baraza Kuu.

Katika Baraza la Usalama, wingi huo ni kura nane, bila kujali wanachama wa kudumu au wa muda.

Katika Baraza Kuu, ambapo nchi zote 193 wanachama hupiga kura, idadi ya chini ya kura zinazohitajika ni 97.

Kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ

Mahakama ya Kimataifa ya Haki, yenye makao yake jijini The Hague, Uholanzi, ni chombo kikuu cha kimahakama cha Umoja wa Mataifa. Mahakama hiyo inaundwa na majaji 15, na jukumu lake ni kusuluhisha migogoro ya kisheria kati ya nchi wanachama pamoja na kutoa maoni ya kisheria kwa masuala yanayoletwa na vyombo vya Umoja wa Mataifa au mashirika maalum.

Tofauti na taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa, majaji wa ICJ ni huru, si wawakilishi wa serikali zao.

Aidha, Mahakama haiwezi kuwa na majaji wawili kutoka nchi moja, na lazima iakisishe uwakilishi wa mifumo mikuu ya kisheria na tamaduni za dunia.

Wajumbe waliopo wa mahakama

Baada ya kuchaguliwa kwa Bi. Okowa, wajumbe wa sasa wa Mahakama ni,
Iwasawa Yuji (Japani), Rais; Julia Sebutinde (Uganda), Makamu wa Rais Ronny Abraham (Ufaransa), Bogdan-Lucian Aurescu (Romania), Dalveer Bhandari (India), Leonardo Nemer Caldeira Brant (Brazil), Hilary Charlesworth (Australia), Sarah Hull Cleveland (Marekani), Juan Manuel Gómez Robledo (Mexico), Mahmoud Daifallah Hmoud (Jordan), Georg Nolte (Ujerumani), Phoebe Okowa (Kenya), Dire Tladi (Afrika Kusini), Peter Tomka (Slovakia) na Xue Hanqin (China).