Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafanikio ya kimataifa katika kudhibiti TB yapo hatarini kutokana na ukata: WHO

Daktari akihudumia mgonjwa hospitalini anayeugua kifua kikuu huko Mumbai, India.
© WHO/David Rochkind
Daktari akihudumia mgonjwa hospitalini anayeugua kifua kikuu huko Mumbai, India.

Mafanikio ya kimataifa katika kudhibiti TB yapo hatarini kutokana na ukata: WHO

Afya

Kifua kikuu au TB bado ni moja ya magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza duniani, kikiua zaidi ya watu milioni 1.2 na kuwaathiri takribani watu milioni 10.7 mwaka uliopita, kwa mujibu wa  ripoti mpya ya kimataifa ya kifua kikuu 2025 iliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO).

Kwa mujibu wa ripoti licha ya maendeleo yanayoonekana katika utambuzi, matibabu, na ubunifu, changamoto za kudumu katika suala la ufadhili na upatikanaji sawa wa huduma za afya vinatishia kufuta mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu katika mapambano ya dunia dhidi ya TB.

Kupungua kwa mzigo wa kifua kikuu duniani, pamoja na maendeleo katika upimaji, matibabu, ulinzi wa kijamii, na utafiti ni habari njema baada ya miaka ya changamoto, lakini mafanikio haya bado si ushindi, kutokana na ukweli kwamba kifua kikuu bado kinaua zaidi ya watu milioni moja kila mwaka, licha ya kuwa ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika, hili ni jambo lisilokubalika. WHO inashirikiana na nchi mbalimbali kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuharakisha safari ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.”  amesema  Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO

Maendeleo ya kimataifa na hadithi za mafanikio

Kati ya mwaka 2023 na 2024, ripoti imesema maambukizi ya kifua kikuu  duniani yalipungua kwa karibu asilimia 2, huku vifo vikishuka kwa asilimia 3, ishara ya kuimarika kwa huduma za afya baada ya janga la coronavirus">COVID-19.

Kanda ya Afrika ya WHO ripoti inasema ilipunguza maambukizi kwa asilimia 28  na vifo kwa asilimia 46, huku Kanda ya Ulaya ikipunguza maambukizi kwa asilimia 39 na vifo kwa asilimia 49 kati ya mwaka 2015 na 2024.

Ripoti hiyo imeongeza kwamba zaidi ya nchi 100  zilipunguza maambukizi kwa angalau asilimia 20 na nchi 65 zikapunguza vifo kwa 35 au zaidi, zikifikia malengo ya awali ya mkakati wa “Kutokomeza TB.”

Hata hivyo, asilimia asilimia 87 ya wagonjwa wapya wa TB mwaka 2024 inasema ripoti walitoka katika  nchi 30, ambapo nchi nane ikiwemo India, Indonesia, China, Pakistan, Nigeria, Congo DRC, Ufilipino na Bangladesh ambazo zilichangia asilimia 67 ya maambukizi yote duniani.

Maendeleo makubwa katika utambuzi na matibabu ya TB

Matibabu ya kifua kikuu kwa wakati yameokoa takribani maisha ya watu milioni 83  tangu mwaka 2000. Kati ya mwaka 2023 na 2024, maendeleo yaliendelea kuongezeka katika utambuzi, kinga na matibabu ya TB, yakionesha athari chanya za jitihada endelevu na ubunifu katika nchi mbalimbali.

Mafanikio muhimu ni pamoja na:

·        Mwaka 2024, watu milioni 8.3 waligunduliwa na TB na kuanza matibabu  sawa na asilimia 78 ya watu wote waliougua ugonjwa huo mwaka huo.

·        Matumizi ya vipimo vya haraka vya TB yaliongezeka kutoka asilimia 48 mwaka 2023  hadi asilimia 54 mwaka 2024.

·        Matibabu ya TB isiyo na usugu yalibaki yenye mafanikio makubwa, kwa asilimia 88 ya wagonjwa kupona.

·        Idadi ya watu wanaopata TB sugu kwa dawa ilipungua, huku zaidi ya  watu 164,000 wakipokea matibabu mwaka 2024. Kiwango cha mafanikio ya matibabu kiliongezeka hadi asilimia 71, kutoka asilimia 68 mwaka uliopita.

·        Watu milioni 5.3 walio katika hatari kubwa ya TB walipokea tiba ya kinga mwaka 2024, ikilinganishwa na watu  milioni 4.7 mwaka 2023.

Ulinzi wa kijamii na ushirikiano wa sekta mbalimbali

Kwa mara ya kwanza, WHO imetoa taarifa kuhusu maendeleo kuelekea lengo la ulinzi wa kijamii lililowekwa katika mkutano wa pili wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu TB mwaka 2023, kwa kutumia takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa  la kazi Duniani (ILO).

Miongoni mwa nchi 30 zenye mzigo mkubwa wa TB, ripoti imesema kiwango cha ulinzi wa kijamii bado hakilingani  kuanzia asilimia 3.1 nchini Uganda hadi asilimia 94 nchini Mongolia. Nchi 19 kati ya hizo zinaripoti kiwango cha chini ya asilimia 50.

Ripoti pia inasisitiza umuhimu wa kushughulikia sababu kuu za hatari zinazochochea maambukizi ya TB, kama vile utapiamlo, maambukizi ya VVU, kisukari, uvutaji sigara, na matumizi ya pombe.

Kukabiliana na vichocheo hivi pamoja na sababu za kimuundo kama umasikini, kunahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali imesisitiza ripoti.

Pengo la ufadhili linatishia maendeleo na utafiti

Licha ya mafanikio yaliyopatikana, dunia bado iko mbali na kufikia malengo ya mkakati wa kutokomeza Kifua Kikuu (TB)  kutokana na upungufu mkubwa wa ufadhili imesema ripoti.

Mwaka 2024, zilitolewa dola bilioni 5.9 pekee kwa ajili ya kinga, uchunguzi na matibabu, chini ya robo ya lengo la kila mwaka la dola bilioni 22 kufikia mwaka 2027.

Kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kuanzia mwaka 2025 kwa mujibu wa ripoti kunatishia kusababisha hadi vifo vya watu milioni 2 na maambukizi mapya milioni 10 ifikapo 2035. Aidha, utafiti wa TB unakabiliwa na upungufu wa fedha, kwani mwaka 2023 ulipokea dola bilioni 1.2 pekee  ambayo ni asilimia 24 tu ya lengo.

Hata hivyo, WHO inaendelea kuongoza juhudi za kimataifa za kukuza utafiti na chanjo mpya kupitia Baraza la Kuendeleza Chanjo ya TB, huku vipimo 63, dawa 29 na chanjo 18 zikiwa katika hatua mbalimbali za maendeleo.

Wito wa WHO

Tuko katika kipindi cha maamuzi muhimu katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, kupunguzwa kwa ufadhili na kuendelea kwa sababu za hatari za ugonjwa huu kunatishia kusambaratishamafanikio tuliyoyapata kwa bidii. Lakini kwa utashi wa kisiasa, uwekezaji endelevu, na mshikamano wa kimataifa, tunaweza kubadilisha hali hii na kumtokomeza muuaji  wa kale milele na mara moja,”  amesema Dkt. Tereza Kasaeva, Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya VVU, TB, Homa ya ini na Magonjwa ya Zinaa (STIs).

WHO inatoa wito kwa serikali na washirika kuongeza utashi wa kisiasa, uwekezaji wa ndani, na kuimarisha utafiti ili kuharakisha maendeleo katika kutokomeza kifua kikuu duniani.