Maisha ni ngumu, uharibifu ni mkubwa baada ya kimbunga Melissa - Waathirika Jamaica
Maisha ni ngumu, uharibifu ni mkubwa baada ya kimbunga Melissa - Waathirika Jamaica
Wiki ya pili baada ya Kimbunga Melissa kupiga magharibi mwa Jamaica, mitaa ya Savanna-la-Mar na Watercress bado ipo kimya, kimya cha mji unaojaribu kujikwamua na Athari zilizoachwa na zahma hiyo. Nyumba zimebomoka, shule zimeharibiwa, maisha yamepinduliwa. Makadirio yanaonesha kuwa watu milioni 1.6 wameathirika, na sasa timu za misaada zinafanya kazi kwa haraka usiku na mchana kutoa msaada muhimu wa chakula, makazi, na usalama.
Trevolyn mlinzi wa shule katika eneo la Savanna -la-Mar. Shule ya Msingi ya Sir Clifford Campbell anakofanya kazi ina ukuta ulioanguka na vyumba vya madarasa vimejaa vioo na fanicha zilizovunjika. Kwa Trevolyn na jamii yake, uharibifu huu unamgusa kila mtu, kwani anasema "Oh, ni uharibifu mkubwa. Ni ngumu. Kwa kweli, ni ngumu sana. Watu bado wako kwenye makazi ya muda. Hawajarudi nyumbani kwa sababu jengo lote limebomoka."
Kinachoendelea sasa baada ya uharibifu Mkubwa wa kimbunga Melissa ni kusafisha Charmaine ameungana na wakazi wengine katika eneo hili kusafisha mabaki ya uharibifu huo lakini anasema maisha yao sasa ni mtihani mgumu.
"Chakula ndiyo kipaumbele cha wengi. Lakini kutoka wapi? Kwa sababu baadhi ya watu bado hawana mahali pa kulala."
Hali ni mbaya barabarani kinachoonekna ni ajengo yaliyoporomoka na vifusi vilivyorukikana Paa za nyumba zimeezuliwa , nyumba zimeharibiwa, na watu wanatembea katika mitaani ambayo sasa inaonekana kama eneo la vita. Timu za misaada zikiwemo za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA zinafanya kazi bila kuchoka kutathmini uharibifu. Rogerio Mobilia ni afisa wa operesheni za OCHA katika eneo la Black River ambalo limeathirika vibaya
"Nyuma yangu, unaweza kuona hata majengo makubwa, ukuta wenye nguvu haukuweza kustahimili nguvu ya kimbunga kama hicho. Mji mzima nyuma yangu wa Black River umegeuka kama eneo la vita. Watu wanatembea wakijaribu kutambua makazi yao. Wanajaribu kuona wapi waende. Nini cha kufanya na maisha yao. Ni muhimu kwamba serikali za dunia zizingatie hali mbaya ya hewa na zichukue tahadhari."
Kiwango cha uharibifu ni kikubwa. Kuna zaidi ya tani milioni 4.8 za mabaki na vifusi , takriban malori 480,000 yanahitaji kuondolewa kutoka barabarani na maeneo ya umma. Lakini Katikati ya mabaki haya, hadithi za uhai na machungu zinaibuka. Kemeisha mkazi wa Watercress amepoteza kila kitu kwenye kimbunga hicho kama walivyo wakaazi wengine wengi anasema
"Hili ndio ilikuwa nyumba yetu. Kama unavyoona, hapa kuna nyumba takriban 30 hadi 40. Kila mtu amebakia bila sehemu ya kuishi."
Na hali ni Dhahiri shairi Kemeisha anaongeza kuwa "Uzoefu huu si wa kawaida, kwa sababu nimepitia Kimbunga Gilbert. Na hiki hakilingani na Gilbert. Kwa sababu nilikuwa ndani ya jengo lamatofali, na niliweza kusikia kila kitu kikitetemeka, madirisha, bati, kila kitu kikipasuka. Kila kitu nyumbani kwangu kimeharibiwa. Kitanda, sijui kiko wapi, kabati, sina cha kuona. Mwanangu hana nguo ya kuvaa. Nalazimika kutembea kuomba kitu cha kuvaa. Hivyo tunahitaji msaada."
Kimbunga Melissa kimeacha alama kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Jamaica. Familia zimepoteza makazi, watoto hawana mahitaji ya msingi, na jamii zinatafran bila kujua mustakbali wao. Lakini katikati ya uharibifu, matumaini ya Wajamaica yanaangaza. Timu za msaada zinaendelea na kazi yao, wahudumu wa kjitolea hawakati tamaa, na majirani wanashirikiana kwani kila hatua ndogo ni hatua kuelekea kujikwamua
Na kadri siku zinavyosonga, kila msaada, kila michango, kila kitendo cha mshikamano kina maana kwa waathirika hawa. Kwa sababu baada ya kimbunga, kazi halisi inaanza, kujenga upya maisha, nyumba, na jamii, hatua kwa hatua.