Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujenga mnepo: Jinsi jamii moja nchini Brazil inavyokabiliana na ongezeko la mawimbi ya bahari

Kuongezeka kwa kina cha bahari na uharibifu wa pwani kumebadilisha maisha ya Marajó, na kusomba nyumba na njia za kujikimu kando ya ufuo.
© IOM/Filipe Bispo
Kuongezeka kwa kina cha bahari na uharibifu wa pwani kumebadilisha maisha ya Marajó, na kusomba nyumba na njia za kujikimu kando ya ufuo.

Kujenga mnepo: Jinsi jamii moja nchini Brazil inavyokabiliana na ongezeko la mawimbi ya bahari

Tabianchi na mazingira

Kwa zaidi ya miaka 40, Ivanil ameishi katika nyumba iliyoinuliwa kwa nguzo, umbali wa mita 20 tu kutoka kando ya maji, katika jamii ile ile aliyo zaliwa, kwenye Kisiwa cha Marajó ambako mto Amazon unakutana na Bahari ya Atlantiki kaskazini mwa Brazil.

Kutoka hapo, yeye na mumewe walikuwa wakienda uvuvi, kulima mashamba, na kulea wanyama. “Nilikuwa mtu wa furaha sana kwenye kipande kidogo cha ardhi hiyo ilikuwa paradiso yangu,” anasema.

Kisha ikaja usiku uliobadilisha kila kitu maishani mwake. Mvua ilifika na radi na umeme uliochomoza gizani, ukitetemesha nyumba ndogo zilizo kando ya pwani.

Ivanil alilazimika kuhama kwa sababu ya kuongezeka kwa mawimbi na uharibifu wa pwani
© IOM/Filipe Bispo
Ivanil alilazimika kuhama kwa sababu ya kuongezeka kwa mawimbi na uharibifu wa pwani

Kwenye Vila do Pesqueiro, jamii ndogo ya kitamaduni inayokabiliana na kuongezeka kwa mawimbi na mmomonyoko wa ardhi wa pwani, familia zilikusanyika pamoja katikati ya dhoruba ambayo ingebadilisha maisha yao.

Karibu miaka miwili baadaye, kumbukumbu bado ipo wazi kwa Ivanil, kila sauti, kila mwangaza wa umeme, ni kielelezo cha jinsi bahari ilivyokuwa imekaribia.

Wakati mawimbi yalipopita katika jamii hiyo Februari 2024, yalisomba pamoja na ardhi waliyokuwa wakiita nyumbani kwa vizazi na vizazi.

Ivanil na majirani zake hawakuwa na chaguo isipokuwa kuacha nyumba zao na kujenga maisha yao kwenye ardhi iliyo kando kidogo. Umbali ulikuwa mfupi, chini ya kilomita moja, lakini mabadiliko waliyahisi makubwa.

“Hata tukihama umbali mfupi, unahisi kama dunia tofauti kabisa,” Ivanil ameeleza. “Hili ni eneo la mikoko, joto zaidi, kelele zaidi, na hakuna sehemu ambapo tunaweza kulea wanyama au kulima.”

Vila do Pesqueiro ina makazi ya familia takriban 160 ndani ya Hifadhi ya Baharini ya Soure, eneo lilnaolindwa.

Iko kando ya mdomo wa mto Amazon kutoka Belem, ambapo jamii ya kimataifa kwa sasa inakutana kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Tabianchi, unaojulikana kama COP30.
Uhamisho wa watu kutokana na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi ni moja ya masuala muhimu yanayojadiliwa.

Jhonny, mwana wa Ivanil, anapekua vifusi vya nyumba zilizoharibiwa.
© IOM/Filipe Bispo
Jhonny, mwana wa Ivanil, anapekua vifusi vya nyumba zilizoharibiwa.

Hifadhi kama Soure Marine zimeundwa kulinda maisha na utamaduni wa jamii za asili huku zikikuza matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Uvuvi bado ni chanzo kikuu cha kipato cha jamii hizo, huku upishi wa kienyeji na utalii mdogo ukisaidia familia kudumisha maisha yao.

Maisha hatari

Lakini kadri mawimbi yanavyoongezeka, maisha na makazi yanakuwa hatarini zaidi.
Kwa wengi katika kijiji hicho, mabadiliko yamekuwa jambo binafsi sana. Kando na Ivanil anaishi mwanawe, Jhonny ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu aliyekuwa amepita mtihani wake wa kujiunga na shahada ya biyolojia wakati mawimbi yalipovuma.

Alikua akiangalia bahari ikibadilika mwaka baada ya mwaka, mawimbi makali na mmomonyoko wa haraka wa ardhi ukibadilisha pwani aliyokuwa anaijua.
Jhonny anakumbuka jinsi kila kitu kilivyobadilika haraka. Kila msimu, maji yalikaribia kidogo kidogo hadi siku moja yalifikia nyumba zao. “Sehemu tulikokuwa na nyumba sasa iko chini ya maji,” anasema.

Mara nyingi anafikiria kuhusu familia bado wanaoishi kando ya maji, akijua kuwa mawimbi makali yanatarajiwa mwaka ujao. “Kwangu mimi, kuhama siyo tu kuhusu usalama,” anasema. “Ni kuhusu kulinda mahali na watu ambao wameniumba mimi na maisha yangu.”