Hatua ndizo zinazohitajika baada ya mkutano wa dunia wa Maendeleo ya Kijamii: Diana Pasha
Hatua ndizo zinazohitajika baada ya mkutano wa dunia wa Maendeleo ya Kijamii: Diana Pasha
Mkutano wa Pili wa Dunia wa Maendeleo ya Kijamii umefunga pazia mjini Doha, Qatar, mwishoni mwa wiki hii, ukiwaleta pamoja viongozi wa dunia, mashirika ya kiraia na vijana wakitoka na wito wa pamoja dhidi ya umasikini, ukosefu wa usawa na kutengwa kijamii. Kutoka Kenya, mwanaharakati kijana amesema mkutano huo umekuwa wa kuhamasisha akitoa wito wa hatua za haraka.
Kwa muda wa wiki moja, wajumbe walibadilishana mawazo na kushirikiana suluhu za kujenga jamii zenye usawa zaidi. Mmoja wao ni kijana Diana Pasha, mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa wakfu wa Empower Her Life nchini Kenya. Shirika lake linafanya kazi na wanawake na wasichana walio hatarini kwa kuwapa elimu, ujuzi wa kidijitali na fursa za kiuchumi.
"Tunawawezesha wanawake na wasichana walio hatarini Kenya kupitia elimu, uwezeshaji kiuchumi, ujumuishaji wa kidijitali na utetezi wa haki zao za binadamu."
Pasha anasema kushiriki kwenye mkutano huo kumemsaidia kuona kwamba mabadiliko ya kudumu yanahitaji zaidi ya mazungumzo tu ya kuketi ukumbini
"Na ninachotoka nacho kwenye mkutano huu ni kwamba tunapaswa kuendelea na mazungumzo, lakini jambo muhimu zaidi ni utekelezaji, jinsi tunavyochukua hatua."
Wajumbe walijadili mada muhimu ikiwemo kutokomeza umasikini, kutoa ajira bora zenye staha na kuimarisha ujumuishaji wa kijamii. Pasha anasema ana hamu ya kurudisha kile alichojifunza nyumbani Kenya na kuhamasisha wengine katika jamii yake kuchukua hatua.
"Hatuwezi kutokomeza umasikini mara moja, lakini tunapochukua hatua hizi, tunapaswa kurudi katika nchi zetu na kutekeleza kile tulichojifunza."
Mkutano wa Doha umefungwa kwa wito wa pamoja kutoka kwa serikali na mashirika ya kiraia kuhakikisha maendeleo yanayomlenga mwanadamu na pia hakuna mtu anayeachwa nyuma. Kwa wadau kama Pasha, hatua inayofuata sasa ni kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa kwa vitendo.