Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women: Vita nchini Sudan vimegeuka kuwa vita dhidi ya wanawake

Mwanamke na watoto wanahudhuria kliniki ya muda huko Tawila kwa watu ambao wamekimbia migogoro huko Darfur.
© UNFPA
Mwanamke na watoto wanahudhuria kliniki ya muda huko Tawila kwa watu ambao wamekimbia migogoro huko Darfur.

UN Women: Vita nchini Sudan vimegeuka kuwa vita dhidi ya wanawake

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women) limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha ukatili na mateso yanayowakumba wanawake na wasichana nchini Sudan, likisema kuwa vita vinavyoendelea vimegeuka kuwa “vita dhidi ya wanawake.”

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa UN Women kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Anna Mutavati, amesema kuwa kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo, kila mstari wa mapigano nchini Sudan umeathiri maisha, miili, makazi na mustakabali wa wanawake na wasichana.

“Takwimu za hivi karibuni kutoka kwenye Ripoti Maalum ya Tahadhari ya Masuala ya Kijinsia ya UN Women, yenye kichwa Mtazamo wa Kijinsia kuhusu Tatizo la Uhaba wa Chakula nchini Sudan, zimeonesha kuwa takribani wanawake na wasichana milioni 11 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula,” amesema Mutavati.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa njaa, ukosefu wa huduma za afya, ubakaji, na ukatili wa kijinsia vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wanawake hasa katika maeneo ya Darfur na Kordofan, huku njaa ikionekana kuwa “kitu kinachotabirika kwa wanawake nchini humo.”

Wanawake wanahudhuria kliniki ya utapiamlo na afya ya uzazi inayoendeshwa na UNFPA huko Tawila, Sudan.
© UNFPA
Wanawake wanahudhuria kliniki ya utapiamlo na afya ya uzazi inayoendeshwa na UNFPA huko Tawila, Sudan.

Njaa na mateso makali

Mutavati amesema hali ya baa la njaa imetangazwa rasmi katika maeneo ya El Fasher, mji mkuu wa Darfur kaskazini, magharibi mwa Sudan, na Kadugli kusini-magharibi mwa nchi hiyo kufikia mwezi Novemba mwaka huu 2025, ambapo zaidi ya asilimia 73 ya wanawake hawapati lishe yenye virutubisho muhimu.

“Tulipoongea na wanawake walioko mashinani, wengi walikiri kupitisha milo ili watoto wao wapate chakula. Wasichana balehe mara nyingi hupata sehemu ndogo zaidi ya chakula, jambo linaloathiri afya yao kwa muda mrefu,” amesema.

Katika baadhi ya maeneo yaliyotengwa, wanawake wamelazimika kukusanya majani ya porini na matunda ili kuyachemsha kwa ajili ya chakula. Wakati wakifanya hivyo, wamekuwa wakikabiliwa na hatari za kubakwa, kutekwa, au kuuawa.

Taarifa hiyo ya UN Women pia inaonesha ongezeko kubwa la utapiamlo mkali kwa watoto wachanga kutokana na njaa wanayopata mama zao. Huduma za afya zimeporomoka, huku zaidi ya asilimia 80 ya vituo vya tiba vikifungwa tangu vita kuanza.

Huduma za afya na heshima ya kibinadamu zasambaratika

Katika mji wa El Fasher, wanawake waliosalia wameelezea hali ya kutisha ya kuzalia mitaani baada ya hospitali ya mwisho ya uzazi kuvamiwa na kuharibiwa. Wengi wamekimbia makazi yao kuelekea Tawila, Korma na Malit miji iliyoko kaskazini magharibi mwa Darfur Kaskazini ambako huduma za kibinadamu ni haba.

“Wanawake wanaripoti kuwa kila hatua wanayochukua iwe ni kwenda kuteka maji, kukusanya kuni au kusimama foleni ya chakula ni hatari ya kubakwa. Kuna ushahidi unaoongezeka kuwa ubakaji unatumika kwa makusudi kama silaha ya vita. Miili ya wanawake imekuwa kama eneo la uhalifu,” amesisitiza Mutavati.

Hali ya hadhi ya binadamu pia imesambaratika. Kifurushi kimoja cha taulo za kike kinagharimu kiasi cha dola 27 za Kimarekani, huku familia inayopokea msaada wa fedha ikipokea chini ya dola 150 kwa kaya ya watu sita.

“Hali hii inawalazimu familia kuchagua kati ya chakula, dawa, au heshima. Na mara zote, mahitaji ya wanawake na wasichana ndiyo yanayowekwa mwisho,” amesema.

Mhudumu wa afya akimpima mtoto kama kuna dalili za utapiamlo huko Khartoum, Sudan. Ulimwenguni kote, migogoro na mishtuko inayohusiana na hali ya hewa inasababisha njaa inayoongezeka, na kuacha familia zikijitahidi kupata chakula, matunzo na ustawi.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih
Mhudumu wa afya akimpima mtoto kama kuna dalili za utapiamlo huko Khartoum, Sudan. Ulimwenguni kote, migogoro na mishtuko inayohusiana na hali ya hewa inasababisha njaa inayoongezeka, na kuacha familia zikijitahidi kupata chakula, matunzo na ustawi.

Mashirika ya wanawake bado yanashikilia uhai

Licha ya hali hiyo ngumu, mashirika yanayoongozwa na wanawake yameendelea kuwa nguzo muhimu ya uhai na msaada.

Huko Darfur Kaskazini, wanahamasisha uwepo wa‘majiko ya kijamii’ yanayolisha familia zisizofikiwa na msaada rasmi, huku, huko Kordofan wakifundisha akina mama jinsi ya kuandaa milo yenye virutubisho.

Hata hivyo, ni asilimia 3 pekee ya fedha za kibinadamu ndizo zinazopelekwa moja kwa moja kwa mashirika haya ya wanawake, ambayo mengi yanaendeshwa na wajitoleaji.

Wito wa UN Women kwa dunia

UN Women imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti, ikiwemo:

1. Kusitisha mara moja mapigano yote nchini Sudan na kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya usitishaji mapigano ya kibinadamu;

2. Kuhakikisha usalama wa wanawake, wasichana na raia wote, na kufungua njia salama za misaada ya kibinadamu;

3. Kutoa kipaumbele kwa wanawake na kaya zinazoongozwa na wanawake katika mgao wa chakula na urejeshaji wa maisha;

4. Kulinda wahudumu wa kibinadamu, hasa wanawake wanaofanya kazi mstari wa mbele;

5. Kutoa misaada ya moja kwa moja kwa mashirika ya wanawake, hasa yale yanayoendesha jikoni za kijamii;

6. Kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, msaada wa kisaikolojia, na huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia;

7. Na kuzingatia ushirikishwaji kamili wa wanawake katika maamuzi ya misaada na ulinzi.

Mutavati amehitimisha kwa maneno yenye kugusa moyo akisema “Wanawake na wasichana wa Sudan si takwimu  wao ndiyo kipimo cha ubinadamu wetu wa pamoja. Kila siku dunia inapochelewa kuchukua hatua, mwanamke mwingine anajifungua chini ya risasi, anazika mtoto wake kwa njaa, au anapotea bila haki.”

Kwa mujibu wa UN Women, shirika hilo linaendelea kushirikiana na washirika wa ndani, hususan mashirika yanayoongozwa na wanawake, ili kutoa msaada wa kuokoa maisha na kulinda utu wa wanawake na wasichana walioko katikati ya mgogoro mkubwa zaidi duniani kwa sasa.