Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP30 Brazil: IOM, UNHCR na UN Women na mustakabali utakiwao

Rhoda Lukaria akivuna mboga za majani, zilizolimwa kwa kutumia mbinu za kilimo bunifu kinachozingatia tabianchi, kutoka shamba la familia yao katika kaunti ya Laikipia, nchini Kenya.
UN Women/James Ochweri
Rhoda Lukaria akivuna mboga za majani, zilizolimwa kwa kutumia mbinu za kilimo bunifu kinachozingatia tabianchi, kutoka shamba la familia yao katika kaunti ya Laikipia, nchini Kenya.

COP30 Brazil: IOM, UNHCR na UN Women na mustakabali utakiwao

Tabianchi na mazingira
  • IOM yasisitiza umuhimu wa watu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi 
  • UNHCR yasema Madhara ya tabianchi yamefurusha watu 70,000 muongo uliopita
  • UN Women yataka Mpango Madhubuti wa Utekelezaji wa Usawa wa Kijinsia (GAP)

Wakati viongozi wa dunia wanakutana leo tarehe 10 Novemba 2025, huko mjini Belém, Brazil kwenye lango kuu la kuingia kwenye Msitu wa Amazon kwa ajili ya Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limeitaka jumuiya ya kimataifa kuelekeza uangalizi kwa mamilioni ya watu wanaokabiliana kila siku na changamoto halisi za mafuriko, ukame na majanga.

Ujumbe wa IOM mjini Belém ni bayana: wakati makazi na riziki za watu zinapotishiwa, wanastahili nafasi ya kubaki salama, kupona na kupanga maisha yao ya baadaye.

Kila jamii inastahili fursa ya kuzoea na kujenga mustakabali salama zaidi, lakini kwa wengi, athari hasi tayari zimekuwa kubwa mno,” amesema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM anayeshughulikia Operesheni, Bi. Ugochi Daniels, ambaye anaiwakilisha IOM katika kikao cha ngazi ya juu cha Nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC).

Na pale inapokuwa haiwezekani kubaki, watu wanapaswa kuwa na uwezo wa kuhama kwa usalama na kwa heshima. Hilo ndilo tunalolenga – kutafuta suluhisho za vitendo zinazolinda maisha na kuimarisha jamii.”

Jamii za watu wa asili zinapanda zinapanda  mbegu asilia katika Mbuga ya Kitaifa ya Chapada dos Veadeiros huko Goiás, Brazil, ili kusaidia kurejesha mfumo wa ikolojia na kuimarisha ustahimilivu wa tabianchi.
IOM/Juliana Hack
Jamii za watu wa asili zinapanda zinapanda mbegu asilia katika Mbuga ya Kitaifa ya Chapada dos Veadeiros huko Goiás, Brazil, ili kusaidia kurejesha mfumo wa ikolojia na kuimarisha ustahimilivu wa tabianchi.

Takwimu

Kwa mujibu wa takwimu za IOM, mwaka 2024 pekee majanga yalichangia kuhama kwa idadi ya watu milioni 45 ndani ya nchi zao, na kusababisha hasara ya zaidi ya kiasi cha dola bilioni 240. Nyuma ya takwimu hizi wapo wakulima waliopoteza nyumba zao kutokana na mafuriko, na watoto ambao shule zao zimebomolewa.

IOM inaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa ndani kusaidia jamii kupona, kujenga upya na kujiandaa kwa majanga yajayo.

Mkutano wa COP30, ambao mwaka huu umeandaliwa na Serikali ya Brazil, ni mkutano wa kwanza wa tabianchi kufanyika katika eneo la Amazon, na unasisitiza uongozi wa watu wa asili, jamii za wenyeji, na makundi mengine yanayoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa kuzingatia kuwa mafuriko, ukame, moto wa nyika na joto kali vinaendelea kulazimisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao kila mwaka, IOM imesisitiza kwamba maamuzi yatakayofikiwa mjini Belém lazima yalinde haki za watu na kuimarisha uwezo wao wa kuhimili na kuzoea madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Madhara ya tabianchi yamefurusha watu 70,000 muongo uliopita

Hapa ni Chad, maelfu ya wakimbizi wa Sudan wanaendelea kukimbia vita, lakini shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi linaonya kwamba mifumo ya msingi ya kuwanusuru wakimbizi tayari iko katika hali ya msukosuko.
© UNHCR/Ala Kheir
Hapa ni Chad, maelfu ya wakimbizi wa Sudan wanaendelea kukimbia vita, lakini shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi linaonya kwamba mifumo ya msingi ya kuwanusuru wakimbizi tayari iko katika hali ya msukosuko.
Mamilioni ya wakimbizi, watu waliolazimika kukimbia makwao, na jamii zinazowapokea wamekwama katika mzunguko mkali unaozidi kuongezeka wa migogoro na majanga ya tabianchi, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa leo na UNHCR, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi. Ripoti hiyo inaonya kuwa mishtuko ya hali ya hewa inaharibu fursa za kujikwamua, inaongeza mahitaji ya kibinadamu, na kuzidisha hatari za kuhama mara kwa mara.
 
Kufikia katikati ya mwaka 2025, watu milioni 117 walikuwa wamehama kutokana na vita, vurugu, na mateso. Watatu kati ya wanne kati yao wanaishi katika nchi zilizo katika hatari kubwa hadi ya juu sana ya kukumbwa na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
 
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, majanga yanayosababishwa na tabianchi yamesababisha takriban watu milioni 250 kuhama ndani ya nchi zao – sawa na takriban watu 70,000 kwa siku. Iwe ni mafuriko yanayoikumba Sudan Kusini na Brazil, joto kali lisilowahi kushuhudiwa nchini Kenya na Pakistan, au ukosefu wa maji nchini Chad na Ethiopia, hali mbaya ya hewa inazisukuma jamii ambazo tayari ni dhaifu kufikia ukingoni.
 
“Duniani kote, hali mbaya ya hewa inaweka usalama wa watu katika hatari kubwa zaidi. Inavuruga upatikanaji wa huduma muhimu, inaharibu nyumba na vyanzo vya maisha, na inalazimisha familia – nyingi ambazo tayari zilikimbia vurugu – kukimbia tena,” amesema Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi na mkuu wa UNHCR.
 
“Hawa ni watu ambao tayari wamepitia machungu makubwa, na sasa wanakabiliwa tena na mateso na uharibifu uleule. Wako miongoni mwa wanaoathirika zaidi na ukame mkali, mafuriko yenye maafa, na mawimbi ya joto yasiyowahi kutokea, ilhali wao ndio walio na rasilimali chache zaidi za kuweza kupona,” amesema Grandi.
 
Licha ya changamoto zilizopo, UNHCR inasisitiza kwamba suluhisho yanawezekana. Jamii za watu waliolazimika kuhama na zile zinazowapokea zinaweza kuwa nguvu kubwa ya ustahimilivu, lakini ni ikiwa tu zitajumuishwa katika mipango ya kitaifa ya tabianchi, zitaungwa mkono kupitia uwekezaji maalum, na kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Hata hivyo, mipango mingi ya kitaifa ya tabianchi bado inawapuuza wakimbizi na watu wengine waliolazimika kuhama, pamoja na jamii zinazowapokea.
Mkazi mmoja huko Les Cayes nchini Haiti akikarabati paa la nyumba yake lililoharibiwa na kimbunga Melissa kilichokumba ukanda wa Karibea
© UNICEF/Patrice Noel
Mkazi mmoja huko Les Cayes nchini Haiti akikarabati paa la nyumba yake lililoharibiwa na kimbunga Melissa kilichokumba ukanda wa Karibea

COP30: UN Women yataka Mpango Madhubuti wa Utekelezaji wa Usawa wa Kijinsia (GAP)

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women limesema COP30 lazima ipitishe Mpango wa Utekelezaji wa Usawa wa Kijinsia (GAP) ulio thabiti, wenye ufadhili wa kutosha na unaowajibika, ili kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unabaki kuwa kiini cha hatua za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 
“Mabadiliko ya tabianchi si jambo lisilo na jinsia,” UN Women inaonya kupitia taarifa iliyochapishwa leo kwenye wavuti wake, ikisisitiza kwamba wanawake na makundi yaliyotengwa ndio wanaokumbwa zaidi na athari kali za migogoro ya tabianchi. Shirika hilo linasema kuwa GAP imara ni muhimu si tu kwa ajili ya haki, bali pia kwa suluhisho bora za tabianchi.
 
Sarah Hendriks, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa UN Women, ameonya kwamba “kushindwa kupitisha GAP madhubuti kutarejesha nyuma juhudi za usawa wa kijinsia na haki za binadamu,” na hivyo kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi.”
 
Beatrice Nabwire Okumu kutoka Busia akiwa na mtoto wake nje ya hema lao baada ya kukumbwa na mafuriko. Yeye ni mnufaika wa msaada wa lishe kutoka UNICEF Kenya.
© UNICEF
Beatrice Nabwire Okumu kutoka Busia akiwa na mtoto wake nje ya hema lao baada ya kukumbwa na mafuriko. Yeye ni mnufaika wa msaada wa lishe kutoka UNICEF Kenya.
Mpango wa kwanza wa Utekelezaji wa Usawa wa Kijinsia, uliopitishwa mwaka 2017, ulisaidia kuingiza mitazamo ya kijinsia katika juhudi za kimataifa za tabianchi — kuanzia hatua za kupunguza athari, kuhimili mabadiliko, hadi ufadhili na teknolojia. Katika COP30, UN Women inazitaka serikali kuchukua hatua zaidi — kushughulikia mizizi ya ukosefu wa usawa, kuhakikisha ufadhili wa kutosha, na kulinda haki na uongozi wa wanawake katika maamuzi kuhusu tabianchi.
 
Ili kuimarisha uwajibikaji, UN Women kwa ushirikiano na Taasis ya Kaschak kwa Haki ya Kijamii kwa Wanawake na Wasichana leo imezindua Tathmini ya Usawa wa Kijinsia na Sera za Tabianchi (Gender Equality and Climate Policy Scorecard), inayopima juhudi za nchi 32 kuunganisha usawa wa kijinsia katika mipango yao ya kitaifa ya tabianchi.
 
Matokeo yanaonyesha kwamba ingawa mataifa mengi yanatambua madhara yanayokumba wanawake mbele ya mabadiliko ya tabianchi, ni mataifa machache yanayotambua mchango wao muhimu katika suluhisho za tabianchi.
 
UN Women inasema kwamba COP30 ni wakati wa kihistoria wa kuthibitisha tena kwamba usawa wa kijinsia si suala la pembeni, bali ni nguzo kuu ya hatua za tabianchi zenye ufanisi, jumuishi na zenye haki.
Washiriki wakiwasili siku ya kwanza ya COP30 huko Belém, Brazil.
© UNFCCC/Kiara Worth
Washiriki wakiwasili siku ya kwanza ya COP30 huko Belém, Brazil.

Yatarajiwayo

Miongoni mwa matokeo makuu yanayotarajiwa katika COP30 ni kupitishwa kwa Lengo la Kimataifa la Uhimilivu (GGA), ambalo litaweka malengo mahsusi ya kulinda jamii kupitia mifumo ya tahadhari za mapema, kuimarisha riziki na kuboresha makazi salama — hatua muhimu katika kupunguza uhamaji unaosababishwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Malengo haya yanaendana na kazi za IOM, ambapo mwaka 2024 pekee shirika hilo liliwasaidia idadi ya watu zaidi ya 875,000 kupona kutokana na majanga, na kuunga mkono zaidi ya jamii 100,000 zilizokumbwa na majanga, mishtuko ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, kwa lengo la kuwawezesha kujiandaa vyema na changamoto za baadaye.

Aidha, Mpango wa Mpito wa Haki unalenga kuhakikisha kuwa kadri nchi zinavyohamia kwenye nishati safi, wafanyakazi na jamii wanapata ajira zenye staha, ulinzi wa kijamii na njia salama za uhamaji. Wakati huo huo, Mfuko Mpya wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu unakusudia kuelekeza rasilimali kwa jamii zilizo hatarini, ili ziweze kujenga upya maisha yao kwa heshima na uthabiti.

Kwa kuwa maamuzi yatakayofikiwa mjini Belém yataathiri maisha kwa miaka mingi ijayo, ushiriki wa IOM katika mkutano wa COP30 unaongozwa na lengo kuu moja: kuhakikisha kuwa watu walioko mstari wa mbele wa janga la mabadiliko ya tabianchi hawasahauliki.