Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majiji ya kisasa pamoja na kukumbatia teknolojia izingatie watu

Bogotá, Kolombia, ilichaguliwa na UN-Habitat kama mji rasmi mwenyeji wa Siku ya Miji Duniani 2025-tukio kuu la Umoja wa Mataifa juu ya ukuaji endelevu wa miji.
© Bogota Mayor's Office/Cristian Martinez
Bogotá, Kolombia, ilichaguliwa na UN-Habitat kama mji rasmi mwenyeji wa Siku ya Miji Duniani 2025-tukio kuu la Umoja wa Mataifa juu ya ukuaji endelevu wa miji.

Majiji ya kisasa pamoja na kukumbatia teknolojia izingatie watu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Dunia leo ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majiji, majiji ya kisasa pamoja na kukumbatia teknolojia yametakiwa kuhakikisha yanazingatia zaidi watu ili wengine wasiachwe nyuma au kutengwa na maendeleo hayo.

Maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Majiji, kimataifa yanafanyika katika jiji la Bogota, makao makuu ya Colombia huko America ya Kusini.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa wanashiriki kwa namna mbalimbali safari hii wakijikita katika kuhamasisha majiji ya kisasa kuwazingatia watu zaidi.

“Kila jiji linapaswa kuwa mahali pa fursa kwa wote. Lakini katika dunia ya leo, watu wengi wameachwa nyuma.”

Ndivyo anavyouanza ujumbe wake, Annaclaudia Rossbach, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani, UN Habitat.

Anasema, takriban watu bilioni tatu wanaishi katika makazi yasiyofaa. Zaidi ya bilioni 1.1 wanaishi katika makazi holela na mabanda. Zaidi ya milioni 300 hawana makazi kabisa. Masuala haya mara nyingi hayazingatiwi katika mipango ya “miji ya kisasa.”

Bogotá, Kolombia, inatambuliwa kama kiongozi katika mipango mahiri ya jiji, ikilenga mabadiliko ya kidijitali, uhamaji, na uendelevu wa miji.
© Bogota Mayor's Office/Cristia
Bogotá, Kolombia, inatambuliwa kama kiongozi katika mipango mahiri ya jiji, ikilenga mabadiliko ya kidijitali, uhamaji, na uendelevu wa miji.

Kiongozi huyo wa UN Habitat anaendelea kueleza kwamba wakati teknolojia inasonga mbele kwa kasi, zaidi ya watu bilioni 2.7 bado hawajaunganishwa mtandaoni. Hakuna cha “usasa” kuhusu jiji linalowaacha watu nyuma.

Majiji yeye usasa lazima yawe yenye kuzingatia watu. Teknolojia inapaswa kuwahudumia wananchi, na si kinyume chake, anasisitiza Bi Rossbach akiongeza kuwa, “kwa kutumia zana sahihi za kidijitali kutoka ramani za kijiografia hadi ufuatiliaji wa data na mifumo ya tahadhari za mapema  tunaweza kuokoa maisha, kulinda haki za ardhi, na kupanua upatikanaji wa makazi na huduma mijini.

Teknolojia ina maana tu pale inapobadilisha maisha ya kila siku: pale familia inapopata maji safi, mwanafunzi anapoweza kusoma mtandaoni, au jamii inapokuwa tayari kukabiliana na mafuriko au wimbi la joto lijalo.

Siku hii ya Miji Duniani ni fursa ya kufikiria upya maana halisi ya “usasa” katika maendeleo ya mijini. Jiji lenye usasa linaloweka watu katikati linatumia teknolojia kuboresha ubora wa maisha ya watu.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake mahususi kwa siku hii ya kimataifa ya majiji duniani anasisitiza hayo akisema

Katika dunia yetu inayozidi kuwa ya kidijitali, teknolojia inabadilisha maisha ya mijini. Kutoka kwenye mifumo ya onyo la mapema hadi ramani za kijiografia na majukwaa yanayohusisha wananchi zaidi, zana za kidijitali zinaweza kuboresha huduma za msingi, kuimarisha ustahimilivu, na kuunda maeneo ya kijani kwa wote. Lakini ubunifu lazima ufungue pengo sio kuupanua.

Anaeleza kwa hivi sasa, janga la makazi duniani na ukuaji wa makazi ya kiholela unawaacha mabilioni ya watu bila makazi yanayofaa. Mji wa kweli wa kisasa unaweka watu kipaumbele hasa wale walio katika mazingira magumu zaidi.

Katibu Mkuu Guterres anafafanua kuwa katika Siku ya Kimataifa ya Majiji Duniani, tunasherehekea serikali za mitaa na kitaifa zinazofanya kazi na wakazi ikiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kama washiriki katika kuunda mustakabali endelevu wa mijini.

Miji ni injini za fursa. Tunapoweka watu katikati, ubunifu wa kidijitali unaweza kusaidia kuendesha usawa na uendelevu kwa wote.

Mtazamo wa mji wa Bogotá, Kolombia.
World Bank/Dominic Chavez
Mtazamo wa mji wa Bogotá, Kolombia.

Jaribio Kubwa la Bogotá

Bogotá, jiji lililojulikana kwa ubunifu wa mijini, limepata sifa ya kimataifa kwa kuunganisha teknolojia na ushirikishwaji wa wananchi.
 
Kuanzia TransMilenio mfumo wake wa mabasi ya haraka unaotambulika duniani  hadi Ciclovía, mpango unaogeuza barabara kuwa maeneo yasiyo na magari kila Jumapili kwa ajili ya jamii, jiji hili limefafanua upya jinsi usanifu wa miji unavyoweza kuimarisha uhusiano wa kijamii na uendelevu.
 
Kwa Elkin Velásquez, Mkurugenzi wa Kanda wa UN-Habitat kwa Amerika ya Kusini na Karibe, Bogotá ni mfano bora unaoonesha jinsi takwimu na majadiliano yanavyoweza kuunda mustakabali bora.
 
“Maadhimisho ya kimataifa hapa yatakuza mazungumzo ya kimataifa kuhusu miji yenye teknolojia inayoweka watu mbele  ambapo teknolojia inaboresha ubora wa maisha na kuimarisha uhusiano wa kijamii,” anasema.

Kulisikiliza Jiji

Miongoni mwa wazungumzaji wakuu jijini Bogotá ni Carlo Ratti, mbunifu, mhandisi, na mkurugenzi wa Maabara ya MIT Senseable City nchini Marekani, ambaye pia ni msimamizi wa Venice Architecture Biennale ya mwaka 2025.
Bogotá, mji mkuu wa Colombia
© Unsplash/Delaney Turner
Bogotá, mji mkuu wa Colombia
 
Bwana Ratti, mmoja wa wataalamu wakuu duniani kuhusu ubunifu wa miji, anaamini kuwa miji inapaswa kusonga mbele zaidi ya dhana ya “jiji la kisasa” (smart city) kuelekea kile anachokiita “jiji linalohisi” (senseable city).
 
“Sipendi sana neno ‘smart city’,” anasema Bwana Ratti. “Mara nyingi linamaanisha mfumo wa juu kwenda chini unaoendeshwa na teknolojia pekee. Miji inapaswa kuwa, kabla ya yote, kuhusu watu yenye mwitikio, jumuishi, na inayoweza kubadilika. ‘Jiji linalohisi’ hutumia teknolojia si kwa ajili ya teknolojia yenyewe, bali kusikiliza na kuhudumia wananchi wake vyema.”
 
Kwa Bwana Ratti, Bogotá inaakisi roho hiyo. “Kwa muda mrefu imenivutia kama jiji linaloongoza katika ubunifu wa mijini,” alisema. “Miradi kama TransMilenio na Ciclovía imekuwa mifano ya kimataifa ya kujifunza.
 
“HIyo inaonesha jinsi hatua za ndani, zinapopanuliwa na kukubalika, zinavyoweza kubadili mwelekeo wa miji.”
 
Kimsingi, Bwana Ratti anaamini kwamba katika enzi ya dharura ya hali ya hewa na mabadiliko ya kidemografia, “kitendo cha kishujaa zaidi kinaweza kuwa ni kutokujenga kabisa  au kujenga kwa njia tofauti.” Kama mbadala, anapendekeza kuweka kipaumbele katika kutumia upya, kukarabati, na kubadilisha majengo yaliyopo.
 
“Na ikiwa kweli unahitaji kujenga katika maeneo mapya, jifunze kutokana na mantiki ya asili. Kwa upande wa nishati na mzunguko wa maisha, mti bado ni mwerevu zaidi kuliko jengo lolote tunaloweza kubuni,” amehitimisha.