Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN aeleza wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka kwa mapigano El Fasher, Sudan

Mwanamke mmoja aliyefukuzwa kutoka makazi yake anapitia majivu na vitu vilivyochomwa katika kambi moja nchini Sudan baada ya vita na moto, akikazia mgogoro wa kibinadamu.
© UNICEF/Mohammed Jamal Mwanamke anapekua mabaki yaliyoteketezwa ya makazi yake katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Darfur, Sudan.

Katibu Mkuu wa UN aeleza wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka kwa mapigano El Fasher, Sudan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameelezea wasiwasi wake mkubwa kufuatia kuongezeka kwa mapigano ya kijeshi mjini El Fasher, jimbo la Darfur Kaskazini, nchini Sudan.

Taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa usiku wa tarehe27 Oktoba 2025 kwa saa za New York marekani na msemaji wake, Stéphane Dujarric, imesema kuwa kwa zaidi ya miezi kumi na nane, wakazi wa El Fasher na maeneo ya jirani wamekuwa wakikabiliwa na mateso makubwa huku makundi ya Wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) yakizingira mji huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mamia ya maelfu ya raia wamekwama bila njia salama za kupokea misaada ya kibinadamu, huku utapiamlo, magonjwa na vurugu vikiendelea kupoteza maisha ya watu kila siku.

Mwanamke anayeitwa Amani amembeba mtoto wake mchanga akiwa ameketi na watoto wengine wawili katika makazi ya muda huko Tawila, Kaskazini mwa Darfur, Sudan.
© UNICEF/Mohammed Jamal

“Katibu Mkuu amelaani vikali ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na uvunjaji wa haki za binadamu unaoripotiwa kufanyika El Fasher, ikiwemo mashambulizi holela dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, mashambulizi ya kibaguzi na unyanyasaji wa kimwili.” Amesema Dujarric

Ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mzingiro huo, na kuhimiza upitishaji wa misaada ya kibinadamu kwa haraka, kwa usalama na bila vizuizi, ili kuwafikia wote wanaohitaji msaada.

Katibu Mkuu pia ameelezea hofu yake kubwa kuhusu uingizwaji unaoendelea wa silaha na wapiganaji kuingia Sudan, jambo linalochochea hali ya hatari zaidi nchini humo. Ametaka hali hiyo ikome mara moja.

Aidha, amesisitiza tena wito wake wa kusitishwa kwa mapigano mara moja, akiyataka makundi ya wanamagambo wa Jeshi la Sudan (SAF) na RSF kuanza mazungumzo ya dhati na Mjumbe wake Maalum kwa Sudan, Ramtane Lamamra, ili kuchukua hatua za haraka na za maana kuelekea suluhisho la mazungumzo.