Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Melissa ni tishio Carribea ,watoto milioni 1.6 wako hatari: UNICEF

Jumuiya za Visiwa vya Karibea zilikabiliana na Kimbunga Melissa, ambacho tayari ni dhoruba ya Aina ya 4 na kinatarajiwa kuimarika zaidi. (picha ya faili)
© UNICEF/Roger LeMoyne
Jumuiya za Visiwa vya Karibea zilikabiliana na Kimbunga Melissa, ambacho tayari ni dhoruba ya Aina ya 4 na kinatarajiwa kuimarika zaidi. (picha ya faili)

Kimbunga Melissa ni tishio Carribea ,watoto milioni 1.6 wako hatari: UNICEF

Tabianchi na mazingira

Wakati Kimbunga Melissa kikitarajiwa kuleta mvua kubwa na upepo mkali katika eneo la Carribea, takriban watoto milioni 1.6 wako hatarini, huku familia katika nchi za Jamaica, Haiti na visiwa jirani zikijiandaa kwa mafuriko, maporomoko ya ardhi na uharibifu mkubwa kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.

Kwa sasa kimbunga hicho kipo katika ukali wa daraja la 4 na kinajongea taratibu katika Bahari ya Cariibea, huku kikitarajiwa kuimarika hadi daraja la 5, kikiwa na upepo unaoendelea wa angalau maili 157 kwa saa ambazo ni takriban km 252 kwa saa.

Nchi mbalimbali katika eneo hilo, ikiwemo Jamaica, Haiti, Cuba na Jamhuri ya Dominika, zinatarajiwa kukabili siku kadhaa za hali mbaya ya hewa, huku wakiogopa kwamba miundombinu inaweza kushindwa kuhimili na huduma muhimu kuathirika.

Jitihada za kupunguza athari

UNICEF inasema “Kila jitihada za kujiandaa kwa kuwasili kwa kimbunga ni muhimu ili kupunguza madhara na vifo katika jamii zilizo hatarini zaidi, hasa katika maeneo kama Karribea.

“Visiwa vidogo daima vinakabiliwa na hatari kubwa zaidi kutokana na matukio makali ya tabianchi,” amesema Roberto Benes, Mkurugenzi wa Kanda ya Amerika Kusini na Carribea wa UNICEF.

Ameongeza kuwa “UNICEF inasaidia kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kutabiri na kujkabiliana na dharura zinazohusiana na tabianchi na kutoa huduma muhimu kwa watoto. Huu ni msingi wa kulinda wale wanaohitaji zaidi msaada.”

Maandalizi na hatua za kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake yameweka vifaa vya kuokoa maisha mapema, ikiwa ni pamoja na vifaa vya usafi, tembe za kusafisha maji, vifaa vya matibabu na misaada ya fedha kusaidia familia zilizo hatarini.

UNICEF inasema Haiti, tani 450 za chakula zimeshafikishwa mapema na misaada ya fedha imetolewa kwa kaya 9,500 katika mkoa wa kusini ili kupunguza athari za kimbunga. Takriban vifaa 3,400 vya usafi, bidhaa zisizo za chakula na makazi kwa kaya 44,000 pamoja na vifaa vya matibabu kwa watu 11,000 vimeshafikishwa.

Jamaica, Shirika la Chama cha Msalaba Mwekundu na mamlaka za nchini humo wamechukua hatua mapema, wakiandaa makazi ya dharura na kuhifadhi vifaa vya msaada kwa watu takriban 165,000 katika manispaa zilizo hatarini, ikiwa ni pamoja na Saint Elizabeth, Clarendon, Saint Catherine, Kingston, Saint Thomas na Portland.

Jamii Zinajiandaa kwa athari

Shirika hilo la kuhudumia watoto limesema jamii tayari zinakabiliwa na mvua kubwa na upepo mkali, na watabiri wa hali ya hewa wameonya kuwa mafuriko yanaweza kuzidi yale yaliyosababishwa na Kimbunga Beryl miezi 16 iliyopita, ambacho kilisababisha uharibifu mkubwa wa kifedha na miundombinu.

Mafuriko yanatarajiwa kuwa makubwa katika maeneo ya chini, pwani na makazi yasiyo rasmi, huku mvua kubwa ikitarajiwa kusababisha maporomoko ya ardhi katika maeneo ya milima.

Shirika hilo limeongeza kuwa Bandari, viwanja vya ndege na miundombinu muhimu pia inaweza kuathirika, na kufanyahatua za dharura kuwa changamoto.

Ripoti pia zinasema kuhusu vifo na majeruhi. Haiti, watu watatu wamepoteza maisha na mmoja kujeruhiwa vibaya katika maporomoko ya ardhi katika sehemu ya magharibi ya mji mkuu Port-au-Prince. Kifo pia kimeripotiwa katika Jamhuri ya Dominika.

Hatari Zinazoongezeka kwa Karibiani

Katika muongo uliopita, takriban watu milioni 11, wakiwemo karibu watoto milioni nne, waliathirika moja kwa moja kila mwaka na majanga katika Ukanda wa Amerika ya Kusini na Carribea, kwa mujibu wa UNICEF.

Wakati kimbunga kinakaribia, mamlaka za kitaifa zinawahimiza wananchi kufuata miongozo ya usalama, kuhama maeneo hatarishi na kutafuta makazi salama.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kuratibu na serikali na washirika, yakisisitiza ulinzi wa watoto na watu walio hatarini zaidi.