Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Herufi moja tu ya uongo: Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kukomesha uhalifu wa mtandaoni

Maafisa wa polisi nchini Kambodia wakifuatilia matukio ya uhalifu wa mtandaoni kwenye mtandao.
© UNODC/Laura Gil
Maafisa wa polisi nchini Kambodia wakifuatilia matukio ya uhalifu wa mtandaoni kwenye mtandao.

Herufi moja tu ya uongo: Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kukomesha uhalifu wa mtandaoni

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Fikiria hivi: unatembelea tovuti unayoijua ya duka lako la vifaa vya ujenzi la karibu yako. Kila kitu kinaonekana sawa, muundo uleule, jina la chapa lilelile, na mfumo uleule wa kutumia.

Unaweka oda yako, unalipa, na baadaye tu ndipo unatambua jambo dogo: herufi moja tu kwenye anwani ya tovuti ilikuwa tofauti.

Ndivyo ilivyo rahisi kuingia kwenye mtego wa wahalifu wa mtandaoni. Ukiwa na bahati, kiasi kilichopotea ni kidogo, na benki yako inachukua hatua haraka kurejesha fedha na kutoa kadi mpya. Lakini si kila mtu huwa na bahati hiyo: katika nchi nyingi, kurejesha fedha zilizoibwa ni jambo lisilowezekana.

Hatua moja tu kutoka kupoteza kila kitu

Mwanasheria wa masuala ya kufilisika ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa idadi inayoongezeka ya watu inalazimika kutangaza kufilisika baada ya kupoteza pesa kutokana na uhalifu wa mtandaoni.

Kituo cha kazi ya ulaghai kilitelekezwa baada ya kuvamiwa na polisi Manila
UN News/Daniel Dickinson
Kituo cha kazi ya ulaghai kilitelekezwa baada ya kuvamiwa na polisi Manila

Mtu yeyote anaweza kuwa mwathirika wa shambulio la mtandaoni popote pale alipo na kila mtu anastahili ulinzi na msaada.

Wakati katika baadhi ya nchi, matendo ya uhalifu wa mtandaoni bado hayajajumuishwa wazi kisheria kama “uhalifu wa mtandaoni,” na taratibu za ushirikiano wa kimataifa bado ni dhaifu, uhalifu wa mtandaoni wenyewe unazidi kukua kwa kasi.

Kile kilichokuwa mashambulio madogo yaliyofanywa na wahalifu binafsi, sasa kimegeuka kuwa operesheni kubwa zinazoendeshwa na mitandao ya wahalifu walioandaliwa.

Mtandao na teknolojia mpya, ikiwemo akili unde (AI), vinawaruhusu wahalifu kufanya mashambulio haraka zaidi, kwa kiwango kikubwa, kuwafikia waathiriwa duniani kote, na kutekeleza uhalifu bila ushiriki mkubwa wa binadamu.

Kuanzia mashambulio ya moja kwa moja ya kiotomatiki, picha bandia zinazotengenezwa kwa teknolojia ya “deepfake,” hadi programu hatarishi na kampeni za ulaghai (phishing) zinazotumiwa vibaya kupitia AI matumizi mabaya ya teknolojia mpya yanatia changamoto mifumo ya jadi ya uchunguzi na udhibiti wa uhalifu wa mtandaoni.

Aina za uhalifu

Aina ya uhalifu wa mtandaoni iliyoenea zaidi leo ni “phishing”,  ulaghai unaowafanya waathiriwa kufichua nywila au taarifa zao za kifedha kupitia tovuti au barua pepe bandia, kama ile ya duka lako la vifaa vya ujenzi.

Hata wahalifu wasio na uzoefu sasa wanaweza kutumia ujumbe wa udanganyifu unaoaminika.

Katika miaka ya hivi karibuni, mabilioni ya mchanganyiko wa majina ya watumiaji na nywila zilizoibiwa zimeonekana kwenye mtandao wa giza (“dark web”). Taarifa hizi zinatumika katika mashambulio yanayojulikana kama credential stuffing, majaribio ya kuingia kiotomatiki kwenye maelfu ya tovuti kwa wakati mmoja.

Ukurasa mpya dhidi ya uhalifu wa mtandaoni

Huenda ukurasa huu wa historia ya kidijitali ukakaribia kufungwa.

Mwezi Desemba 2024, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni mkataba wa kwanza wa kimataifa kuhusu haki ya jinai katika kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

Kupitishwa kwa waraka huu kulikuwa matokeo ya miaka mitano ya majadiliano kati ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, kwa ushiriki wa wataalamu, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu, na sekta binafsi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, aliuita kupitishwa kwa Mkataba huo kuwa “hatua muhimu” katika juhudi za kimataifa za kuhakikisha usalama mtandaoni.

Mnamo Oktoba 25, mkataba huo utafunguliwa kwa kutiwa saini katika hafla rasmi mjini Hanoi, Viet Nam, na utaanza kutumika siku 90 baada ya kuridhiwa na nchi 40.

Simu ya rununu, ushahidi katika oparesheni ya kupambana na uhalifu mtandaoni Kusini-mashariki mwa Asia, imetengwa kwa ajili ya uchunguzi.
© UNODC/Laura Gil
Simu ya rununu, ushahidi katika oparesheni ya kupambana na uhalifu mtandaoni Kusini-mashariki mwa Asia, imetengwa kwa ajili ya uchunguzi.

Majibu ya pamoja kwa tishio la pamoja

Waraka huu mpya unaweka mfumo wa pamoja wa kimataifa wa kupambana na uhalifu wa mtandaoni. Unaleta ufafanuzi wa pamoja, viwango vya uchunguzi, na mifumo ya kusaidia waathiriwa ikiwemo fidia, urejeshaji wa mali, na kuondolewa kwa maudhui haramu.

Nchi zitatekeleza hatua hizi kulingana na sheria zao za kitaifa lakini ndani ya misingi iliyokubaliwa kimataifa. Na huenda, kupitia mkataba huu, enzi mpya ikaanza  enzi ambayo herufi moja tu mbaya kwenye anwani ya tovuti haitakugharimu kila kitu tena.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inaongoza majibu ya Umoja wa Mataifa dhidi ya uhalifu wa mtandaoni kwa kutoa mafunzo na msaada kwa nchi kote duniani.

Shirika hilo lililoko Vienna linatumia utaalamu wake maalum katika mifumo ya haki ya jinai kutoa msaada wa kiufundi katika kuzuia na kuongeza uelewa, marekebisho ya sheria, kuboresha uwezo wa vyombo vya sheria, ushirikiano wa kimataifa, msaada wa uchunguzi wa kisayansi, pamoja na ukusanyaji wa takwimu, utafiti na uchambuzi kuhusu uhalifu wa mtandaoni.