Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa: Vijana na watumishi wa UN Tanzania watoa kauli zao
Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa: Vijana na watumishi wa UN Tanzania watoa kauli zao
Kila mwaka ifikapo tarehe 24 mwezi Oktoba, dunia huadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa, ikiashiria kuanzishwa kwa shirika hili mnamo mwaka 1945. Mwaka huu, maadhimisho hayo yana mvuto wa kipekee huku UN ikiadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, chini ya maudhui yasemayo, “Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa: Kujenga Mustakabali Wetu kwa Pamoja - Ishara ya Matumaini kwa Ushirikiano wa Kimataifa."
Siku hii ni ukumbusho wa wajibu wa kila mmoja kuendeleza maono ya shirika hili. Katika kumulika hili, Sabrina Saidi wa idhaa hii amezungumza na mwakilishi wa vijana pamoja na mmoja wa watumishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu umuhimu wa siku hii, wakiwa katika ofisi za UN Tanzania jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Vijana wana wajibu wa kuendeleza maono ya UN
Suzane Sylvester, Mwenyekiti wa Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (YUNA Tanzania), amemueleza Sabrina Saidi siku hii ina maana gani kwake;
“Maadhimisho ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa ni kumbukumbu ya historia ya amani, umoja na matumaini kwa dunia yote. Siku hii inanigusa, kwa sababu inatukumbusha wajibu wetu kama vijana kwenye kuendeleza maono ya Umoja wa Mataifa yaani haki za binadamu, usawa, maendeleo endelevu kwa dunia yote. Sisi kama vijana wa Kitanzania, tuna wajibu wa kuendeleza kazi njema ya Umoja wa Mataifa hasa kwa vitendo ambavyo vinaleta maendeleo chanya kwenye jamii zetu, nchi yetu na dunia kwa ujumla.”
Akielezea namna YUNA inavyowezesha vijana wa Kitanzania kuwa sauti na sehemu ya ajenda ya UN, Suzane amesema kuwa YUNA Tanzania ina programu mbalimbali zinazoshirikisha vijana, ikiwemo Jukwaa la Vijana la Kimataifa la Umoja wa Mataifa Tanzania (TIMUN).
“Kupitia programu ya TIMUN, YUNA imekuwa ikishirikisha vijana ndani ya Tanzania, pamoja na nje ya Tanzania, nchi mbalimbali za bara la Afrika, Ulaya pamoja bara la Asia, kwenye kushiriki kama wanachama wa Umoja wa Mataifa. Wanachangia, na kutoa mapendekezo ya suluhisho ya changamoto mbalimbali zinazokabili nchi wanachama wa Umoja huo. Hii imepelekea vijana mbalimbali kupata uzoefu na kujifunza masuala ya uongozi, diplomasia, uwajibikaji, pamoja na kuwa wabunifu kwenye maendeleo endelevu.”
Amani yatiliwa mkazo kama nguzo ya maendeleo endelevu
Kwa upande wa watumishi wa UN, Fausta Luila, dereva kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi nchini Tanzania (UNOPS), ametoa kauli yake kuhusu siku hii hisia,
“Siku hii kwangu ni fursa ya kipekee, kwani ninajisikia vizuri kuwa sehemu ya watu wanaochangia uwepo wa amani, upatikanaji wa haki, na usalama duniani kote. Ujumbe wangu katika siku hii ya leo, tuendeleze amani, na tuidumishe katika jamii yetu.”
Fausta amehitimisha kwa kusema kuwa jukumu lake kama dereva ni kuhakikisha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanafika salama katika maeneo ya miradi ili kutekeleza majukumu yao na kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Siku ya Umoja wa Mataifa ni kiashiria cha matumaini, ikikumbusha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za dunia na kujenga mustakabali bora kwa wote.