Baraza la Usalama lajadili changamoto ya misaada na usitishwaji mapigano Gaza
Baraza la Usalama lajadili changamoto ya misaada na usitishwaji mapigano Gaza
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo jijini New York kujadili masuala ya Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina ambapo Ramiz Alakbarov, Naibu Mratibu Maalum wa kanda hiyo, ametoa taarifa ya hali katika Baraza hilo.
Kikao hiki kinakuja wakati maendeleo ya makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano Gaza yanapungua na mahitaji ya kibinadamu yanapoongezeka baada ya vita vya miaka miwili, huku njaa ikibaki kuwa tishio katika baadhi ya sehemu za eneo hilo.
Wajumbe huenda wakajadili pia maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ yaliyotolewa jana yanayothibitisha wajibu wa Israel kuruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa msaada kisheria chini ya sheria za kimataifa.
Kutumia fursa ya kihistoria kumaliza mgogoro wa Palestina na Israeli
Mratibu Maalum Msaidizi kwa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati Ramiz Alakbarov akitoa taarifa mbele ya wajumbe wa Barazala Usalama amesema “Hali Gaza bado ni hatarishi”
Bwana Ramiz amekaribisha makubaliano yaliyoafikiwa tarehe 9 Oktoba kulingana na mpango wa hoja 20 wa Rais Trump, akiuita ni matumaini kwa siku zijazo zilizo bora kwa watu wa Palestina na Ukanda mzima.
Ameongeza kuwa “Baada ya miaka miwili ya vita vilivyoharibu kila kitu na mateso yasiyo na kifani kwa binadamu, sasa tuna fursa ya kufunga ukurasa wa sura mbaya katika historia ya mgogoro wa Palestina na Israeli na kuunda njia ya kuelekea zama zijazo zilizo na haki na amani,”.
Lakini pia ameonya kuwa “hali bado ni mbaya na hatarishi na huu sio wakati wa kubweteka ni wa kuhakikisha usitishaji huo wa mapigano unakuwa wa kudumu.”
Wito kwa pande zote Kuheshimu makubaliano
Bwana Ramiz Amezitaka pande zote kuheshimu ahadi zao chini ya makubaliano na kufikia mapatano haraka kwa ajili ya utekelezaji wa hatua inayofuata.
“Utulivu wa kudumu wa eneo hili utategemea kuheshimu ahadi hizi,” amesisitiza, akizihimiza pande zote kuepuka kwa gharama yoyote kurudi kwenye migogoro. Pia ametaka kurudishwa mara moja kwa mabaki ya mateka waliokufa.
Mratibu huyo Maalum Msaidizi pia amesisitiza “umuhimu wa kupeleka msaada mkubwa wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ili kukidhi mahitaji makubwa ya wananchi, bila kujali wanapoishi.”
Israel lazima izingatie sheria za Kimataifa
Kiongozi wa Kamati ya Kutekeleza Haki zisizopingika za na Kutochukuliwa za Watu wa Palestina Coly Seck amekaribisha Mkutano wa Amani wa Gaza wa Sharm el-Sheikh kama mwanzo wa uponyaji baada ya miaka miwili ya mateso makubwa.
Amesisitiza kuwa makubaliano ya usitishaji mapigano lazima yawe ya kudumu na yasiyoweza kubadilishwa. Israel lazima izingatie sheria za kimataifa.
Amekosoa vurugu zinazofanywa na Israel na upanuzi wa makazi ya Walowezi katika Ukingo wa Magharibi, akitaka yondolewe kama inavyotakiwa na Baraza la Usalama, na akirejelea Tamko la New York kama ramani ya njia ya suluhisho la mataifa mawili.
“Lazima tuhakikishe masharti yamewekwa ili Wapalestina na Waisraeli waweze kuishi pamoja kwa amani,” amesisitiza.
Israel: Kabla ya madarasa Gaza kufunguliwa, Hamas lazima iondoke
“Mara nyingi Israel imefanya kile ambacho wengi walidhani hakiwezekani,” alisema mwakilishi wa kudumu kwenye Umoja wa Matifa wa nchi hiyo
Danny Danon akibainisha kuwa mateka wote waliokuwa hai wako salama nyumbani, mabaki ya mateka 15 waliopoteza yamerudishwa, na “Hamas imelazimishwa kukubali mkataba ambao ilikuwa imeukataa tangu mwanzo.”
Hata hivyo, ameongeza tusifanye makosa kwa “Hamas tayari imevunja mkataba wa usitishaji mapigano,” akionesha kuwa iliahidi kurudisha miili ya waliopoteza maisha ndani ya saa 72 na bado haijafanya hivyo. “Wajua kabisa na tunajua wanajua wapi watu wetu waliopoteza maisha wako, wanakataa tu kuchukua hatua.”
Ameonesha kifaa cha uhalisia pepe na kuwaomba waliohudhuria “waondoe miwani na waone kilicho kweli kinachoendelea leo, kwa sababu kabla ya madarasa kufunguliwa au nyumba moja kujengwa ukweli mmoja lazima utimizwe amesema ambao ni “ Hamas lazima iende, Hamas lazima iondoe silaha.”
Palestina: Usitishaji mapigano lazima udumu kupuuza wanaotaka ushindwe’
“Tulijua kuwa usitishaji mapigano ndio njia pekee ya kusonga mbele kumaliza machafuko,” alisema naibu mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Majed Bamya.
Ameongeza kuwa ngawa kuna sababu nzuri za kuwa na shaka kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo, “kazi yetu sio kuwa watazamaji wakati mambo yanaposambaratika.” Usitishaji mapigano lazima uvumilie na kuwapuuza wale wanaotaka ushindwe, amesisitiza, akishukuru Misri, Qatar, Uturuki na Marekani kwa juhudi zao za kuingilia kati.
Hakuna usalama wa Israeli unaoweza kutokea kwa gharama ya maisha na haki za Wapalestina, amesisitiza, akinukuu Katiba ya Marekani kwamba watu wote wana haki sawa za “maisha, uhuru na kutafuta furaha.”