Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD: Jukwaa jipya la Sevilla linalolenga kutatua mgogoro wa madeni duniani limezinduliwa

Wafanyakazi katika kiwanda huko Laos wanakusanya bidhaa za kielektroniki kwa ajili ya kuuza nje.
© ADB/Ariel Javellana
Wafanyakazi katika kiwanda huko Laos wanakusanya bidhaa za kielektroniki kwa ajili ya kuuza nje.

UNCTAD: Jukwaa jipya la Sevilla linalolenga kutatua mgogoro wa madeni duniani limezinduliwa

Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa jipya lililopatiwa msaada na Umoja wa Mataifa limezinduliwa leo  Jumatano Sevilla kusaidia nchi zinazoendelea kutoka kwenye mzigo wa madeni yasiyodhibitika ambayo yamewaacha zaidi ya watu bilioni tatu duniani wakiishi katika uchumi unaolazimisha kutumia zaidi kwa malipo ya madeni kuliko afya au elimu.

Jukwaa la Sevilla kuhusu  madeni litalenga kukuza ukopaji wa haki, marekebisho ya haraka na mageuzi ya muda mrefu ya mfumo wa fedha baada ya vita.

Kwa mujibu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo UNCTAD jukwaa hilo ambalo limeandaliwa na Uhispania na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa, limeundwa kuhakikisha mgogoro wa madeni unaendelea kuwa kipaumbele cha kimataifa huku ahadi thabiti zilizotolewa kwenye Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4) uliofanyika Juni mjini Sevilla zikitafsiriwa kuwa hatua za dhahiri.

Janga la deni
UNCTAD
Janga la deni

Mazungumzo kuhusu madeni

UNCTAD imesema serikali, mawaziri wa fedha na wakopeshaji kutoka nchi zilizoendelea na zinazoendelea wataungana katika kile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anachokiita “mazungumzo ya kimataifa juu ya madeni” yanayolenga kuhakikisha haki ya kifedha na kuhakikisha mkopo unafanya kazi na si kwa dhidi ya uchumi wa nchi zinazoendelea.

Akizungumza katika uzinduzi wa jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema “Nchi zinazoendelea zinatumia dola trilioni 1.4 kila mwaka kwa huduma ya kulipa madeni.”
Ameongeza kkuwa “Na watu bilioni 3.4 wanaishi katika nchi zinazotumia zaidi fedha kwa malipo ya madeni kuliko afya au elimu. Nchi haziwezi kamwe kuhitajika kuchagua kati ya kulipa madeni au kuhudumia wananchi wake.”

Ahadi ya hatua

Jukwaa jipya pia litaunga mkono Ahadi ya Sevilla, ramani ya kipaumbele iliyokubaliwa kwenye mkutano wa FFD4 ya kufanya fedha za kimataifa ziwe za haki zaidi na endelevu.

Hati hiyo ilieleza mipango ya kupunguza gharama za ukopaji, kuwezesha marekebisho ya madeni kwa wakati na kwa usawa, na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.

Pia ilianzisha jukwaa la wakopaji, lililozinduliwa Sevilla mwezi Julai, kusaidia nchi zilizo na madeni mengi kuratibu jitihada zao, kushirikiana ujuzi wa kisheria na kiufundi, na kuongeza sauti yao katika mfumo ambao kwa muda mrefu umedominwa na wakopeshaji wakubwa.

Kutoa matokeo kwa wananchi

Kwa mujibu wa UNCTAD mchakato wa Sevilla ukijumuisha Ahadi na Jukwaa la Hatua unaakisi wasiwasi unaoongezeka kwamba madeni yanayopanda yanaingilia maendeleo kuelekea utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Zaidi ya nchi 60 zinazoendelea sasa zinatumia angalau asilimia 10 ya mapato ya serikali kwa malipo ya riba ya madeni, huku nyingi zikikabiliwa na kupungua kwa upatikanaji wa mikopo nafuu.

Chini ya mfumo mpya, UNCTAD inasema nchi zitashirikiana kuunda kanuni za pamoja kwa ukopaji na ukopeshaji wenye uwajibikaji, kuimarisha mifumo ya kuzuia migogoro na kuchunguza mageuzi ya mfumo wa madeni wa kimataifa ambao kwa muda mrefu umeonekana kuwa wa zamani na uliogawanyika.

“Jukwaa la Sevilla kuhusu madeni litaleta haki ya kifedha inayohitajika na inayostahiliwa na watu na nchi,” amesema Bwana Guterres akiongeza kuwa “Umoja wa Mataifa unajivunia kuwa sehemu ya juhudi hii, na ninamshukuru Waziri Cuerpo na Serikali ya Uhispania kwa jitihada zao zisizo na kipimo.”