UN yatoa wito wa kufungua mipaka yote ya Gaza kuepuka njaa inayoongezeka
UN yatoa wito wa kufungua mipaka yote ya Gaza kuepuka njaa inayoongezeka
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo yamerejea kusisitiza wito wake wa kutaka mipaka yote kuingia Gaza ifunguliwe ili kuingiza kiwango kinachohitajika na misaada ya kuokoa maisha na kuepuka baa la njaa linaloongezeka.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linasema lina chakula cha kutosha kumlisha watu wote wa Ukanda wa Gaza kwa miezi mitatu, lakini linaonya kuwa hatua za dharura zinahitajika kufungua mipaka yote, hasa kaskazini mwa eneo hilo lililoharibiwa, ambapo njaa ilitangazwa mwezi Agosti.
Wiki moja baada ya usitishaji wa mapigano, WFP inapeleka takriban tani 560 za chakula kila siku Gaza.
“Makubaliano ya usitishaji mapigano yamefungua dirisha dogo la fursa, na WFP inafanya kazi kwa haraka na ufanisi kuongeza msaada wa chakula na kufikia familia ambazo zimekumbwa na kizuizi, kufurushwa makwao na njaa kwa miezi mingi,” amesema Abeer Etefa, Afisa Mkuu wa Mawasiliano wa Kanda na Msemaji wa WFP kwa Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki.
Vituo vitano vya chakula vimefunguliwa
Etefa amethibitisha kuwa usambazaji wa chakula, wafanyakazi na mitandao vimeandaliwa. “Kwa chakula wastani wa tani 560 kila siku, bado hatufikii mahitaji yote, lakini tunaendelea kufika kwa wenye uhitaji,” amesema.
Kwa sasa, vituo tano vya chakula vipo na vinapatikana kwa wanawake na watoto. “Lengo letu ni kupanua hadi vituo 145 vya chakula kote Gaza kutoka vitano hadi 145, hiyo ndicho kiwango tunacholenga,” ameongeza.
Mipaka yote lazima ifunguliwe
Mashirika ya kibinadamu yanatoa onyo kuwa upatikanaji salama na endelevu ni muhimu kudumisha na kupanua operesheni.
Kwa sasa, mipaka miwili tu imefunguliwa, na barabara za kaskazini bado zimefungwa, jambo linalopunguza sana usambazaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na njaa.
“Mizigo ya misaada inapaswa kusafirishwa kutoka mipaka ya kusini hadi kaskazini,” amesema Etefa. “Lakini barabara zimezibwa na kuharibiwa. Hii ni kizuizi kikubwa kwa usafirishaji.”
Hadi sasa, hakuna usambazaji wa chakula umefanyika Gaza City, isipokuwa vyakula vya lishe kwa watoto, wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.
OCHA yawataka Israel kufungua mipaka ya kaskazini
Akizungumza Geneva, Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na masuala ya Dharura (OCHA), amesema mipaka ya kaskazini bado imefungwa kwa sababu mamlaka za Israeli hazijafungua.
Ameongeza kuwa hata baada ya kufunguliwa, ukarabati mkubwa wa barabara na kuondoa mabomu yasiyolipuka unahitajika kabla ya kutumia njia hizo salama.
“Ni muhimu sana kufungua mipaka hii kaskazini, kwani hapo njaa ndipo ilipoenea zaidi,” amesisitiza Laerke.
Kauli yake imefuatia ziara ya Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu , Tom Fletcher kwenye mpaka wa Rafah, ambapo ameomba Israel kufungua mipaka zaidi kuwaruhusu wakimbizi wengi kupata misaada, kama ilivyokubaliwa katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya 11 Oktoba 2025.
WFP tayari na tani 57,000 za chakula, inalenga kuongeza hadi 170,000
WFP imesema kwa sasa ina tani 57,000 za chakula zilizohifadhiwa nchini Misri, Jordan na Israel, tayari kusafirishwa Gaza.
Shirika hilo linakusudia kuongeza hadi tani 170,000 za chakula cha kutosha kwa watu 1.6 milioni kwa miezi mitatu.
Etefa amesema msaada wa wafadhili tayari umeanza, lakini amesisitiza uhitaji wa ufadhili wa kudumu.
Amesema “Zaidi ya miezi mitatu, tunahitaji kuendelea kudumisha usambazaji ili kuwa na angalau chakula cha miezi mitatu kila wakati.”
Ili kushughulikia hali ya njaa, maelfu ya malori ya misaada yanahitajika kila wiki. Kwa mujibu wa OCHA, malori 950 yameingia Gaza tarehe 16 Oktoba, ikijumuisha malori manane ya mafuta na malori matatu ya gesi.
Takriban 1/3 ya malori haya yamepangwa kupitia mifumo ya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, Wapalestina kote Gaza bado wanakabiliwa na upungufu wa chakula, maji safi na vifaa vya matibabu, huku eneo lote likiharibiwa na hali ya usalama kuwa hatarishi.